Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
Jana, Jumatano, Aprili 10, 2013 ametia saini Kitabu cha Maombolezo cha
aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Bi. Margaret Thatcher ambaye
alifariki dunia Jumatatu wiki hii kwa ugonjwa wa kiharusi akiwa na umri
wa miaka 87.
Rais Kikwete ametia saini Kitabu hicho kwenye Ubalozi wa Uingereza katika Tanzania ulioko Jengo la Umoja mjini Dar es Salaam.
Rais
alikaribishwa kwenye Ubalozi huo na Balozi wa Uingereza katika
Tanzania, Mheshimiwa Bi. Dianna Melrose na wafanyakazi wengine wa
ubalozi huo na amekwenda moja kwa moja kutia saini kitabu hicho mara
baada ya kuwasili kwenye Ubalozi huo.
Mara
baada ya kumaliza kutia saini Kitabu hicho, Balozi Melrose amemwambia:
“Kwa niaba ya Serikali ya Uingereza na Watu wa Uingereza nakushukuru
sana Mheshimiwa Rais kwa heshima hii ya kuja kutia saini Kitabu cha
Maombolezo cha Mheshimiwa Margaret Thatcher. Waziri Mkuu wa nchi yetu
atafurahi kujua kuwa umepata muda wa kuja kuungana nasi katika
kuomboleza kifo hiki.”
Naye
Mheshimiwa Rais Kikwete amemjibu: “Kwa mara nyingine Mheshimiwa Balozi
nakupa wewe binafsi, Serikali na watu wa Uingereza pamoja na familia
ya Bi. Margaret Thatcher salamu zetu nyingi za rambirambi kufuatia
msiba huu. Bi.Thatcher alikuwa kiongozi mashuhuri. Alikuwa kiongozi
mwenye nguvu na msimamo na ndiyo maana anaheshimiwa na sisi sote.”
Bi.
Margaret Thatcher alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa miaka 11 kati
ya 1979 na 1990. Alikuwa mwanamke wa kwanza na pekee mpaka sasa
kushikilia nafasi hiyo na ndiye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza kukaa
madaraka kwa muda mrefu zaidi kuliko waziri mkuu mwingine yoyote katika
kipindi cha miaka 150.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
10 Aprili, 2013
No comments:
Post a Comment