Friday, April 12, 2013

CAG abaini ubadhirifu mkubwa


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni, 2012 zilizowasilishwa bungeni jana mjini Dodoma. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Rajab Mbarouk Mohammed. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Dodoma. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilitolewa jana ikiweka bayana madudu mbalimbali ya ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, udhaifu katika usimamizi wa mikataba na Serikali kushindwa kutoa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 


Moja ya matatizo yaliyojitokeza ni Wizara ya Nishati na Madini kushindwa kukusanya nyongeza ya mrabaha wa madini baada ya kuongezwa kutoka asilimia tatu hadi nne.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha ripoti hiyo ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2012, CAG Ludovick Utouh alisema pamoja na kuwapo mafanikio ya kimahesabu ukilinganisha na miaka iliyopita, bado kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.

Alilishauri Bunge kuangalia upya suala la kuivunja Kamati ya Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC) na kuunganisha shughuli zake na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na mkakati wa ofisi kufanya ukaguzi wa misamaha ya kodi ambayo imeongezeka kuangalia uhalali wake.

Hata hivyo, Utouh alikataa katakata kuzungumzia deni la taifa ambalo pia limeongezeka akisema “amefanya hivyo makusudi”.

Bajeti na miradi ya maendeleo
Kwa mujibu wa CAG, imebainika kuwa kuna tatizo kubwa la Serikali kushindwa kutoa kwa halmashauri mbalimbali fedha za maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge.
Alisema Bunge lilipitisha vifungu vya fedha za maendeleo vyenye jumla ya Sh595,064,422,505 katika halmashauri 113, lakini fedha zilizopokewa ni Sh345,568,067,477 sawa na asilimia 42 tu, hivyo kufanya upungufu wa Sh249,496,355,027.

Licha ya fedha hizo kutokutolewa zote, kiwango kilichotolewa hakikutumika chote kutokana na kucheleweshwa. “Hadi mwishoni mwa mwaka, kulikuwa na baki ya fedha za miradi ya maendeleo kiasi cha Sh188,405,740,589 ambayo ni sawa na asilimia 55 ya fedha zilizotolewa na Serikali,” alisema Otouh na kuongeza: “Tunashauri bajeti iendane na shughuli zilizopangwa, kwa sasa utaratibu wa bajeti haujawa mzuri.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hata fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinazotolewa kwa wabunge hazikutumika zote. Sh2,561,882,820 zilizotengwa kwa ajili ya sampuli ya majimbo 69 zilibaki.

“Sababu ya kutokutumika ni ama halmashauri hazina utaratibu maalumu wa kutumia fedha hizo au Serikali kutoa fedha hizo mwishoni mwa mwaka,” alisema.

Udhaifu katika usimamizi wa mikataba ya madini
Katika ripoti hiyo, CAG alisema Wizara ya Nishati na Madini ilishindwa kukusanya Dola za Marekani 12,634,354 (sawa na Sh19,709,593,191) zilizotokana na ongezeko la mirabaha ya madini, baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini.

Katika iliyokuwa Wizara ya Miundombinu, ukaguzi huo umebaini kuwa madeni yake ya mwaka 2010/11 yanayofikia Sh253 bilioni yamelipwa kwa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara mwaka uliofuata wa 2011/12.

Katika kipindi hicho, CAG alisema dhamana za Serikali za jumla ya Sh578.4 bilioni zilikuwa zimeisha muda wake na hivyo kuifanya Serikali ikiwa mdhamini kuwajibika kulipa deni hilo.

Vilevile, CAG ameona kuna kodi inayopotea kutoka sekta isiyo rasmi, hivyo kuishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwatumia vizuri makatibu kata kuwatambua walipakodi kama vile wamiliki wa kumbi za harusi na mikutano.
Alishauri kuwa TRA ianze kukusanya kodi kwenye huduma za kuhamisha fedha kwa njia ya simu za kiganjani maarufu kama M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na nyinginezo.
Alisema kampuni hizo zinatakiwa kulipa kodi ya zuio ya malipo ya kamisheni inayolipwa kwa wanaofanya biashara hiyo na kodi hiyo ipunguzwe kutoka katika kodi ya mwisho itakayotakiwa kulipwa na kampuni za simu. 


Misamaha ya kodi
Ripoti hiyo ya CAG ilishauri mikataba ya madini ijadiliwe na Kamati ya Bunge inayohusika na kutoa mapendekezo kabla haijasainiwa na hati za misamaha ya kodi ziwekwe bayana kuwa ni msamaha wa muda gani, inaanza na kumalizika lini.
Alishauri pia vipengele vyote vya misamaha ya kodi vipitiwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kushauri kabla ya kusainiwa na upande husika.

Katika mwaka 2013/14, CAG ameamua kuanza kuikagua misamaha yote ya kodi kwa madhumuni ya kuangalia manufaa yake kwa uchumi wa taifa, kwa kuwa misamaha hiyo pia ni fedha za Serikali. Hesabu za TRA zimeonyesha makusanyo ya kiasi cha Sh6,703,229,704,887 ikilinganishwa na makadirio ya Sh6,456,832,630,000 na kusababisha makusanyo ya ziada ya Sh 246,397,074,887 sawa na asilimia nne ya makadirio.

Taarifa ya CAG inaonyesha mwelekeo wa misamaha ya kodi unaonyesha ongezeko kwa kiasi cha Sh789,883,259,827 sawa na asilimia 78 kutoka kiasi cha Sh1,016,320,300,000 kilichoripotiwa mwaka 2010/2011 hadi Sh1,806,203,559,827 kwa mwaka 2011/2012.

Kuvunjwa kwa POAC
Utouh alisema kitendo cha kuvunjwa kwa POAC na kuunganisha majukumu yake na PAC ni bahati mbaya kwa kuwa sababu za kuanzishwa kwake bado zipo hai kama ilivyokuwa wakati inaanzishwa na kwamba uamuzi huo hautakidhi matarajio ya wadau.

“Kamati ya PAC itazidiwa na ukubwa wa majukumu, hivyo ofisi bado inashauri kuona uwezekano wa kurudisha kamati hii hata kama itakuwa na haja ya kubadilisha jina lake,” alisema.

Spika Anne Makinda aliamua kuvunja kamati zote za Bunge kwa kuunda mpya na kuvunja nyingine.
POAC iliyokuwa chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe iliunganishwa na ile ya PAC, ambayo pia inaongozwa na mbunge huyo.

“Kamati ya PAC itazidiwa na ukubwa wa majukumu, hivyo ofisi bado inashauri kuona uwezekano wa kurudisha kamati hii hata kama itakuwa na haja ya kubadilisha jina lake,”


MWANANCHI

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...