Sunday, March 03, 2013

Makamu wa Rais Dkt. Bilal Kufungua Miradi ya Maendeleo ya Ujenzi Mkoani Mara.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal atakuwa Mgeni Rasmi katika sherehe za uzinduzi wa  Miradi ya  Maendeleo inayotekelezwa na Wizara ya Ujenzi kuanzia tarehe  04/03/2013 mkoani Mara.
Pamoja na shughuli nyingine, siku ya  Jumatatu tarehe 04 Machi 2013 akiwa mkoani humo, Mhe. Makamu wa Rais  ataweka  jiwe la msingi kwa ajili ya  ukarabati wa barabara ya kutoka mpakani mwa Mkoa wa Simiyu na Mara hadi  Musoma yenye urefu wa kilomita 85.5.  Barabara ambayo ujenzi wake utawekewa jiwe la msingi ni sehemu ya Barabara ya Mwanza – Nyanguge – Makutano – Musoma ambayo ni kiungo muhimu  na nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.  Hivyo kukamilika kwake ni fursa nyingine nzuri ya kuibua uchumi wa nchi yetu na ukanda huu.
Jumanne ya tarehe 5 Machi 2013 asubuhi Mhe. Makamu wa Rais atazindua Kivuko cha Musoma kinachotoa huduma kati ya Musoma na Kinesi.  Siku hiyo hiyo mchana Makamu wa Rais ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) zilizoko eneo la Old Customs katika barabara ya Lake Side, Musoma.
Uzinduzi wa miradi hii ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya nne ya kuboresha miundombinu muhimu ya usafiri na makazi kwa wananchi wake. Aidha, uzinduzi  wa Kivuko cha Musoma (MV Musoma) kinachotoa huduma kati ya Manispaa ya Musoma na Kinesi Wilayani Rorya ni utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais baada ya kupokea ombi la Kivuko kutoka kwa wakazi wa Musoma na vitongoji vyake.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...