Majid Mjengwa.
MWANDISHI wa safu katika magazeti
mbalimbali nchini, Majid Mjengwa amekamatwa na polisi kwa tuhuma za
kuhusika na tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.
Habari zilizoufikia mtandao huu jana mchana na baadaye
kuthibitishwa na polisi zinasema Mjengwa alikamatwa muda wa asubuhi na
kwamba alikuwa akihojiwa na makachero wa jeshi hilo hadi alasiri
kuhusu tukio la kuteswa kwa Kibanda.
Msemaji Mkuu wa Polisi Advera Senso alisema kwamba:
“Ni kweli kwamba tunaye, tunaendelea kumhoji, tunachoomba ni
kwamba mtupe nafasi ili tufanye kazi yetu na kukiwa na jambo lolote
tutawajulisha.”
Hata
hivyo, Senso hakuwa tayari kueleza kwa undani muda aliokamatwa Mjengwa
wala sababu za kukamatwa na kuhojiwa kwake, lakini chanzo chetu ndani
ya Jeshi la Polisi kilithibitisha kwamba pamoja na mambo mengine
kuhojiwa kwake kulihusu uteswaji wa Kibanda.
Jumatatu wiki
hii, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini, Issaya Mngulu
alisikika akizungumza na Kituo cha Radio One cha Dar es Salaam kwamba
kesho Jumatatu (April 15, 2013) polisi watatoa taarifa rasmi ya hatua
waliofikia katika upepelezi wa kesi ya Kibanda.
Kwa upande wake Mia Mjengwa ambaye ni mke wa Mjengwa, alisema
mumewe alipata wito kutoka polisi makao makuu Alhamisi na kwamba juzi
Ijumaa alisafiri kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam kuitikia wito
huo.
“Ninachojua ni kwamba aliitwa kwenda polisi
na leo (jana) alinipigia simu kama saa 7:00 mchana na aliniarifu
kwamba yupo polisi, sasa tangu wakati huo sijaongea naye tena na wala
simu zake hazipatikani,” alisema Mia na kuongeza: “Kwa hiyo mimi kwa
kweli sifahamu kwamba anahojiwa kwa sababu gani.”
Taarifa za kukamatwa kisha kuhojiwa kwa Mjengwa ambaye pia ni
mmiliki wa Mjengwa Blog, zimekuja siku chache tangu msaidizi wake
katika Blog hiyo, Joseph Ludovick akamatwe, kuhojiwa kisha kufikishwa
mahakamani kwa tuhuma za ugaidi.
Ludovick
alifikishwa mahakamani pamoja na Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Willifred Lwakatare wakikabiliwa na
tuhuma za ugaidi na kupanga kumteka Mhariri Mtendaji wa Mwananchi,
Dennis Msacky.
Kuteswa Kibanda.
Machi 5, mwaka huu saa 5.30 usiku, Kibanda
ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Kampuni ya New Habari
(2006) Ltd, alinusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana
nyumbani kwake kisha kupigwa na kujeruhiwa vibaya.
No comments:
Post a Comment