Tuesday, October 08, 2013

UCHAGUZI UTAFANYIKA OKTOBA 27- TENGA


Leodgar-Tenga1 5ecb7
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa kupata Kamati mpya ya Utendaji ya shirikisho utafanyika Oktoba 27 mwaka huu kama ilivyopangwa.
"Wazungu wanasema ije mvua au jua, uchaguzi utafanyika. Isipokuwa tunachotaka kuhakikisha ni kuwa unakuwa uchaguzi huru na wa haki," amesema Rais Tenga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana (Oktoba 7 mwaka huu).
Amesema mchakato unakwenda vizuri kilichobaki ni revision (mapitio) na rufani, masuala ambayo yako mbele ya Kamati ya Rufani ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi.
Rais Tenga amesema lengo la hatua hizo si kuzuia watu wasigombee kwani ni lazima mambo ya msingi ikiwemo sifa za wagombea yaangaliwe, lakini kwenye haki ni lazima kuhakikisha inatendeka hata kama ni kwa mtu mmoja.
Mchakato wa uchaguzi ulivutia waombaji 58 ambapo watatu wamekata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kupinga kuondolewa na Kamati ya Uchaguzi wakati wengine wanane masuala yao yamepelekwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa njia ya mapitio (revision) ili kupata mwongozo wa utekelezaji.

HATARI....!!! VIJANA WAKAMATWA MSITUNI MTWARA NA CD ZENYE MAFUNZO YA AL-QAEDA, AL-SHABAAB

zzzzzkamanda_mtwara_ca9c9.jpg
Na Abdallah Bakari, Mtwara
POLISI mkoani Mtwara inawashikilia watu 11 kwa tuhuma za kupata mafunzo ya kijeshi msituni kwa kutumia CDs za al-Shabaab.
Tukio hilo la aina yake limetokea katika mlima Makolionga wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa ambapo pia CDs zenye mafunzo mbalimbali ya kijeshi 25 zimekamatwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen ameuambia "mtandao wa Kusini Leo" kuwa watuhumiwa hao
walikamatwa wiki moja iliyopita baada ya jeshi lake kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema: "CD hizo zilikuwa zinatoa mafunzo ya Al-Shabaab ya kuchinja watu, Mauaji wa Osama Bin Laden, Zindukeni Zanzibar, Kuandaa Majeshi, Mauaji wa Idd Amin na Mogadishu Sniper," alisema Stephen.


Monday, October 07, 2013

WASTARA APEWA MGUU WA BANDIA BURE NCHINI KENYA...!!!

STAA wa filamu za Kibongo, Wastara Juma Jumamosi iliyopita alikwea pipa kuelekea nchini Kenya ambako ana ziara ya siku nne kikazi na akiwa humo alipata fursa ya kupewa mguu wa bandia bure na wenyeji wake huku pia akiahidiwa kufanyiwa ‘check-up’ ya mwili mzima.
 
Wastara Juma.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Wastara alisema kuwa anajisikia furaha kupewa ofa hiyo kutoka kwa wadau wa tasnia ya filamu pande za Kenya ambao wamekuwa wakivutiwa na kazi zake.
“Nimepewa ofa ya mguu bandia wa bure ambao utanisaidia, pia nitafanyiwa uchunguzi wa mwili mzima pamoja na mambo mengine. Nina furaha kwa heshima hiyo niliyopewa na wadau hao na kwa msaada wao huo, Mungu atawalipa,” alisema Wastara.
Enzi za uchumba wake na marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’ walipata ajali iliyosababisha Wastara kukatwa mguu ambapo aliwekewa wa bandia. hivyo mguu huo aliopewa ni wa pili ili kama atahitaji abalishe ule wa zamani.

KAULI YA SERIKALI JUU YA MGOMO WA WASAFIRISHAJI

Picha_1_1fb96.jpg
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akisisitiza jambo kuhusu mgomo uliopangwa kufanywa na wadau wa usafirishaji nchini wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar Es Salaam
Picha_33_60d3c.jpg
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam Kamishna Suleiman Kova akieleza jinsi Jeshi la Polisi lilivyojipanga kulinda usalama ili watumiaji wa barabara wasiweze kupata usumbufu huku akisisitiza kuwa kabla ya Jeshi la polisi kuchukua hatua za kisheria ni vema vyombo vinavyosimamia usafirishaji vikachukua hatuaKushoto ni Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli
Picha_4_5579d.jpg
Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Ujenzi na Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini maelezo toka kwa Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli.
Picha Zote na Eliphace Marwa (MAELEZO)

MAGAZETI YA LEO JUMATATU OKTOBA 07, 2013

DSC 0013 193f0
DSC 0014 7b671

MTUHUMIWA'MUHIMU'WA MAUAJI YA BILIONEA AKAMATWA AKIDAIWA KUTOROKA

erastomsuya_5e7a1.jpg
Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa muhimu wa mauaji ya mfanyabiashara bilionea wa Arusha Erasto Msuya wakati akijaribu kutoroka kwenda Burundi.
Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema mtuhumiwa huyo (jina tunalo), alikamatwa juzi asubuhi mkoani Kigoma akiwa katika harakati za kutoroka kuelekea nchi jirani ya Burundi.
Mtuhumiwa huyo ndiye anadaiwa kumshawishi marehemu kwenda kukutana na wauaji wake eneo la Mijohoroni wilayani Hai Agosti 7, mwaka huu na alikwenda pamoja na marehemu hadi eneo la tukio.
Habari zinadai mara baada ya marehemu kuuawa kwa kumiminiwa risasi zaidi ya 20, mtuhumiwa huyo alitoroka kutoka eneo la tukio akitumia moja kati ya pikipiki mbili zilizotumika katika mauaji hayo.

TUNDU LISSU AMJIBU JK

siku-tundu-lisu-alipokutana-na-jk-ikulu-jijini-dar-es-salaam_f685e.jpg
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu amesema hotuba ya kila mwezi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa siku tatu zilizopita, imejaa maneno mengi ya kuambiwa hasa kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, ikiwa ni pamoja na uteuzi alioufanya wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu wa Chadema, Lissu alisema kauli zilizotolewa na Rais za kumshutumu yeye (Lissu) kuzungumza uongo bungeni, kuhusu uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba zilikuwa zakuambiwa, hazina ukweli wowote.
"Pengine rais Kikwete angesoma hotuba yangu niliyoitoa bungeni asingezungumza vile kuhusu mimi."


Katika hotuba yake, Rais Kikwete alimshutumu Lissu kwa kusema kwamba katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa Rais hakuheshimu mawazo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Rais Kikwete alisema kauli hiyo ya Lissu ni uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu huku akisisitiza kuwa Lissu alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.

Saturday, October 05, 2013

WALINZI WA MLIMANI CITY WANASWA WAKIPOKEA RUSHWA LIVE LIVE

Harufu ya rushwa! Safu ya ulinzi katika maduka ya biashara ya Mlimani City, Dar kwenye geti la kuingilia na lile la kutokea, inadaiwa kutawaliwa na rushwa ambapo walinzi wamenaswa ‘laivu’ wakipokea ‘mlungula’.
Kwa mujibu wa walalamikaji, walinzi hao wanadaiwa kujiwekea utaratibu usiyo rasmi chini ya kampuni ya ulinzi wa eneo hilo iliyotajwa kwa jina la Omega Nitro Risk Solutions ya jijini Dar ambapo ‘vijana’ wake wanatuhumiwa kutoza watu faini ya shilingi elfu kumi kwa gari ambalo mhusika wake amepoteza kadi ya kuingia na kutoka. 
 
Madai hayo yalikwenda mbele zaidi ikielezwa kuwa kumekuwa hakuna utaratibu mahususi kwenye ishu hiyo kwani baadhi ya walinzi kila mmoja hujiamulia kuchukua fedha bila mhusika kupewa risiti ya malipo. “Kuna tatizo kwenye safu ya ulinzi, huwa tunatozwa faini shilingi elfu kumi ukipoteza kadi,” alisema mmoja wa walalamikaji hao.

MUSWADA BINAFSI KUFUTA SHERIA YA MAGAZETI YA 1976

Zitto-Kabwe_839e8.jpg
Na Zitto Kabwe
Napenda kuujulisha umma kwamba leo Ijumaa tarehe 4 Oktoba, 2013 nimewasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi Bungeni kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Changamoto iliyopo ni Sheria mbadala ya vyombo vya habari baada ya Sheria ya sasa kufutwa. Hata hivyo wadau wa habari kama Baraza la Habari Tanzania wameshafanyia kazi suala hili kwa muda mrefu sana na wana mawazo kuhusu sheria mbadala. 
Nimejulishwa kuwa muswada wa sheria mpya ya habari tayari upo. Kwa hiyo katika mchakato wa kujadili muswada binafsi wa kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976 mabadiliko yanaweza kufanywa ili kutunga sheria mpya. Hatua ya kwanza ni kuifuta sheria hii kandamizi ambayo kiukweli tumechukua muda mrefu sana na baada ya madhara makubwa kufikia hatua ya muswada wa kuifuta.
Nimeamua kutumia njia za kawaida za kuwasilisha muswada na kuepuka njia ya dharura ili kujenga mazingira ya wadau wa habari kushiriki vya kutosha katika mabadiliko yanayotakiwa.

MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI OKTOBA 05, 2013

DSC 0038 be9ab
DSC 0039 6c203

RATIBA YA LIGI KUU YA UINGEREZA LEO JUMAMOSI

Premier-Leage2_7f8b6.jpg
14:45 Manchester City na  Everton
17:00 Cardiff City na Newcastle United
17:00 Fulham na Stoke City
17:00 Hull City na Aston Villa
17:00 Liverpool na Crystal Palace
19:30 Sunderland na Manchester United

Friday, October 04, 2013

HOTUBA YA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013

JKNEWCABINET_7ce8b.jpg
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013

Ndugu Wananchi;

Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa sababu nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno. Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.

Uhusiano na Rwanda

Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.

WAFUASI WA MORSI WAKABILIANA NA POLISI MISRI

131003231510_egypt_muslim_brotherhood_mb_304x171_ap_nocredit_e5ae6.jpg
Vikosi vya usalama nchini Misri vimeimarisha ulinzi katika sehemu kadhaa mjini Cairo baada ya vurugu kuzuka kutokana na makabiliano kati ya wafuasi wa Mohammed Morsi na vikosi vya usalama katika mji huo na ule wa Alexandria.
Mwandishi wa BBC mjini Cairo Quentin Sommerville anasema kuwa milipuko na milio mikuwa ya risasi imesikika katika sehemu za katikati mwa mji mkuu.
Sehemu ambazo zimezingirwa ni kama vile ambako wafuasi wa rais aliepindiliwa Mohammed Morsi waliwahi kupiga kambi baada ya Morsi kuondolewa kwa nguvu mamlakani na vikosi vya usalama mwezi Agosti katika operesheni iliyosababisha mamia kadhaa kupoteza maisha.
Pia usalama umeimarishwa karibu na medani ya Tahrir ambako waandamanaji waliokuwa wanapinga Morsi walikusanyika katika maandamano ya kumtaka ajiuzulu kabla ya majeshi kumtoa madarani miezi mitatu iliopita.
Vyombo vya habari vimeripoti kutokea ghasia zaidi katika mkoa wa Kaskazini wa Sharqiya, Mashariki mwa Giza, pamoja na Kaskazini mwa mji wa bandarini wa Alexandria.
Mamia ya watu wameuwa tangu jeshi kumuondoa mamlakani Morsi mwezi Julai.
Maelfu ya wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood pia wamezuiliwa katika miezi miwili iliopita.
Baadhi ya maafisa wakuu wa chama hicho akiwemo bwana Morsi na generali Mohammed Badie, wanazuiliwa kwa madai ya kuchochea ghasia na mauaji.
Vuguvugu hilo limelalamika na kusema kuwa maafisa wanazifanya juhudi zao dhidi yaokuonekana kama vita dhidi ya ugaidi

KABURI LA ALIYEFUFUKA LAFUKULIWA

DSCF1980 800x600 5ffda
Valence Robert, Geita
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida kaburi ambalo alizikwa mtoto Shabani Maulidi (15), ambaye anadaiwa kufariki dunia miaka mitatu iliyopita na kuonekana akiwa hai hivi karibuni, jana lilifukuliwa na viungo vya mwili wake kukutwa ndani.
Kazi hiyo iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi pamoja na Mtafiti wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Lucas Ndungulu, ilizua taharuki kwa umati wa watu waliokuwa eneo hilo, baada ya nyumba ya jirani lilipo kaburi hilo, Masanja Marwa, kubomoka ghafla wakati ufukuaji huo ukiendelea, huku mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja naye akianguka na kuzirai. 

Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Ndungulu alisema kuwa wameamua kufukua kaburi hilo ili kupata sehemu ya viungo vya mwili kwa ajili ya vipimo.
"Lengo la kufukua kaburi hili ni kutaka tupate kiungo chochote cha mwili wa marehemu ili tufanye utafiti wa kitaalamu ili tujue kama ni kweli huyu anayedaiwa kuwa ni mtoto wao ndiye," alisema.

130 WAFA MAJI WAKIJARIBU KWENDA ULAYA

wafa_maji_de7d8.jpg
Maafisa katika kisiwa kikubwa cha Sicily katika bahari ya Meditarenia wanasema kuwa wamepata maiti 130 baada ya mashua iliyokuwa imewabeba takriban wahamiaji 500 wa kiafrika kushika moto na kuzama katika kisiwa cha Lampedusa.
Boti hiyo ilikuwa safarini kuelekea Ulaya lakini ikazama katika kisiwa cha Lampedusa katika pwani ya Utaliana
Takriban miili 103 imepatikana baharini na mingine zaidi kupatikana ndani ya boti iliyozama.
Inaarifiwa abiria walijirusha baharini wakati moto ulipozuka ndani ya boti
Zaidi ya wahamiaji 150 wameokolewa.
Wengi wa wahamiaji hao walikuwa raia wa Eritrea na Somalia,kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Shughuli kubwa ya uokozi ingali inaendelea kuwatafuta manusura kwani inahofiwa mamia zaidi huenda wamefariki kutokana na ajali hiyo.
Meya wa mji huo anasema kuwa walionusurika wako hatika hali ya mshutuko na walimwambia kuwa moto mdogo uliwashwa baada ya meli kukwama na lengo lilikuwa kuitisha msaada.
Lakini alisema kuwa moto ulisambaa kupita kiasi na ikawa vigumu kuudhibiti.
Kisiwa cha Lampedusa kiko kati ya Tunisia na Sicily na kimekuwa kiingilio kikuu cha wahamiaji kuingia barani Ulaya.

Thursday, October 03, 2013

MAJAMBAZI YATEKA BASI LA ABIRIA NA KUPORA SIMU NA FEDHA.....!!!

Abiria hamsini na moja waliokuwa wakisafiri na basi la Taqwa kutoka  Bujumbura kuelekea Dar-es-Salaam wametekwa katika kijiji cha Milade wilayani Mkalama na kuporwa mali , simu na fedha zaidi ya shilingi milioni mia mbili hamsini.
Akieleza kamanda wa polisi mkoani Singida bwana Godfrey Kamwela  amesema watekaji hao waliwaamrisha abiria kushuka chini ya basi baada ya kuvunja vyoo na kuanza kuwasachi na kufanikiwa kupora simu, fedha za  kitanzania shilingi milioni tano ,dola za kimaerekani dola laki moja elfu sitini na  faranga zenye thamani ya elfu ishirini kufuatia tukio hilo kamanda Kamwela amewaomba wananchi na makampuni ya simu kushirikiana na jeshi la polisi ili kuweza kuwa kamata watu ambao wamefanya tukio hilo.

Kwa upande wake dereva la basi hilo bwana Ahamed Seif amesema gafla aliona majani barabarani na alipoangalia vizuri aliona kuna mawe makubwa  mawili  yakiwa barabarani na kushindwa  kuyakwepa ,baada ya kugonga mawe hayo magurudumu yote mawili ya mbele yalipasuka na gari  ikaserereka umbali wa mita mia moja.

MWANAMKE AFARIKI DUNIA MARA BAADA YA KUNYWA DAWA ZA KIMASAI KAMA TIBA HUKO MOSHI.

DAWA za kienyeji za Kimasai zinadaiwa kusababisha kifo kwa mkazi wa Moshi Vijijini, Restituta Alen baada ya kuzinunua kutoka kwa mfanyabiashara na kunywa.Mfanyabiashara wa dawa hizo, Lanyani Lukumay anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mwanamke huyo. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema tukio hilo lilitokea Septemba 30 saa 9.30 alasiri eneo la Marangu wilayani Moshi Vijijini.

Kwa mujibu wa Kamanda, Lukumay alimuuzia dawa za miti shamba mteja wake kisha kuzinywa na alifariki muda mfupi baadaye.
Hata hivyo haikufahamika ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.
Lukumay anauza dawa za asili ya Kimasai, ambazo ni baadhi ya mitishamba na vitu vingine, inadaiwa siku ya tukio alimpa dawa mteja wake huyo ambaye uchunguzi wa awali unaonesha alifariki baadaye, tunamhoji kujua chanzo cha kifo,”alisema.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa ya Mawenzi. Polisi inafuatilia kufahamu iwapo dawa za mtuhumiwa huyo zinatambuliwa na mamlaka zilizopo na kama anatambulika kuendesha biashara anaifanya kienyeji.
Pamoja na tukio hilo la kifo, pia polisi imetoa taarifa juu ya mtoto mchanga wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miezi sita na saba aliyekutwa amekufa akiwa katika dampo lililopo Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi. Polisi imeomba wananchi kushirikiana na polisi kubaini wahusika wa tukio hilo

MASHINE ZA TRA ZAZUA BALAA.... MBEYA WAGOMA KUZINUNUA, VURUGU ZAZUKA

9161303_orig_67cda.jpg

Mabomu ya machozi yalipigwa ili kuzuia wafanyabiashara wasilete vurugu

7024725_orig_b85b7.jpg

Maduka yakiwa yamefungwa

2503579_orig_f146a.jpg

Wafanyabiashara hao walichoma matairi ili kuwazuia polisi wasiweze kuwafikia

MAGAZETI YA LEO ALHAMISI OKTOBA 03, 2013

DSC 0011 c3260
DSC 0012 8e34e

LIGI YA MABINGWA WA ULAYA

ulaya_88499.jpg
CSKA Moskva 3 - 2 Viktoria Plzeň
Shakhtar Donetsk 1 - 1 Manchester United
Bayer Leverkusen 2 - 1 Real Sociedad
Juventus 2 - 2 Galatasaray
Real Madrid 4 - 0 København
PSG 3 - 0 Benfica
Anderlecht 0 - 3 Olympiakos Piraeus
Manchester City 1 - 3 Bayern München

KAULI YA CHADEMA KUHUSU KUFUNGIWA KWA MAGAZETI.

chadema-logo-i2 6aded
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO Idara ya Habari ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), tangu ilivyopokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa za Serikali ya CCM, kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, imeendelea kufuatilia kwa ukaribu hatua zinazochukuliwa na kauli mbalimbali zinazotolewa na pande zote mbili, serikali na wadau wa uhuru wa habari na vyombo vya habari. 
Ni wazi bila shaka yoyote kuwa kwa mara nyingine tena, serikali hii, imeendelea kutumia sheria mbaya, kutumia madaraka vibaya kufanya uamuzi mbaya, kila inapokosa hoja na uwezo wa kukabiliana na sauti mbadala au maoni kinzani.
Suala hili limekuwa dhahiri zaidi baada ya Serikali kuamua hata kuanza kuingilia uhuru wa habari na maoni kwenye mitandao ya kompyuta (on line) na pia kutishia kulifungia Gazeti la Rai, linalotolewa na Kampuni ya New Habari (2006) Limited, kwa sababu limeanza kuchapiswa kila siku.
Wakati wamiliki wa gazeti hilo wametoa ushahidi unaotokana na nyaraka za serikali hiyo hiyo iliyotoa idhini kwa chombo hicho kuchapishwa kila siku, Serikali yenyewe kwa upande wake imetoa utetezi wa ajabu juu ya tishio lake hilo ikijitetea kuwa kibali hicho kilitolewa kwa Kampuni ya Habari Corporation iliyouza hisa zake kwa Kampuni ya New Habari (2006) Limited.
Katika hili serikali inajichanganya. Hii ni dalili ya wazi kwamba uamuzi wake huo ni mwendelezo wa maamuzi ya kibabe, yasiyofanywa kwa masilahi ya Watanzania, ndiyo maana yanaanza kuipatia tabu jinsi ya kujibu na kujenga hoja za kutetea uovu wake.
CHADEMA, inapinga na itaendelea kupinga kwa kauli na vitendo, hatua hii ya serikali yenye lengo ovu dhidi ya umma wa Watanzania.

Wednesday, October 02, 2013

ZITTO KABWE AMJIBU NAY WA MITEGO...!!!

Rita Paulsen aka Madam Rita wa Bongo Star Search na Walter Chilambo tayari wameshazijibu Salamu za Nay wa Mitego na jana ilikuwa zamu ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe

Kwake mbunge huyo, Nay ni msanii wa pili wa Hip Hop anayemkubali zaidi Tanzania baada ya Roma na kwamba anakiheshimu kile alichokisema kwenye wimbo huo kwakuwa ni kazi ya sanaa.

Tazama tweets hizi.


CarolNdosi @CarolNdosi
I wonder if @zittokabwe  ever listens to hip hop..local or international..



@CarolNdosi: I wonder if @zittokabwe ever listens to hip hop..local or international..” I do. Roma is my favourite followed by Ney

VYOMBO VYA USALAMA VIKOMESHE UHALIFU, UMAFIA TANZANIA

Meno-ya-tembo_a1920.jpg
Na Daniel Mbega
UHALIFU nchini Tanzania umekuwepo kwa miaka mingi, lakini katika miaka ya karibuni umeonekana kushika kasi kuliko ilivyowahi kutokea, kiasi cha kutishia amani kwa Watanzania kuhusu usalama wa maisha na mali zao.
Kati ya Januari 2005 hadi Januari 2006 kulikuwepo na matukio ya uhalifu na ujambazi wa kutumia silaha ambapo kiasi cha Shs. 16,782,172,419 kiliporwa katika benki kadhaa za maduka ya kubadilishia fedha nchini.
Takwimu zinaeleza kwamba jumla ya wahalifu 46, wakiwemo raia 12 wa Kenya, walikamatwa katika kipindi hicho wakihusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu.


Baada ya hapo ikafuatia kasheshe kubwa ndani ya Jeshi la Polisi, sekeseke ambalo lilifanya iibuliwe orodha ya maofisa 20 wa jeshi hilo ambao wanashirikiana na majambazi katika wizi huo.
Lakini wakati huo zilikuja taarifa mfululizo zikiwatuhumu askari kadhaa ndani ya jeshi hilo ambao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu, huku wakiwa wamechuma mali nyingi ambazo haijulikani namna walivyozipata kulinganisha na mishahara yao.
Kama nilivyotangulia kusema, vitendo vya uhalifu hapa nchini vimekuwepo kwa miaka mingi, na kwa kumbukumbu zangu vitendo hivi vilianza kushika kasi mwanzoni mwa miaka ya 1980.

MAGAZETI YA LEO JUMATANO OKTOBA 02, 2013

DSC 0004 b425a

DSC 0002 b7cb1

BAADA YA KUYAFUNGIA MAGAZETI YA MWANANCHI NAMTANZANIA, SERIKALI SASA YAINYOOSHEA KIDOLE GAZETI LA RAI.

SERIKALI imeitaka kampuni ya New Habari 2006, kuacha kuchapisha gazeti la Rai kila siku na kampuni ya Mwananchi kuacha kuchapisha gazeti la Mwananchi kwenye mtandao.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Malelezo, Assah Mwamebene, alitoa onyo hilo ofisini kwake jana na kuongeza kuwa ameziandikia barua kampuni hizo, zijieleze ni kwanini zinafanya hivyo.
Tumeona gazeti la Mwananchi baada ya kufungiwa, limeendelea kuchapishwa kwenye mtandano wa intaneti kinyume na amri iliyotolewa. Vivyo hivyo kwa Rai ambayo ilikuwa ikichapishwa mara moja kwa wiki, imeanza kutoka kila siku, tunawataka warejee ratiba yao,” alisema.
Alisema endapo vyombo hivyo havitatekeleza agizo hilo na kujieleza katika ofisi yao ifikapo kesho, Serikali italazimika kuchukua hatua kali zaidi ikiwa ni pamoja na kuongeza adhabu, ikiwemo kufungia kwa muda usiojulikana na kufutiwa usajili wake.
“Umma ufahamu kuwa Serikali haikukurupuka kufungia magazeti hayo, uamuzi ulifanywa baada ya kufuata taratibu zote za msingi ikiwemo kuwasikiliza wahusika.

TAMKO LA GAZETI LA MWANANCHI BAADA YA KUFUNGIWA KUCHAPISHA HABARI KWA NJIA YA MTANDAO

Tunasikitika kuwaarifu kuwa kutokana na sababu zisizozuilika, tutashindwa kuendelea kuwaletea habari mpya kupitia tovuti yetu (www.mwananchi.co.tz) na mitandao ya kijamii ya Mwananchi kwa wakati wote ambapo uzalishaji wa gazeti la Mwananchi utakuwa umesitishwa.

Tunasikitika kwa usumbufu wowote utakaosababishwa na hali hii na tunatumaini mtaendelea kuwa nasi wakati wa kipindi 
 hiki kigumu cha mpito. Tunatarajia kurejea rasmi hewani na habari moto moto wiki ijayo, Ijumaa, tarehe 11 October.

Tunawakaribisha muendelee kusoma habari zetu za zamani (archives) kwenye tovuti ya Mwananchi na kurasa zetu za Facebook na Twitter ili mzidi kuhabarika.

Pia tunawakaribisha mtembelee tovuti zetu za www.thecitizen.co.tz na www.mwanaspoti.co.tz ambazo zitaendelea kufanya kazi kwa ufanisi, zikiwaletea habari za uhakika na kuaminika kipindi hiki ambapo Mwananchi imefungiwa.

Ahsanteni,

Wahariri.

WEMA AMWAGA MACHOZI MARA BAADA YA MAGAZETI KUMWANDIKA KUWA AMEHUKUMIWA KUNYONGWA NCHINI CHINA


C.E.O wa kampuni ya Endless Fame Film maarufu kma Wema Sepetu ameonekana kuchukizwa na kitendo cha kuchafuliwa kwa jina lake katika moja ya magazeti ya udaku ya hapa nchini.
Mapema asubuhi ya leo kupitia account yake ya Instagram mwanadada Wema alitupia picha ya gazeti hilo lililo mchafulia jina kwa kumuandika kuwa "Wema Kunyongwa China Awaomba Watanzania Wamuombee".Pia dakika chache zilizopita kupitia account yake hiyohiyo ya Instagram wema amefunguka zaidi kwa kitendo hicho cha kuchafuliwa jina na kuandika hivi ... 

ANGALIA VIDEO YA MCHINA ALIYEOTESHWA PUA KWENYE PAJI LA USO ILI IKIKUA IWEKWE BAADA YA PUA HALISI KUHARIBIKA.


Mchina aoteshwa pua nyingine kwenye paji lake la uso. Mchina huyo ambaye anatumia jina moja tu la Xiaolian, alipata matibabu ya kuunda pua ambayo itakaa badala ya pua yake halisi ambayo iliathirika na kuharibika.
Taratibu zilifanyika katika hospitali iliyoko Fuzhou huko Fujian
Mwanaume huyo mwenye miaka 22 aliharibu pua yake kwenye ajali ya gari Agosti 2012 lakini alishindwa kupata matibabu. 
Matokeo yake  pua yake ikaathirika mpaka wale madaktari wakashindwa kuirekebisha.
Hawakuwa na jinsi nyingine yeyote ila kumuotesha pua nyingine alafu kuiondoa baadae ili iwekwe pale ambapo pua halisi iliharibiwa.

Pua hiyo ilitengenezwa kwa kuweka tissue expander za ngozi kwenye paji la uso la Xiaolian.Ilikatwa kwenye shepu ya pua na ikawa imehimarishwa na cartilage iliyotolewa kwenye mbavu zake. Madaktari hao wa oparesheni wamesema kuwa pua hiyo imekua vizuri na oparesheni ya transplant itafanyika hivi karibuni

Ila mh! Kweli hii nose job! Mchina ana pua nyingine kwenye paji la uso kuireplace pua halisi iliyoharibika kwenye ajali ya gari....!!

KENYA - BILA USALAMA SOMALIA, HATUTOKI

President-Uhuru-Kenyatta3_9e43d.jpg
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa majeshi ya Kenya yataendelea kukaa Somalia hadi usalama utakapoimarishwa katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya miaka mingi.
Rais Kenyatta amesema kuwa nchi yake haitashurutishwa na magaidi walioteka jengo la maduka la Westgate kwa siku 4.
Rais Kenyatta alihutubia umati uliokusanyika kwa maombi ya pamoja ya dini mbali mbali, kwa ajili ya watu 67 waliouawa katika shambulio la Westgate.
Shambulio hilo ndio baya zaidi kuwahi kutokea nchini Kneya tangu majeshi yake yaingie nchini Somalia mwaka wa 2011.
''Hawa wauaji waliokuja kutenda ukatili wao ulio na woga hapa nchini kwetu, walikuwa wanadai kuwa wanafanya hivyo kwasababu majeshi ya Kenya yapo nchini Somalia. Nataka niwaeleze bayana kuwa, majeshi yetu yatakaa huko hadi kuwepo amani katika nchi hiyo.''

PAPA JOHN PAUL KUTANGAZWA MTAKATIFU APRILI MWAKANI

zzzzzzzzzzzzpope_25f2f.jpg
Papa John Paul II na John XXIII wanatarajiwa kutangazwa watakatifu Aprili 27 mwakani, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa sasa wa kanisa Katoliki, Papa Francis.
Taarifa ya uamuzi huo imetolewa leo kwenye mkutano wa makadinali unaoendelea mjini Vatican, ikiwa ni hatua mihimu ya kuthibitisha tangazo lake la Julai mwaka huu kwamba atawapa heshima viongozi hao wawili wa juu wa Kanisa waliopita katika karne ya 20.
Katika taarifa iliyonakiliwa kutoka kwenye gazeti la mtandaoni la Daily Mail, alisema wakuu hao wa Kanisa Katoliki duniani ambao kwa sasa ni marehemu waliweza kutumia karama zao kwa uamunifu na kuonyesha matendo makuu.
Wachambuzi wa masuala ya Kanisa hilo alieleza kwamba inaonekana umuzi huo ni wa makusudi ikiwa ni hatua ya kujaribu kuliunganisha kanisa hilo ambalo lina mkanganyiko kwa sasa.
Kila mmoja ana watu wanaomuunga mkono na wanaompinga, ambapo kwa sasa Francis anaonekana kuungwa mkono na wote wa pande zote mbili hivyo kuwa kichocheo cha kuunganisha na kufuta makovu yaliyolikumba Kanisa hilo kwa miaka ya hivi karibuni.

Tuesday, October 01, 2013

WAKAZI DODOMA WAANDAMANA KUPINGA BOMOABOMOA YA CDA




 Maelfu ya Wananchi wa Kata ya kikuyu kusini wakiandamana katika mitaa ya mji wa Dodoma kwa ajili ya kupinga kubomolewa na mamraka ya ustawishaji makao makuu  [CDA] wanaotarajia kubomoa nyumba, mapagale na misingi ya wakazi hao.

  Maelfu ya Wananchi wa Kata ya kikuyu kusini wakiandamana katika mitaa ya mji wa Dodoma kwa ajili ya kupinga kubomolewa na mamraka ya ustawishaji makao makuu  [CDA] wanaotarajia kubomoa nyumba, mapagale na misingi ya wakazi hao.

JAMAA APEWA ADHABU YA KUOSHA GARI LA ZIMA MOTO MARA BAADA YA KUWADANGANYA KWA KUWAPIGIA SIMU

Mmoja wa wakazi wa Rugelele kata Rujewa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya  DUKA MKWILA[20]ni miongoni mwa wananchi waliopiga simu za uongo katika kikosi cha zimamoto mkoa wa mbeya akiwa amepewa adahabu ya kuosha gari la zimomoto
Hata hivyo DUKA alikiri kutenda kosa na kuomba msamaha kwa jeshi hilo ambapo aliachiwa huru na kisha kurejea kwao huku akijutia kosa alilolifanya na kuahidi kutorudia tena.

VIWANGO VYA NAULI KUTOKA UBUNGO HADI MIKOA MINGINE

MAGAZETI YA LEO JUMANNE OKTOBA 1, 2013

DSC 0051 4272d
DSC 0052 dc9bc

MKENYA ALIYEDAIWA KUMTEKA DK. ULIMBOKWA ATOZWA FAINI 1,000/-

fain_269e9.jpg
Mkenya Joshua Mulundi aliachiwa huru baada ya kulipa faini ya Sh1,000 kwa kupatikana na hatia ya kuidanganya polisi kuwa alihusika kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimhukumu kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini hiyo. Mulundi alilipiwa faini hiyo na Mwandishi wa Habari wa Redio Times, Chipangula Nandule.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka kusoma maelezo ya awali na mshtakiwa huyo kukiri alitoa taarifa ya uongo kwa polisi kuhusu tukio hilo.
Kabla ya hukumu hiyo, Mulundi aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa hilo lilikuwa kosa lake la kwanza. Pia alijitetea kuwa Juni 27, 2012 akiwa Arusha alitekwa na kupelekwa Dar es Salaam ambako alikuwa hana mwenyeji wala hakuwahi kufika.
Alisema kutokana na kutekwa huko alichanginyikiwa hivyo kukubali chochote alichoambiwa afanye kwa kuwa aliyemteka alikuwa na silaha na alimwelekeza mambo ya kuzungumza.
"Mheshimiwa kwa ajili ya vitisho hivyo, nilikwenda Kawe katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko kwenye eneo la Tanganyika Packers, mbele ya Mchungaji Joseph Malwa Kiliba na kuungama kuwa ni miongoni mwa watu waliomtesa Dk Ulimboka katika Msitu wa Pande," alisema Mulundi na kuongeza:
"Siwalaumu Serikali, upande wa mashtaka wala polisi kwa kitendo cha kuniweka gerezani kwa muda mrefu, najilaumu mimi mwenyewe."
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Kweka aliiambia Mahakama kuwa hana kumbukumbu za uhalifu za mshtakiwa lakini aliomba apewe adhabu kali kutokana na mazingira ya tukio hilo.
Akitoa hukumu, Hakimu Katema alisema alifikia uamuzi huo kwa kuzingatia maombi ya mshtakiwa ya kupunguziwa adhabu.

VIJANA WANAVYOSAJILIWA KUPIGANIA AL SHABAAB

alshabaab-soldiers-in-training_495033_e5a43.png
Uchunguzi wa BBC umefichua ambavyo vijana husajiliwa kujiunga na kundi la kigaidi la Al Shabaab katika pwani ya Kenya.
Al Shabaab limekiri kufanya shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la Westgate ambapo zaidi ya watu sitini waliuawa na mamia kujeruhiwa.
Uchunguzi wa BBC, unatizama ambavyo vijana wanafunzwa itikadi kali za dini katika kuwaandaa, kujiunga na kundi la Al Shabaab.
Vikao vya kuwasajili Vijana hao huanza na viongozi wa dini kutoa hotuba kwa vijana waisilamu wengi ambao wamesilimu.
Uchunguzi huo umebaini kuwa vijana hao ambao wanakuwa wamejitolea kupigania kile wanachosema ni dini, hupelekwa katika maeneo ya vijijini katika fuo za bahari kama sehemu ya kwanza ya safari yao kwenda Somalia.
Mmoja wa wahubiri hao kwa jina Makaburi, ametetea shambulizi lililofanywa dhidi ya Jumba la Westgate na kuwaua watu zaidi ya sitini akisema kwamba ilikuwa hatua sahihi.
Kulingana naye, ilikuwa sawa kwa sababu majeshi ya kigeni yanapigana nchini Somalia.
Jeshi la Kenya lilipeleka wanajeshi wake nchini Somalia,miaka miwili iliopita kupambana na kundi la Al Shabaab.
Wakati huohuo, maombi yanafanyika katika sehemu mbali mbali mjini Naiobi kuwaombea waathiriwa wa shambulizi hilo

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...