Benki ya NBC tawi la Moshi. Picha ya Maktaba
Askofu wa Kanisa la Christian Fellowship
Assemblies of God la Arusha, Jumanne Kilongola amehukumiwa kifungo cha
miaka 32 jela baada ya kupatikana na hatia ya kupora Sh5.3 bilioni ndani
ya Benki ya NBC, Tawi la Moshi Mei 21, 2004.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa jana na Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kilimanjaro, Simon Kobelo,
askofu huyo amehukumiwa kifungo hicho pamoja na raia watano wa Kenya
baada ya kupatikana na hatia ya kufanya wizi huo kwa mtutu wa bunduki.
Kati ya fedha hizo, Sh126.2 milioni zilikuwa mali
ya Benki ya NBC wakati Sh5.1 bilioni ni mali ya Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) ambayo ilikuwa ikitumia NBC Moshi kama kituo chake kidogo.
Ilielezwa mahakamani hapo wakati wa ushahidi kuwa
Askofu Kilongola ndiye aliyekodi gari aina ya Toyota Landcruiser
lililotumiwa kubeba fedha hizo kwa Sh320,000 na alimweleza mmiliki wake
kuwa alikuwa anakwenda kubeba wanakwaya wake.
Raia wa Kenya waliohukumiwa kifungo hicho cha
miaka 32 ni Wilfred Onyango Nganyi, Patrick Muthee Murithi, Gabriel
Kungu Kariuki, Jimmy Maina Njoroge na Simon Ndungu Kiambuthi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz