Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma na iwapo hatafanya hivyo utaongoza maandamano nchi nzima.
Umoja huo pia umeeleza kuwa kuendelea kwa Bunge
hilo ni sawa na kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya, kuiweka nchi
rehani, kufuja fedha za walipakodi, kuwahadaa Watanzania kwa kupitisha
Katiba isiyotokana na maoni yao, huku kanuni zikibadilishwa na kuingizwa
mambo ya Tanganyika katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kadhalika, umemtaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu
za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha za Bunge
hilo kwa maelezo kuwa zinatumika bila maelezo sahihi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) akiwa
na wenyeviti wenzake, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba
(CUF), alisema hawatataja muda lakini wanataka jambo hilo lifanyike
haraka iwezekanavyo.
“Iwapo Rais Kikwete hatatumia mamlaka yake
kusitisha Bunge na kukubali liendelee kinyume na matakwa ya wananchi,
Ukawa tutawaongoza Watanzania kupaza sauti kupinga najisi inayotiwa
kwenye maoni yao, kupitia maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima,”
alisema Mbatia.
Akizungumzia iwapo Rais anayo mamlaka ya kusitisha
vikao vya Bunge hilo, Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Jesse James alisema anaweza kufanya hivyo kwa kutumia
dhamana ya uongozi aliyonayo, lakini kisheria hawezi kutokana na Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba kutokuwa na ibara inayompa mamlaka hayo.
“Rais ni Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa nchi na
Serikali. Majukumu hayo ndiyo yanayomfanya awe na uwezo wa kusitisha
shughuli za Bunge hilo, hasa akiona theluthi mbili ya wajumbe kutoka
kila upande kwa ajili ya kufanya uamuzi haitapatikana.”
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wanaotokana na vyama
vya siasa vinavyounda Ukawa na baadhi kutoka Kundi la 201, walisusia
vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba
usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo wa serikali
mbili badala ya tatu zilizopendekezwa katika rasimu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Mbatia alisema Ukawa imechukua uamuzi wa
kuandamana kutokana na wajumbe wa CCM pamoja na wengine 166 walioteuliwa
kupitia kundi la wajumbe 201, kuendelea na vikao vya Bunge hilo na
kuingiza mambo yao katika Rasimu ya Katiba, huku wakilipwa fedha za
walipakodi.
“Mambo wanayoyajadili na kuyachomeka kinyemela
kwenye rasimu kama ardhi, elimu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo na serikali
za mitaa ni masuala yanayopaswa kuandikwa kwa kina ndani ya Katiba ya
Tanganyika siyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Mbatia na
kuongeza:
“Zanzibar walijadili wenyewe mambo yao ya ndani na
kutengeneza Katiba yao, hivyo hatuoni mantiki ya wajumbe kutoka
Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya Tanganyika. Bunge la Katiba halina
sifa za kujadili mambo yasiyo ya muungano. Hii inaonyesha CCM wamelewa
madaraka.”
Alisema ili Bunge hilo lipate uhalali wa kuendelea
yanatakiwa kufanyika maridhiano ya pande zote zinazovutana na
kusisitiza kuwa kinachoendelea sasa kinatokana na kukosekana kwa uongozi
wa kisiasa.
“Wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema kuwa suala la muundo
wa serikali lilitakiwa kupigiwa kura, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba,
Samwel Sitta anaendelea kuongoza Bunge kama mchakato ni mali yake
binafsi. Baadhi ya viongozi wa chama hicho wanataka mchakato usitishwe,
wengine wanataka uendelee,” alisema.
Mbatia alisema Ukawa inashangazwa na Rais Kikwete kwa kitendo chake cha kufanya ziara ya kutembelea ranchi binafsi
ya kufugia wanyama ya aliyekuwa Rais wa Marekani, George Bush wakati
nchi ikiwa katika sintofahamu ya mchakato wa kupata Katiba Mpya huku
watu wa kada mbalimbali wakitaka mchakato usitishwe.
Profesa Lipumba alisema: “Wapo wanaosema kuwa
Ukawa tumegawanyika. Hilo siyo kweli kwa sababu waliotusaliti na
kuhudhuria vikao vya Bunge hata asilimia tano hawafiki. Zaidi ya
asilimia 95 hatujakwenda bungeni,” alisema.
Alisema kuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alitenga masuala ya ardhi,
maliasili na Serikali za Mitaa ili yaingizwe katika Katiba ya
Tanganyika, hivyo kuyajadili mambo hayo katika Katiba ya Jamhuri ya
Muungano si sahihi. Mbowe alisema: “Viongozi wanaiacha nchi ijiendeshe
yenyewe. Ni kama ndege ambayo rubani yupo lakini ameweka ‘auto pilot’,
yaani wameiruhusu ndege ijiendeshe yenyewe.”
CAG achunguze
Kuhusu suala la ukaguzi wa hesabu, Mbatia alisema
katika vikao vya Bunge la Bajeti, baadhi ya wabunge walihoji
zinakopatikana fedha za kuendesha Bunge la Katiba na kusema kutokana na
hali hiyo, ni vyema CAG akachunguza kwa undani suala hilo.
Hoja kutaka Bunge hilo lisitishwe inaungwa mkono
na makundi mbalimbali pamoja na baadhi ya wabunge wa CCM, akiwamo Naibu
Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba (Iramba-Magharibi) aliyesema
likiendelea bila uhakika wa kupata akidi ya uamuzi itakuwa ni kupoteza
zaidi ya Sh20 bilioni za walipa kodi na wananchi hawataelewa.
Hata hivyo, uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa
vikao hivyo ambavyo awali vilifanyika kwa siku 67, vitaendelea kwa siku
60 za kazi zilizoongezwa na Rais Jakaya Kikwete, bila kuhusisha siku za
Jumamosi na Jumapili ambazo zinaongeza muda wa wajumbe kukaa Dodoma kuwa
84. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment