Wednesday, September 18, 2013

TANZANIA YAMEGWA EAC

*Rwanda, Kenya, Uganda na Burundi zaungana kuunda Shirikisho la Kisiasa
*Waziri Sitta asema zina ajenda ya siri, ashangaa marais kuwaburuza wananchi wao

HATIMAYE Tanzania imewekwa kando rasmi na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika kuunda Shirikisho la Kisiasa litakaloziongoza nchi hizo.

Tayari marais wa nchi hizo, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre Nkurunzinza wa Burundi wamekwishafikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC, bila kuishirikisha Tanzania.

Waziri wa Serikali za Mitaa wa Rwanda, James Musoni, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza kuwa makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki, yalifikiwa Septemba 12 mwaka huu, mjini Kampala na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda na hivi karibuni Rais wa Burundi ambaye alialikwa katika mkutano huo na kushindwa kuhudhuria, naye sasa amethibitisha ushirika wake katika shirikisho hilo jipya.

Gazeti la The Sunday Times la Rwanda, limemnukuu Waziri Musoni kuwa marais wa nchi hizo wamekubaliana kukamilisha rasimu hiyo ndani ya muda mfupi.

SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA BALOZI WA CHINA ALIYEHUDHURIA MKUTANO NA WA CCM

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imehadharisha mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, kuepuka kujihusisha na mambo ya ndani.

Hadhari hiyo imetolewa jana katika taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari, baada ya Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China, Lu Younqing, kuonekana katika mkutano wa hadhara wa CCM, akiwa amevalia kofia yenye nembo ya chama hicho.

“Wizara inaelekeza kwamba kitendo cha Balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa, sio sahihi na kinakiuka Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa 
kidiplomasia.

“Mkataba huo wa Vienna unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi, ikiwemo siasa wanapofanya kazi zao katika nchi za uwakilishi,” ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na msemaji wa wizara hiyo, Mkubwa Ally.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa hata Sheria ya Diplomasia ya Tanzania ya Mwaka 1986, ambayo ni zao la Mkataba wa Vienna, pia hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi, kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi.

MAGAZETI YA LEO JUMATANO SEPTEMBA 18, 2013

DSC 0013 c0ea2
DSC 0014 12cc6

MSEMAJI WA BROTHERHOOD AKAMATWA MISRI

misri b89cf
Msemaji rasmi wa vuguvugu la Muslim Brotherhood amekamatwa nchini Misri. Hii ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali
Gehad al-Haddad alikamatwa akiwa na mwanachama mwingine mmoja wa vuguvugu hilo katika nyumba moja mjini Cairo.
Taarifa zinazohusianaMisri
Bwana Haddad aliwahi kuhudumu kama afisa wa ngazi ya juu wa naibu mkuu wa majeshi, Khairat al-Shater, wa vuguvugu hilo na kawaida alizungumza na vyombo vya habari vya kigeni.
Serikali ya Misri imekuwa ikifanya msako dhidi ya makundi ya kiisilamu tangu jeshi kumwondoa mamlakani aliyekuwa rais Mohammed Morsi mwezi Julai.
Awali, mahakama ya uhalifu mjini Cairo, iliamua kuwa mali zote za viongozi wa vuguguvu hilo pamoja na lile la Gamaa Islamiya kupigwa tanji.
Viongozi wa mashtaka waliwaekea vikwazo maafisa wa ngazi ya juu wa Brotherhood akiwemo, Mohammed Badie, Shater na wengine wengi mnamo mwezi Julai.
Wengi wao wamezuiliwa kuhusiana na madai ya kuchochea ghasia na mauaji.
Mamia ya watu wanataka Bwana Morsi kurejeshwa mamlakani , wengi wakiwa wanachama wa Brotherhood .
Aidha makabiliano yaliyotokea mwezi jana kati na polisi na wafuasi wa Morsi yalisababisha vifo vya wanachama wengi pale polisi walipovamia kambi zao mbili walipokuwa wanataka Morsi kurejehswa mamlakani. Chanzo: bbcswahili

BABU WA MIAKA 95 AMUOA BABU MWENZIE WA MIAKA 65



Wanaume wawili wazee ambao ni maaskari wakongwe walioshiriki vita ya pili ya dunia, ijumaa iliyopita (September 13) walifunga ndoa ya jinsia moja (mashoga) baada ya kuwa katika uhusiano kwa miaka 20 kabla ya kufikia uamuzi wa kuoana.
gays-1

John Banvard mwenye miaka 95 alimuoa Gerald Nadeau mwenye miaka 67 huko Diego, California Marekani.

RPF CHAIBUKA NA USHINDI NCHINI RWANDA

zkagame_32c2c.jpg
Chama tawala nchini Rwanda, RPF kimeibuka mshindi katika uchaguzi wa wabunge uliofanyika Jumatatu.
Chama hicho chake Rais Paul Kagame kimeshinda uchaguzi huo kwa asilimia 76 ya kura zote zilizopigwa .
Aidha chama hicho kiliingia mamlakani baada ya mauaji ya kimbari yaliyofanyika mwaka 1994 na kimepata viti 40 kati ya 53 vilivyokuwa vinawaniwa.


Chama cha upinzani, FDU-Inkingi, ambacho kiongozi wakeVictoire Ingabire yuko jela, hakikushiriki uchaguzi huo kwani hakijasajiliwa rasmi.
Vyama vingine viwili vya kisiasa vinavyosemekana kuwa washirika wa RPF, vilipata asilimia 13 na asilimia tisa ya kura.
Shughuli ya kupiga kura ilifanyika siku mbili baada ya vifo vya watu wawili kutokana na shambulio la maguruneti mjini Kigali.

MAGUFULI AAGIZA VITUO VYA MIZANI YA BARABARANI MKOANI IRINGA VICHUNGUZWE


Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (pichani) ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Iringa ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu utendaji wa vituo vya mizani mkoani Iringa. Agizo hilo lilitolewa katika mkutano ambao Waziri huyo wa Ujenzi alikutana na wafanyakazi wa taasisi zinazosimamiwa na Wizara ya Ujenzi mkoani humo.

Wakati akisomewa taarifa za utekelezaji wa majukumu ya kila taasisi mkoani humo ndipo lilipojitokeza suala la tozo iliyokusanywa kwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamezidisha uzito kwa kipindi cha mwezi mmoja wa Julai mwaka huu wa 2013 katika kituo cha mizani cha Wenda kilichopo kati ya Iringa na Ifunda katika barabara kuu ya TANZAM.


Meneja wa Tanroads wa mkoa wa Iringa Injinia Poul Lyakurwa alimtaarifu Waziri Magufuli kuwa kiasi cha Shilingi milioni 31.9 kilikusanywa katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.
 
Akishitushwa na kiwango hicho Waziri Magufuli  alibainisha kuwa, kiasi hicho kilichosomwa katika taarifa kimetokana na magari 735 yaliyokamatwa kati ya magari 20,700 yaliyopimwa sawa na asiliamia 3.5. “Takwimu hizi sizikubali kwani wastani wa magari yanayokamatwa katika nchi nzima unakaribia asiliamia 40 iweje barabara kuu kama hii iwe na kiwango kidogo kiasi hicho cha magari yaliyokutwa na makosa” hapa ni lazima pafanyike uchunguzi” alisisitiza Mheshimiwa Magufuli na kueleza kuwa hali hiyo hawezi kuiruhusu hata kidogo kuendelea.

KIGOGO WA MAGARI YA WIZI TZ ANASWA....!!!


Jengo ambalo linadaiwa ndiyo kiwanda hatari cha kubadilisha magari ya wizi, kimefumuliwa na mmiliki wake sasa hivi yupo nyuma ya nondo akingoja kufikishwa mahakamani.
 
Kigogo wa magari ya wizi, Benovilla Luhanga baada ya kunaswa.
Benovilla Luhanga, 43, ametajwa kuwa ndiye mmiliki wa kiwanda hicho na siku ananaswa, alikutwa na magari ya kihafari matano ambayo yote inadaiwa ni ya wizi.
Vilevile, Luhanga alikutwa na Bajaj moja ambayo imedaiwa nayo ni ya wizi na kwamba alikuwa tayari ameshaibadili rangi.
Luhanga alikamatwa akiwa na mkewe ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
 
Moja ya gari alilokutwa nalo mtuhumiwa.

KESI YA MAKAMU WA RAIS KENYA, SHAHIDI WA KWANZA ATOA USHAHIDI ICC

zruto_fecef.png
Shahidi wa kwanza kutoka upande wa mashtaka, amefika mbele ya mahakama ya kimataifa ICC kutoa ushahidi dhidi ya naibu Rais wa Kenya William Ruto.
Mahakama inamlinda shahidi huyo kwa kutoonyosha sura yake.
Ruto anakabiliwa na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007-2008
Kesi dhidi ya Ruto na mshtakiwa mwenzakeJoshua Arap Sang, ilianza tarehe 10 mwezi Septemba, baada ya wawili hao kutuhumiwa katika kuhusika na ghasia hizo za mwaka 2007.
Kumekuwa na wasiwasi kuhusu mashahidi kujiondoa kwenye kesi hiyo wakihofia usalama wao. Mwishoni mwa wiki, mashahidi wanne walijiondoa katika kesi hiyo baada ya kuelezea wasiwasi kuhusu usalama wao ikiwa watatoa ushahidi mbele ya mahakama hiyo.
Wiki jana mkuu kwenye kesi hiyo, aliakhirisha kesi hiyo kwa sababu mashahidi hawakuwa wamefika kwenye mahakama hiyo kutoa ushahidi wao.
Rais Uhuru Kenyatta, anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo mwezi Novemba kwa mashtaka sawa na hayo.

MADEREVA WA BODABODA DAR WAUA JAMBAZI

MAJAMBAZI wawili wameuawa katika matukio mawili tofauti Dar es Salaam akiwamo mmoja aliyeuawa na madereva wa pikipiki katika eneo la Vingunguti karibu na kituo cha mafuta. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa majambazi wapatao wanne walimvamia mfanyabiashara Abas Mussa (47) wa Vingunguti wakiwa na bunduki na mapanga.

Alisema mfanyabiashara huyo akiwa dukani kwake, ghafla walifika vijana wawili, mmoja akiwa na bunduki fupi na mwingine akiwa na panga na kumpora mwenye duka Sh 1,400,000.

Pia walimpora simu moja ya Nokia na ufunguo wa gari na alipotoka nje ya duka alisikia mlio wa bunduki na kumuona mfanyakazi wake Ally akiwa chini na watu wengi wakiwa wamejikusanya.

Alisema baada ya tukio hilo kutokea madereva wa pikipiki waliwaona majambazi hao na kuwafukuza na walipofika njia panda ya Tabata Relini walimkamata jambazi mmoja na kuwashambulia hadi kumjeruhi.

Kamanda alisema polisi walipata taarifa na walipofika eneo la tukio walimkuta jambazi huyo akiwa na hali mbaya. Walimchukua na kumpeleka hospitali lakini alifariki dunia akiwa njiani.

Alisema jambazi mmoja alikimbia baada ya kuacha pikipiki ya Sunlag na polisi waliweza kuwakamata waliokimbia baada ya tukio hilo.

Katika tukio jingine, jambazi mmoja aliuawa na polisi wakati majambazi sita walipojaribu kupora mamilioni ya fedha katika mtaa wa Jamhuri Kitumbini.

Tuesday, September 17, 2013

MWANAMUZIKI WA TAARAB AHMED MGENI AFARIKI DUNIA LEO ALFAJIRI

 
Mwimbaji wa kundi la Zanzibar Njema Mordern Taarab Ahmed Mgeni amefariki dunia leo alfajiri (September 17) katika Hospitali ya Mnazi mmoja, Kisiwani Zanzibar alikolazwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifua.

Akiongea katika kipindi cha Leo Tena ya Clouds Fm mkurugenzi mwenza wa Zanzibar Njema Modern Taarab Ally Ngereja amesema msiba uko Amani Fresh, Zanzibar ambapo ni kwa baba yake na atazikwa leo (September 17) saa kumi jioni.

Marehemu aliwahi kutamba na nyimbo nyingi ikiwemo sitetereki inayofanya vizuri mpaka sasa.

KESI YA SHEIKH PONDA, AKOSA DHAMANA, KESI YAHAIRISHWA HADI OKTOBA 1

ponda_26617.jpg
Sheikh Ponda Akishuka kwenye basi la Magereza tayari kuingia Mahakamani Kusikiliza kesi yake inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Morogoro. Sheikh Ponda alishatikiwa katika Mahakama Hiyo akikabiliwa na Mashtaka Matatu Ambayo inadaiwa aliyatenda Mkoani Morogoro katika Mkutano Hadhara mwezi uliopita. Kesi hiyo imearishwa tena Mpaka Tarehe 01.10.2013. Sheikh Ponda amenyimwa Dhamana na amerudishwa Rumande.

WATUHUMIWA WA MAUAJI YA BILIONEA ERASTO MSUYA WAKUTWA KWA SANGOMA

Jeshi la polisi mkoa wa kilimanjaro linawashikilia watu wanne zaidi wakidaiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara bilionea wa madini ya tanzanite Arusha Erasto Msuya 43 wawili kati yao walikutwa kwa mganga wa kienyeji (sangoma) wakifanyiwa zindiko ili wasikamatwe na vyombo vya dola.

Pia jeshi limenikiwa kunasa bunduki aina ya SMG yenye namba za usajili KJ10520,inayoaminika kutumika katika mauaji hayo.Msuya aliuawa kwa kupingwa risasi zaidi ya 10 kifuani Augost 7mwaka huu,katika eneo la mijohoroni wilayani Hai.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,kamanda wa Mkoa wa Kilimanjaro ,Robert Boaz aliwataja watuhumiwa kuwa ni Sadiki Jabiri 32 mkazi wa Dar es Salaam na Lang'angata wilayani Hai .

KINANA AMPONZA BALOZI WA CHINA... CHADEMA KUMSHITAKI KWENYE MAHAKAMA YA KIMATAIFA

http://3.bp.blogspot.com/-tB-YS2RGEHk/UjfrTKmUq2I/AAAAAAAAl3k/wO2eYdRF-0M/s1600/1.png
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitamshitaki Balozi wa China nchini, Lu Younqing Umoja wa Mataifa (UN) kwa kukiuka Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa mwaka 1964 ambao unaeleza uhusiano wa kibalozi kati ya nchi na nchi.

Aidha, kimesema kitaiandikia barua Serikali ya China ili kutaka ufafanuzi kama imemtuma Balozi wake kufanya kazi ya uenezi siasa kwenye vyama.


Tukio la Balozi huyo kuhudhuria mkutano wa hadhara wa CCM lilitokea Septemba tisa mwaka huu kwenye mkutano wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Kishapu Shinyanga, ambapo Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana alimtambushisha balozi huyo huku akiwa amevaa sare za chama hicho.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri kivuli wa mambo ya nje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana Jijini Mwanza, Ezekiel Wenje alisema Chadema wameamua kuchukua hatua hizo ili kukomesha vyama vya siasa kutumia mabalozi kama wawakilishi wa vyama vyao kwa kufanya uenezi kwenye mikutano ya siasa.

HATMA YA DHAMANA YA PONDA LEO...!!!

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, leo inatarajiwa kuamua iwapo Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, anastahili dhamana au la, kutokana na kesi inayomkabili.  
Shekhe Ponda alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 19 na kusomewa mashitaka matatu ya uchochezi yanayomkabili. Upande wa mashitaka ulidai mahakamani hapo kuwa utaleta mashahidi 15 na vielelezo vitatu, ili kuthibitisha mashitaka hayo. 
Baadhi ya vielelezo vitakavyotolewa mahakamani hapo ni pamoja na DVD mbili, kibali kilichotolewa Agosti mosi cha kongamano la Kiislamu, kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro (OCD) na Hati ya Hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. 
Kesi hiyo ya jinai namba 128 ya mwaka 2013, iko mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Morogoro, Richard Kabate. Shekhe Ponda katika kesi hiyo, anatetewa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Juma Nasoro, wakati upande wa mashitaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...