*Rwanda, Kenya, Uganda na Burundi zaungana kuunda Shirikisho la Kisiasa
*Waziri Sitta asema zina ajenda ya siri, ashangaa marais kuwaburuza wananchi wao
HATIMAYE
Tanzania imewekwa kando rasmi na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), katika kuunda Shirikisho la Kisiasa litakaloziongoza
nchi hizo.
Tayari marais wa nchi hizo, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni
wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre Nkurunzinza wa Burundi
wamekwishafikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa
Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC, bila
kuishirikisha Tanzania.
Waziri wa Serikali za Mitaa wa Rwanda,
James Musoni, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza
kuwa makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya
Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki, yalifikiwa Septemba 12 mwaka
huu, mjini Kampala na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda na hivi karibuni
Rais wa Burundi ambaye alialikwa katika mkutano huo na kushindwa
kuhudhuria, naye sasa amethibitisha ushirika wake katika shirikisho hilo
jipya.
Gazeti la The Sunday Times la Rwanda, limemnukuu Waziri Musoni kuwa marais wa nchi hizo wamekubaliana kukamilisha rasimu hiyo ndani ya muda mfupi.