Wednesday, October 02, 2013

VYOMBO VYA USALAMA VIKOMESHE UHALIFU, UMAFIA TANZANIA

Meno-ya-tembo_a1920.jpg
Na Daniel Mbega
UHALIFU nchini Tanzania umekuwepo kwa miaka mingi, lakini katika miaka ya karibuni umeonekana kushika kasi kuliko ilivyowahi kutokea, kiasi cha kutishia amani kwa Watanzania kuhusu usalama wa maisha na mali zao.
Kati ya Januari 2005 hadi Januari 2006 kulikuwepo na matukio ya uhalifu na ujambazi wa kutumia silaha ambapo kiasi cha Shs. 16,782,172,419 kiliporwa katika benki kadhaa za maduka ya kubadilishia fedha nchini.
Takwimu zinaeleza kwamba jumla ya wahalifu 46, wakiwemo raia 12 wa Kenya, walikamatwa katika kipindi hicho wakihusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu.


Baada ya hapo ikafuatia kasheshe kubwa ndani ya Jeshi la Polisi, sekeseke ambalo lilifanya iibuliwe orodha ya maofisa 20 wa jeshi hilo ambao wanashirikiana na majambazi katika wizi huo.
Lakini wakati huo zilikuja taarifa mfululizo zikiwatuhumu askari kadhaa ndani ya jeshi hilo ambao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu, huku wakiwa wamechuma mali nyingi ambazo haijulikani namna walivyozipata kulinganisha na mishahara yao.
Kama nilivyotangulia kusema, vitendo vya uhalifu hapa nchini vimekuwepo kwa miaka mingi, na kwa kumbukumbu zangu vitendo hivi vilianza kushika kasi mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Vitendo hivi vya uhalifu si ujambazi tu, bali ni pamoja na uhujumu uchumi, magendo pamoja na wizi wa maofisini. Uhujumu uchumi huu ndio uliomfanya Waziri Mkuu wa wakati ule, hayati Edward Moringe Sokoine, akasimama kidete kukabiliana na wafanyabiashara na watu wote waliokuwa wakijihusisha na magendo mwanzoni mwa miaka hiyo ya 1980.
Wapo wengi waliokumbwa na kimbunga cha Sokoine, na wengi wao walikuwa watumishi wa umma, katika Chama na hata serikali, ambao ama walishiriki moja kwa moja au waliwatumia jamaa zao katika harakati zao za kuvuna wasichopanda.
Sokoine alikuwa sahihi, kwa sababu hali ilikuwa mbaya katika kipindi hicho, kipindi ambacho binafsi siwezi kukisahau kwa sababu bidhaa zote muhimu ziliadimika kiasi kwamba wengine wakaona kulikuwa na afadhali wakati wa mkoloni kuliko kipindi hicho.
Maduka ya kaya, ambayo yalichipua kila sehemu Tanzania, kuanzia mijini mpaka vijijini, yalikuwa hayana vitu vile muhimu kama sukari, sabuni, na kadhalika. Watu wachache, tena wale waliokuwa watumishi wa umma, walishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara kuuza vitu vilivyostahili kuletwa kwenye maduka hayo. Kilikuwa kipindi cha ulanguzi!
Nakumbuka tulikuwa tukiweka foleni ya mawe kwa kusubiri sukari ambayo ilikuwa inakuja baada ya mwezi au miezi miwili, na hata ilipokuja tukalazimishwa kununua kilo moja moja tu ambayo pia iliambatana na kulazimishwa kununua jembe la mkono 'Chapa Jogoo'!
Ni mateso haya ya wananchi ambayo yalimfanya Waziri Mkuu Sokoine aingilie kati na kuanza kupambana na wahujumu uchumi na wafanya magendo, hasa baada ya kugundulika kwamba bidhaa hizo zilikuwa zikiuzwa usiku na kwa usiri mkubwa. Waliohusika ni wale wale waliokuwa na dhima ya kuwatumikia wananchi.
Ujambazi katika kipindi hicho cha Sokoine ulichomoza kwa kasi ya ajabu, na hii ilitokana na ukweli kwamba, kulikuwa na watu wengi waliokuwa na silaha. Watu hawa walivamia benki na kuteka nyara magari ya abiria kwa ya mizigo, kisha kuchota mali ambazo hawakuzichuma.
Watu hawa, kwa asilimia kubwa, walikuwa ni wale askari walioshiriki katika Vita ya Kagera, vita pekee ambayo Tanzania huru imewahi kupigana. Baada ya kumtoa Dikteta Nduli Idi Amini Dada na kumfukuza kabisa Uganda, askari hawa, mashujaa wetu, baadhi yao walirejea makwao wakiwa na silaha pamoja na magwanda ya jeshi. Hawakuyarejesha kwenye kambi zao, nadhani kwa sababu ya furaha iliyokuwepo wakati huo na hakuna aliyewatilia shaka.
Kila mmoja aliwasifu mashujaa hao kwa kumng'oa madarakani Amini, na inawezekana hata makamanda wa jeshi wakajisahau kuwataka askari hao warejeshe silaha, ingawa wapo waungwana ambao walizirejesha.
Hawa ambao hawakuzirejesha, hatimaye wakaamua kabisa kuachana na jeshi na kuingia uraiani, na wengine kwa tamaa zao ama kuona kwamba wao binafsi hawakunufaika na ushindi huo, wakaamua kutumia silaha hizo na magwanda kwa njia haramu ya kujipatia mali. Wakaanza kushiriki vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha.
Alhaji Ally Hassan Mwinyi alipoingia madarakani mwaka 1985 kwa kauli mbiu yake ya 'Fagio la Chuma', aliwagusa zaidi wafanyakazi na viongozi wazembe, lakini kamwe hakuwagusa majambazi kwa kudhani kwamba walikuwa wamekimbia! Lakini kumbe umafia ulikuwa umeingia nchini.
Hakuna mtu asiyelijua neno 'MAFIA' hapa Tanzania. Hata mtoto mdogo ukimuuliza anaweza akakwambia kwamba mtu akisema 'Mafia' ana maana gani. Sikatai kwamba yawezekana wapo wasioijua maana halisi ya neno hili wala asili yake.
Labda nidokeze kidogo asili na fasili ya neno hili. Mafia ni kifupi cha maneno 'Morte alla Francia Italia anela'katika lugha ya Kitaliano yakiwa na maana; 'Kifo kwa Mfaransa ni kilio kwa Mtaliano'. Wengine wanaitafsili Mafia kama: 'Mazzini autorizza furti, incendi, avvelenament' yakimaanisha kwamba 'Mazzini anaruhusu wizi, unyang'anyi, mauaji ya sumu!' Mazzini ndiye aliyekuwa bosi wa Mafia, ambao asili yao hasa ni katika visiwa vya Sicily nchini Italia, ambapo historia inaonyesha kwamba kundi hili liliundwa zamani sana katika mwaka 1282 baada ya kuwatimua Wafaransa waliokuwa wakikikali kisiwa hicho. Lengo lao kubwa lilikuwa kutetea maslahi yao.
Hata hivyo, miaka mingi baadaye wanachama wa kundi hili wakaanza kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama wizi, ujambazi, mauaji ya kutisha, na hata kuhujumu siasa na uchumi wa nchi mbalimbali.
Mpaka leo hii, Mafia bado wapo na wana wanachama wao karibu katika kila nchi ulimwenguni kote, kwani wanajihusisha na ujambazi, uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya, utekaji nyara wa magari ya mishahara na hata viongozi na watu maarufu kwa lengo la kujipatia fedha. Mauaji kwao ni kitu cha kawaida, na karibu wote wamekula yamini kutotoa siri nje hata kama watalazimika kufa.
Hawa ndio Mafia ambao tumezowea kuwarejea tunapozungumzia matukio mbalimbali ya ajabu yanayowahusu watu fulani.
Ni kwa mantiki hiyo basi nimelazimika kuandika makala haya nikisema Mafia wako ndani ya Tanzania na ndio wakijihusisha na vitendo vya uhalifu. Hii ni kwa sababu Mafia hawa miongoni mwao wako serikalini, ndani ya vyama vya siasa, wafanyabiashara na watumishi wa idara nyingine nyingi nyeti.
Wengine wapo hata katika vyombo vya sheria, mathalani Bunge, Mahakama na hata kwenye majeshi.
Itakumbukwa kwamba, Rais Mwinyi alipotoa 'ruksa' kwa kila kitu, ujambazi ukafumuka kama sisimizi. Ulifumuka pamoja na biashara nyingi ambazo kabla ya hapo hazikufikiriwa, ikiwemo biashara ya dawa za kulevya pamoja na utumiaji wake. Pia uuazaji wa nyara za serikali kama pembe za ndovu na faru, ngozi za wanyama pamoja na madini!
Mambo yote haya yasingeweza kufanikiwa kwa mtu wa kawaida. Jambazi wa kawaida hawezi kuota kwamba benki fulani kuna fedha mahali fulani halafu akaja na wenzake na kuiba kwa kutumia muda usiozidi nusu saa. Lazima atakuwa ameshirikiana na watu fulani ambao wanaifahamu ratiba na ramani halisi ya mahali husika.
Kwa maana nyingine, lazima kuwe na mtandao madhubuti, kama ambavyo tumeyashuhudia matukio mengi ya wizi katika benki, maduka ya kubadilishia fedha za kigeni, kwenye majumba na hata kwenye maduka ya wafanyabiashara wakubwa.
Ni mtandao huu ambao tunaweza kuuita uko katika kundi la Mafia, ambao umefanya mpaka maofisa wa jeshi la polisi wahusishwe moja kwa moja, kwani hawa wanawafahamu majambazi.
Taarifa zinaonyesha kwamba, katika baadhi ya matukio, wakati mwingine majambazi huwa wakiwapigia simu baadhi ya polisi, kuwaeleza kwamba wanakwenda kufanya tukio mahali fulani, hivyo wasishangae. Na katika hali ya kushangaza, hata polisi wa doria huwa hawapangwi katika eneo husika na wakubwa zao kwa hofu kwamba wanaweza kuwatibulia.
Kila wakifanya tukio, lazima baadaye kwa siri wawapelekee wazee 'mzigo' katika kujisafishia njia kwamba hata siku nyingine wanaweza kulindwa. Kwa maana nyingine, maofisa hawa wanawafahamu fika wahalifu na wanawajua kama reale kwa ya pili! Ina maana hata leo hii wakibanwa, lazima watawataja majambazi wote wa nchi nzima.
Inavyoonyesha ni kwamba, mtandao wa uhalifu umeenea sana kama ule wa Mafia, kwani siyo ajabu kukuta majambazi wa Tanzania wakaenda kufanya uhalifu wao Kenya, na wale wa Kenya wakaja Tanzania.
Polisi pia wanawafahamu hata wale majambazi wa kigeni kama kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao hujificha katika nyumba za wageni hapa jijini.
Zaidi polisi wanafahamu hata uingiaji wa silaha zinazotumika katika uhalifu huo, mbali ya kwamba hata wenyewe huwa wanawakodisha majambazi silaha zao.
Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita nilikuwa natokea Dodoma. Muda mfupi kabla sijaondoka nikiwa nimekata tikiti yangu, bwana mdogo mmoja anayenifahamu akaniita pembeni na kunielekeza kwa kijana mmoja mdogo tu kama yeye, yapata kama miaka 22 hivi.
"Unamuona yule," alisema kijana huyo akinionyesha kwa kidole kijana huyo ambaye alikuwa mbali kidogo.
Nikamjibu ndiyo nimeomuona. Kisha akasema, "Basi brother, kama unahitaji bastola, rifle au SMG mwambie tu. Ameingia jana na anazo kama saba hivi!"
Nilinyamaza kidogo nikitafakari kabla sijamuuliza kijana wangu huyu alijuaje. Akaniambia kwamba kijana huyo mgeni alimwendea asubuhi hiyo na kumshauri amtafutie wateja wa 'bidhaa' zake.
"Hata wewe kama unataka sema, bastola anauza shilingi 500,000 tu na unaweza kurudisha fedha zako katika kipindi kifupi sana pamoja na faida," akaniambia kijana huyu.
"Nitarudishaje?" nikamuuliza swali kwa mtego. Yeye akajibu haraka haraka kwa kusema ninaweza kuikodisha kwa 'watu wa kazi'! Nilimkazia macho halafu nikamuuliza kwamba niwakodishe majambazi, wakaue na kuiba, kisha ndipo waniletee silaha yangu na fedha? Yeye akajibu haraka haraka kwamba ndivyo alivyomaanisha.
"Kama polisi wanakodisha SMG kwa majambazi na wanachuma fedha, wewe unaogopa nini? Kwani wewe ndiwe unayeingia vitani?" akaniuliza.
Lakini nikamwonya kamwe asijidanganye kuingia katika biashara hiyo. Jambazi anayekwenda kuiba na kuua, na yule anayemkodisha silaha, wote ni majambazi tu!
Kilichonishangaza zaidi ni kwamba, kijana yule inasemekana silaha hizo alikuwa anazinunua kwenye kambi za wakimbizi huko Ngara. Lakini nikajiuliza, anaweza kusafiri kutoka Ngara hadi Dodoma, na pengine hata Morogoro au Arusha, bila kukamatwa na polisi?
"Wewe brother utafikiri siyo msomi? Kuna kitu kinachoshindikana mbele ya fedha? Polisi wenyewe wakati mwingine huwa wanawasindikiza majambazi, sembuse mtu kupita na silaha!" kijana yule akasema katika namna ya kunizodoa.
Huyu ni miongoni mwa watu wengi wanaofanya biashara hiyo ya silaha, na kwamba wanashiriki moja kwa moja kwenye ujambazi na ndiyo maana uhalifu unazidi kumea kila siku. Na hii inatokana na mtandao wao waliouweka mpaka serikalini.
Wapo viongozi wengine wa serikali wanaoshiriki katika uuzaji wa nyara za serikali, wapo wanaoshiriki katika biashara za dawa za kulevya, kama wale wabunge kadhaa ambao waliibuka tu ghafla kutoka vijiweni na kuwa na mali nyingi katika kipindi kifupi.
Hawa nao wameingia kwenye chombo cha kutunga sheria ili waweze kutunga sheria zinazowapa unafuu wahalifu wengi kote nchini. Wahalifu hawa wameingia serikalini ili kuficha maovu yao, japo ni miongoni mwa majambazi sugu waliokuwa wakitafutwa na polisi.
Wapo wafanyabiashara wanaodaiwa kuwa majambazi na wamekuwa mstari wa mbele kuvisaidia vyama vya siasa fedha za kampeni na mambo mengine kadha wa kadha, ili tu kuficha maovu yao.
Pengine nimalizie kwa kusema, vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kutekeleza wajibu wao kikamilifu katika kupambana na mtandao huu mpana wa Mafia hapa nchini. Kinyume cha hapo, wananchi wanaweza kuchoshwa na vitendo hivi, na kwa hakika, mnyonge anaposema 'sasa yatosha' madhara yake huwa ni makubwa, kwani huwa hajali nini kitakachotokea! <MWISHO>.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...