Askofu wa Jimbo la Moshi la Kanisa
Katoliki Tanzania, Askofu Isaac Amani Massawe amesema kuwa Tanzania
imeingiliwa na ugonjwa wa saratani wa kuvunja amani na utulivu na
Watanzania wasipobalika na kukubatia amani watajuta.
Amesema kuwa baada ya miaka 50 ya Uhuru,
Watanzania sasa wamefungua ukurasa mpya na nchi imeanza kupoteza sifa
ya kuwa nchi ya amani na utulivu.
Aidha, amesema kuwa wajibu wa watu
kuishi kwa amani siyo wajibu wa Serikali ama wa Dini ama wa Kanisa bali
ni wa kila mtu kwa nafsi yake.
Askofu Amani ameyasema hayo leo,
Alhamisi, Februari 14, 2013 wakati alipokuwa anatoa neno la shukurani
baada ya kumalizika kwa Ibada ya Mazishi ya aliyekuwa Askofu Jimbo la
Moshi, Askofu Mstahivu Amedeus Peter Msarikie katika Kanisa Kuu la
Kristo Mfalme mjini Moshi.
Askofu amewaambia mamia kwa mamia ya
waumini: “Tumefungua ukurasa mpya katika Tanzania. Baada ya miaka 50 ya
amani na utulivu sasa tumebadilika. Tanzania ya leo siyo Tanzania ya
zamani sasa tumeanza kuongozwa na misingi ya vurugu za kidini na vurugu
za kifedha.”
Ameuliza Baba Askofu Amani: “Tumeelimika
zaidi ama tumechoka amani? Tumeingiwa na saratani ya uvunjifu wa amani
na migawanyiko kwa misingi ya kidini na kifedha na mingine ya aina mbali
mbali. Njia nzuri ya kuagana na mzee wetu Askofu Msarikie ni kuishi
maisha aliyoishi yeye- maisha ya amani na utulivu. Yeye alikuwa chombo
cha amani na anapumzika kwa amani kwa sababu aliishi maisha ya amani.”
Ameongeza: “Kuishi kwa amani na utulivu
siyo suala wala wajibu wa Serikali ama wa Kanisa ama wa Dini ni wajibu
wa kila mtu kwa nafsi yake na kila mmojawetu anao wajibu wa kusali ili
kuombea amani ambayo imedumu katika nchi yetu kwa miaka mingi sana –
miaka 50 sasa lakini inaonyesha kila dalili ya kutoweka.”
Amesisitiza: “Ndugu zangu amani
hairithishwi, amani hujengwa na hulindwa. Changamoto alichotuachia
Askofu Msarikie ni kutafuta na kuilinda amani katika nchi yetu. Huwezi
kuwa mtu wa vurugu na mvunja amani na bado ukapata starehe ya milele
mbele ya Mwenyezi Mungu. Sasa ni wakati wa kulea taifa letu,
kulitengeneza upya na tumwombe Mungu atusaidie katika safari hii ndefu.”
No comments:
Post a Comment