Friday, April 19, 2013


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya akionyesha kitabu alichokiandika kwa wabunge wakati akichangia Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Uratibu na Mahusiano kwa mwaka wa fedha 2013/14, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi. Picha na Pamela Chologola.
Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu),Profesa Mark Mwandosya ametoa majibu kwa wanaoisakama Idara ya Usalama wa Taifa akilieleza Bunge kuwa ni muhimu ikatafutwa kamati itakayokuwa inajadili masuala ya idara hiyo na si bungeni.
Profesa Mwandosya alisema hayo bungeni jana wakati akijibu hoja za baadhi ya wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2013/14.
Juzi wakati wa kuwasilisha hoja kambi rasmi ya upinzani bungeni,iliitaka Serikali kuwachukulia hatua maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa–Ikulu ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu vya utekaji na utesaji watu wanaoonekana kuikosoa Serikali. Madai hayo yalitolewa bungeni na msemaji wa kambi hiyo, kuhusu bajeti ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma,Profesa Kulikoyela Kahigi katika hotuba ambayo awali ilizua mvutano wa mambo gani yasomwe na yapi yabakiwe.
Hata hivyo katika kikao hicho hotuba hiyo iliamriwa iahirishwe kwa muda,hadi kamati ya kanuni ikutane na kutoa uamuzi wa baadhi ya mambo yanayotaja majina ya watumishi wa usalama wa taifa na mengine yaliyoko mahakamani yaondolewe.
Akizungumzia hali hiyo, Mwandosya alisema anashangazwa na watu wanaozungumza kuhusu usalama wa taifa kama vile ni ndugu zao au marafiki kitu ambacho si sawa.
“Usalama wa Taifa hauwezi ukawa unazungumzwa tu hivi hivi, inatakiwa kuwe na kamati ya kuujadili kama ilivyo kwa nchi za wenzetu Marekani, Uingereza katika mashirika yao kama FBI na MI6,”alisema Profesa Mwandosya na kuongeza:
“Usalama wa taifa hauwezi ukazungumzwa hapa kuna sehemu ya kuzungumzia kwani kuzungumza hapa ni sawa na kujianika, usalama hauwezi kuwa wa kutoa kucha watu kwani utakuwa huo si usalama bali ni uhalifu.”
Wakati huo huo, Mbunge wa Longido, Michael Laizer amependekeza Bunge la sasa livunjwe ili Serikali itangaze uchaguzi mpya kutokana na wabunge wengi kutojua wajibu wao.
Mbali na hilo, mbunge huyo amevitaka vyama vya siasa vyenye wabunge kukutana na wabunge wao na kujadiliana namna bora ya kulifanya Bunge liwe na heshima mbele ya Watanzania.
“Hapa hakuna mtu anayestahili kuitwa mbunge, maana sioni mwenye heshima hiyo”, alisema Laizer.
Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...