WANASIASA
wawili vijana ambao wamekuwa katika vita ya maneno na Naibu Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, kuhusu
madai waliyoyatoa kuwa anawindwa kuuawa, mwishoni mwa wiki iliyopita,
walijitokeza katika ofisi za Mtanzania Jumatano na kufunua siri na
matukio ya utesaji raia na mauaji ya kinyama ambayo yamekuwa yakitokea
kwa nyakati tofauti kwenye shughuli za kisiasa hapa nchini.
Wanasiasa
hao, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba, ambao wamefanya mahojiano ya
ana kwa ana na gazeti hili, walisema madai waliyoyatoa awali kuwa Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, alitajwa na kada wa chama hicho,
Ben Saanane, kuwa alimtuma amuwekee sumu Zitto kwa lengo la kumuua ni ya
kweli kwa sababu walimkamata akiwa nayo na alikiri jambo hilo na
kumuomba msamaha Zitto kwa kitendo hicho.
Walidai,
mbali na tukio hilo ambalo baada ya kuliibua limegusa hisia za wengi na
kuzua mijadala mikali, yapo matukio mengine ya mauaji na majaribio ya
kuua, ambayo yamekuwa yakiratibiwa na Chadema kwa lengo la
kuwagombanisha wananchi na Serikali.
Shonza
na Mwampamba walisema kuwa wapo tayari kutoa ushuhuda wa matukio hayo
mahali popote watakapohitajika na walipoulizwa ni kwa nini baada ya
kubaini kuwepo kwa vitendo hivyo, hawakutoa taarifa kwa vyombo vya
sheria au taasisi za ulinzi na usalama, walisema mlengwa mkuu katika
matukio hayo ambayo yalikuwa yakisababisha madhara kwa watu wengine
hakuwa tayari siri hiyo kuanikwa.
Akizungumza
mbele ya jopo la waandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania Jumatano,
Shonza alidai kuwa, yeye na baadhi ya vijana wenzake waliokuwa wakiunda
kundi Patriotic Movement, walimnasa Saanane akiwa na sumu hiyo katika
Hotel ya Lunch Time iliyoko Ubungo, Dar es Salaam, ambao awali alidai
kuwa ni dawa ya Panya, lakini alipobanwa alieleza kuwa ilikuwa sumu
ambayo hakuitaja jina na kwamba alipewa na Dk. Slaa ili amuwekee Zitto
kwa sababu alikuwa akimsumbua sana.
Alisema, sumu ingewekwa kwenye kinywaji cha Zitto akiwa katika kikao hicho, lakini hatua yake ya kutohudhuria ndiyo iliyomuokoa.
Shonza
alisema, baada ya Saanane kukiri kuwa alitumwa na Dk. Slaa kumuwekea
Zitto sumu, walimtaarifu wakati akiwa Marekani na aliporudi alikutana na
kuwataka jambo hilo wasilifikishe polisi kwa sababu lingekivuruga chama
na kwamba kwa sababu alikwishawajua wabaya wake atajilinda.
Alimtuhumu
Zitto kwa kuficha ukweli na kumwita kiongozi mwoga, huku akimuonya kuwa
iwapo ataendelea na tabia ya kukanusha ukweli atamuumbua hadharani kwa
sababu anamjua vizuri.
“Ameongea
hayo kwa sababu ana tabia ya kushindwa kuthibitisha kuwa ana uwezo wa
kujiongoza yeye mwenyewe pamoja na wengine. Mtu wa maslahi Zitto,
anatafuta huruma ya Chadema baada ya kuona amepukutika kisiasa kutokana
na kukosa msimamo kiuongozi na hawezi tena kutetea wanyonge, ni mtu
mwoga.
Mnapokuwa
kwenye mapambano yeye yuko tayari kurudi nyuma, lakini huruma hiyo
asitegemee kuipata Chadema, labda akubali kushaurika na kubadilika kama
kweli anataka kutetea maslahi ya wanyonge,” alisema Shonza.
Aidha,
Shonza alimshambulia pia Saanane kwa kudai anakataa ukweli anaojua, kwa
sababu tukio la kukamatwa kwake akiwa na sumu lilitokea akiwa mbele ya
zaidi ya mtu mmoja na kusisitiza kuwa kada huyo wa Chadema anatumika na
viongozi wa juu wa chama hicho kuwashughulikia baadhi ya wanachama
wasiotakiwa.
Katika
hili, Shonza alidai zaidi kuwa Saanane ni mtu hatari kwa sababu ndiye
aliyeanzisha kundi la PM7, ambalo lilikuwa na lengo la kumpindua Mbowe
kutoka kwenye wadhfa wake wa uenyekiti, lakini baadaye aliwageuka
wenzake na kusababisha kufukuzwa katika chama.
“Saanane
alikuwa anatumika kutuingiza mkenge. Alianzisha kile alichokiita
mapinduzi, Patriotic Movement (PM7), lengo lilikuwa Pindua Mbowe, sisi
hatukujua.
Tulikuwa
saba katika PM7, Saanane alifanikiwa kutuchezea akili na alikuja na
'nick names' (majina bandia) yake. Mimi akaniita Benanzir Bhuto, Mchange
akaitwa Mdude, Mwampamba- Joseph Kony, Zitto- Dogo kama tulivyozoea
kumuita na yeye mwenyewe akajiita Cobra, wapo na wengine sikumbuki
vizuri majina yao hapa.
Sisi
vijana wakati mwingine tunatumika vibaya, sisi hatukujua ana ajenda
yake, tulivyoshtuka akatukana na ndiyo yakatokea hayo yaliyotokea,”
anazidi kueleza Shonza.
Mwampamba
Kwa
upande wake Mwampamba ambaye aliandamana na Shonza katika ofisi za
Mtanzania Jumatano, alidai kushangazwa na hatua ya Zitto kukanusha kauli
ya Shonza iliyokuwa ikieleza namna Saanane alivyokamatwa akiwa na sumu
aliyokuwa ametumwa kumuwekea Zitto.
Alisisitiza
kuwa, Zitto anajua mipango inayopangwa ndani ya Chadema kwa ajili ya
kummaliza na alimtaka aache tabia ya kufunika kombe ili mwanaharamu
apite, kwa sababu inaweza kuwa na athari mbaya kwake.
“Zitto
anajua mpango mzima wa kutaka kumalizwa kwa sumu na Ben Saanane, baada
ya kutumwa na Dk. Slaa kwa sababu tulimwambia na alithibitisha mwenyewe
pale Saanane alipomuomba msamaha, sisi ndiyo tulimbana Saanane hadi
akaeleza ukweli wa mipango yao ya mauaji.
“Leo
namshangaa anavyojikomba eti haamini kuwa anaweza kuuawa na hao jamaa.
Lakini kwa Ben Saanane, namtaka atambue kuwa Ludovick alipokamatwa
alikanwa na Dk. Slaa wakati ndiye alikuwa kijana wake mpenzi, sasa na
yeye ipo siku atakimbiwa.
“Zitto
anatakiwa aache tabia ya kufunika funika mambo, ajue nimemwokoa sana
katika mambo mengi, mfano mauaji ya Morogoro yaliyopangwa na Chadema
yalimlenga Zitto, alikuwa atolewe kafara. Yule muuza magazeti aliyepigwa
risasi Morogoro akafa, siku hiyo ilikuwa afe Zitto,” alidai Mwampamba.
Alipoulizwa
ni kwanini viongozi wa Chadema wanataka kumuua Zitto, alisema ni kwa
sababu ya uhusiano mbaya baina yake na vigogo hao ambao chanzo chake ni
hatua ya kutaka kugombea urais na kutomuunga mkono Dk. Slaa katika
harakati zake za kuwania urais mwaka 2010.
“Zitto
hana uhusiano mzuri na viongozi wa juu wa Chadema. Nia yake ya kutaka
kugombea urais hawaipendi, inawaudhi sana na amekuwa akitofautiana nao
kwa mambo mengi, anajua kuwa anawindwa ndiyo maana hata oparesheni za
M4C hashiriki.
“Mimi
nilikuwa Chadema na nilikuwa karibu sana na Zitto, najua nini kilikuwa
kinaendelea juu yake na najua baadhi ya mambo ya Chadema. Ninaijua
mipango ya mauaji ya Chadema. Zitto aliwahi kuwekewa sumu Bagamoyo
wakati wabunge wa chama hicho walipokuwa kwenye mkutano wao huko.
“Alinusurika kufa. Alipona baada ya sumu hiyo kutolewa mwilini mwake. Waliiflashi.” Alidai Mwampamba.
Alidai
kuwa Zitto alipata kunusurika katika ajali ya gari wakati akitokea
Bagamoyo kuelekea Iringa, baada ya gari alilokuwa akitumia kulegezwa
nati zinazofunga tairi. Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Zitto
na Mbowe kutupiana maneno makali kwenye mkutano
Kauli ya Saanane
Akizungumza
na Mtanzania Jumatano jana kupitia simu yake ya kiganjani, Saanane
alisema madai yaliyotolewa na Shonza na Mwampamba dhidi yake siyo ya
kweli, kwa sababu wanayodai kuwa walimkamata akiwa na sumu, hakuwa nao.
Alisema
kwa mujibu wa kumbukumbu zake, siku ya Desemba 5, mwaka jana, alikuwa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akikutana na wanaharakati na baadaye jioni
alikwenda harusini.
Hata
hivyo, alipoulizwa iwapo alipata kukutana na Shonza na Mwampamba katika
Hotel ya Lunch Time, Saanane alisema amepata kukutana nao mara kadhaa
kwa ajili ya kupanga mikakati ya PM7, ambayo alishiriki kuianzisha
lakini aliachana nao baada ya kubaini walikuwa wakiitumia kwa malengo
mabaya.
Mtanzania
Jumatano lilipombana Saanane aeleze mikakati waliyokuwa wakiipanga yeye
na wenzake katika PM7, alisema ilikuwa ya siri na vikao vyao vilikuwa
vya siri kutokana na hofu ya kufikiriwa vibaya na viongozi wa chama
iwapo wangebainika wanajihusisha na kundi hilo.
Alipoulizwa
kama anafahamiana na Zitto na wapi amekwishakutana naye, alisema
anamfahamu na amekuwa akikutana mara kwa mara huku akishangaa tamko lake
kwenye mitandao ya kijamii lilikokuwa likieleza kuwa, hamfahamu na hata
akimuona anaweza kupishana naye.
Hata
hivyo, baadaye Saanane aliomba anuani ya barua pepe ya Mhariri wa
gazeti hili na kumtumia barua ya kumtaka amuombe radhi kwa kuandika
habari ya uongo iliyokuwa ikieleza madai ya masharika wake
wanaomuhusisha na tuhuma za kutumwa kumuwekea sumu Zitto, pasipo
kumtafuta Zitto mwenyewe kuzungumza hata neno moja
Vituko vya Dk. Slaa
Dk.
Slaa alipotafutwa kwa simu yake ya kiganjani na kuulizwa kuhusu madai
hayo, alianza kuporomosha matusi mazito huku akilituhumu gazeti hili
kutoa nafasi ya kuandika habari zinazowagusa viongozi wa Chadema badala
ya kuandika habari za maendeleo.
“Sina
muda wa kujibu maswali hayo… hayana msingi…tuhuma hizo hazijadiliwi
kwenye magazeti……ni masuala ya kijinga…pumbavu kabisa. Acheni upumbavu
bwana. Nina mambo mengi ya msingi ya kitaifa ya kushughulikia kuliko
haya madai ya kipumbavu.” Aling’aka Dk. Slaa.
Hata
gazeti hili lilipomsihi awe mtulivu ili aweze kutoa ushirikiano,
aliendelea kufoka huku akiporomosha matusi zaidi kabla halijaagana naye
na kukata simu.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe simu yake iliita muda wote bila majibu na hata Zitto.
No comments:
Post a Comment