Wabunge watano wa Chadema
jana walitimuliwa bungeni na kuamriwa kukaa nje ya Bunge kwa siku tano
kutokana na vurugu zilizotokea jana usiku.Wabunge hao ni Lissu,
Hezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi
(Mbeya Mjini) Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa
(Iringa Mjini).
Chanzo za kufukuzwa kwao ni
kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa
kutoka nje na Naibu Spika, Job Ndugai baada ya kuingilia hotuba ya
Mbunge wa Iramba Mashariki,
Mwigulu Nchemba.
Kutokana na tafrani hiyo,
Nchemba hakuweza kuhitimisha hotuba yake hivyo Ndugai alilazimika
kukatisha mkutano wa Bunge.Hata hivyo wakati akiahirisha mkutano huo,
tayari wabunge hao walikuwa wameshatolewa nje baada ya askari
kuongezwa.
Mbali na tukio hilo Lema
naye alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu viongozi wa CCM akiwamo
Rais Jakaya Kikwete kwa udini, madai ambayo Bunge limempa siku saba
kuyathibitisha.
Lema aliituhumu CCM na
Serikali yake chini ya Rais Kikwete kwa kushindwa kutatua mgogoro wa
kidini na badala yake kuwa kama analikwepa tatizo. Alionya kuwa Taifa
linapasuka kwa migogoro kutokana na viongozi wa Serikali kushindwa
kulishughulikia.
Kauli iliwanyanyua vitini
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu na Sera),
William Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Lukuvi na Jaji Werema
walisimama wakidai kuwa Lema alikuwa amemdhihaki Rais Kikwete kwa kauli
zake za kumhusisha na masuala ya udini.
Hata hivyo, Mnadhimu Mkuu wa
Upinzani, Lissu alisimama kumtetea Lema akidai hakuwa amemdhihaki Rais
bali alikuwa amemkosoa kitu ambacho kanuni za Bunge zinaruhusu.
Lema aliruhusiwa kuendelea
na hoja yake na ndipo akamtolea mfano Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira wakati alipokwenda Mwanza kutatua
mgogoro baina ya Wakristo na Waislamu kuhusu suala la kuchinja.
“Wassira akifahamu yeye
ndiye, Waziri alikwenda Mwanza na kuwaacha viongozi wa dini za Kikristo
na Kiislamu watatue wenyewe suala la kuchinja. Sasa alitaka diwani
atatue mgogoro ule?”
Baada ya
kumaliza kuchangia, Naibu Spika alitangaza kuwa Lema anatakiwa
kuwasilisha katika muda wa siku saba uthibitisho kuwa Rais anahusika na
tatizo la udini.
Serukamba
Serukamba
alipewa nafasi ya kutoa taarifa wakati wabunge walipokuwa wakilumbana
juu ya uhalali wa Msemaji wa Upinzani, Profesa Kulikoyela Kahigi
kuzungumzia bungeni masuala yaliyoko mahakamani na shughuli za Idara ya
Usalama wa Taifa.
Wakati akijiandaa kusoma
vifungu vya kukatiza hotuba ya Profesa Kahigi, alitukana tusi zito la
nguoni kwa lugha ya kimombo ambalo kwa sababu za kimaadili hatukuweza
kuliandika, kisha akaendelea kuzungumza huku baadhi ya wabunge
wakipigwa butwaa.
Hata
hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai aliyekuwa akiongoza shughuli za Bunge
wakati huo, hakutoa karipio lolote huku akimruhusu Serukamba kuendelea
kwa muda kabla ya kumkatiza na kumruhusu Mbunge wa Simanjiaro (CCM),
Christopher Ole Sendeka kuzungumza.
Ubishi
ulivyoanza
Muda mfupi kabla ya Profesa
Kahigi kuanza kusoma hotuba yake, Serukamba alisimama na kuomba
mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 68(1) akitaka isisomwe kuanzia
ukurasa wa kwanza hadi wa nne kwa kuwa unaingilia uhuru wa Mahakama...
“Ni juzi tu Akoonay (Mustapha, Mbunge wa Mbulu - Chadema),
alitukumbusha kwamba mambo hayo ni ‘prejudice’ kwa Mahakama kwa hiyo
ukiruhusu hilo Naibu Spika itakuwa ni ajabu.”
Kabla Naibu Spika hajatoa
mwongozo wake, alimtaka Profesa Kahigi kuzungumza kama anakubaliana na
Serukamba, lakini Profesa Kahigi alisema anaomba kuendelea kusoma hotuba
yake kama ilivyo
Baadaye Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika aliomba kumpa taarifa Serukamba kwamba katika
kurasa alizozitaja hakuna jambo lolote lililopo mahakamani hivyo
aangalie vizuri.
“Mheshimiwa Naibu Spika
napenda kumpa taarifa mtoa taarifa kwamba hakuna lolote lililopo
mahakamani, ukurasa wa kwanza unazungumzia Idara ya Usalama wa Taifa,
haipo mahakamani, ukurasa wa pili umemtaja Dk Stephen Ulimboka, halipo
mahakamani hivyo hakuna lolote lililopo mahakamani,” alisema.
Baada ya hapo Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
alisimama na kueleza kuwa aliyoyasema Serukamba ni kwamba hotuba hiyo
inafanya kesi iliyopo mahakamani kuwa ya kisiasa akisema... “Kifungu
cha 16 cha Sheria ya Usalama wa Taifa hakiruhusu watumishi wa Usalama
wa Taifa kutajwa humu ndani wala kuchapishwa popote.”
Naibu Spika alisimama na
kusema jambo hilo limeshajitokeza ndani ya Bunge na Akoonay
alishawakumbusha kuwa ni kuingilia Mahakama.
“Jambo hili lilishaleta
kasheshe humu ndani na ruling (uamuzi) ya hili ilishatolewa na Spika,
‘ruling’ yangu ni kwamba kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa nne, mambo
ya Dk Ulimboka, Usalama wa Taifa na Lwakatare.........,” aliishia hapo
Ndugai na kuwaruhusu Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela
Kairuki na Ole Sendeka kuzungumza.
Mdee alisema ukurasa wa
kwanza mpaka wa tatu wa hotuba hiyo hakuna sehemu jina la Lwakatare
lilipotajwa na kwamba ukurasa wa nne uliotaja jina la Lwakatare
hauzungumzii mwenendo wa kesi... “Hoja anazoleta Lukuvi atusomee hiyo
Sheria ya Usalama na atuelezee na alinganishe na kilichopo hapa.”
Mdee aliungwa mkono na Lissu
aliyesema kuwa sheria anayozungumzia Lukuvi ipo lakini haikatazi
kutajwa majina ya wanausalama ndani ya Bunge... “Ninayo hiyo sheria
hapa ya mwaka 1996, haya maneno kwamba Sheria ya Usalama inakataza
masuala ya Usalama wa Taifa kutajwa ni uchochezi. Hicho kinachoelezwa
kukataza ‘disclosure’ (kuwataja) ni huko nje na si humu ndani.”
Lissu
alisema sheria hiyo inakataza kuchapishwa majina hayo nje ya Bunge na
si vinginevyo.
Kairuki
alipingana na Lissu akieleza kuwa amepotosha kwa kuwa sheria hiyo ya
Usalama wa Taifa hairuhusu kuwataja watumishi wake bila kuomba ruhusa
kwa waziri.
“Lissu
anapotosha kwa kuwa hairuhusiwi mtu yeyote kuchapisha jina la mtumishi
wa Usalama wa Taifa bila kuomba ruhusa kwa waziri,” alisema
Kairuki.Ndipo Naibu Spika alipompa tena nafasi Serukamba na alipoanza
tu kuchangia kuliibuka maneno ya chinichini ambayo yalionekana kumkera
ndipo alipotoa neno hilo zito.
Baadaye
Ndugai alisema kwa kuwa hilo suala ni la kikanuni, anaiagiza Kamati ya
Kanuni ikutane ili tujadili suala hilo.
Katika
hotuba hiyo ambayo awali, waandishi walipata nakala yake, Profesa
Kahigi alikuwa ameandika mambo mbalimbali yanayohusu kutekwa na kuteswa
kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka na
masuala mengine yanayohusiana na kesi ya ugaidi inayomkabili Mkurugenzi
wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare.
SOURCE:;MWANANCHI
No comments:
Post a Comment