Singo Kigaila. |
Huku
kukiwa na madai kuwa Chadema inahusika na matukio ya kula njama za
utekaji na kuteka, kupiga na kuua watu, chama hicho kimekuja juu na
kukanusha madai hayo.
Pamoja
na kukanusha, kimemwomba Rais Jakaya Kikwete aunde tume huru ya
kimahakama kuchunguza matukio yaliyotokea ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mafunzo na
Oganaizesheni wa chama hicho, Singo Kigaila, alisema walishamwomba Rais
aunde Tume lakini akadai ombi hilo halijatekelezwa hadi sasa.
Mkurugenzi
wa Usalama wa Chama hicho, Wilfred Lwakatare anashitakiwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwa madai ya kula njama za
kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky.
Kigaila
alisema kuna wanachama wa vyama vingine vya siasa wamekuwa wakipita
katika kampeni ya uchaguzi zinazoendelea Nachingwea, Lindi wakikituhumu
chama hicho kuhusika na mauaji.
Alitaja
baadhi ya matukio hayo, kuwa ni pamoja na kuuawa kwa Yohana Mpinga
kwenye vurugu za Ndago, Singida; kumwagiwa tindikali kwa kijana Musa
wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo Igunga, Tabora na kuuawa kwa
Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Daud Mwangosi.
Pia
matukio ya kutekwa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari,
Steven Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Absalom Kibanda.
Kigaila
alisema upo ushahidi wa kuwapo ushirika wa baadhi ya watumishi wa
vyombo vya Dola waliopewa mafunzo ya kuua na kutumia silaha, tindikali,
kutesa, kuteka, kuumiza na hata namna ya kutumia sindano kuua kwa sumu.
Alidai
kuwa mara kadhaa wamekuwa wakitoa ushahidi wa silaha zinazomilikiwa na
CCM, ambazo zimepelekwa katika kambi za Ulemo, Singida; Nzega na Uyui
baada ya kuingizwa nchini bila kibali.
"Tunamtaka
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama atwambie ni nani
alitoa ruhusa kwa CCM kuwa na kikundi cha kijeshi na kumiliki silaha
ambazo zimekuwa zikitumiwa na vijana wake kudhuru watu," alihoji.
Kigaila
alitoa madai hayo, huku uchunguzi uliofanywa na kamati iliyoundwa na
TEF na Baraza la Habari Tanzania (MCT), ukionesha kuwa baadhi ya
waliohojiwa walidai kuwa Chadema imepewa mafunzo maalumu kutoka nje ya
jinsi ya kutesa watu na hata kuwaua na kusingizia vyombo vya Dola kuwa
vinahusika.
Walisema
hilo linafanywa makusudi ili kuonesha kuwa Serikali imeshindwa kulinda
watu wake na hivyo wananchi waichukie na kuiondoa madarakani.
No comments:
Post a Comment