Wakati ambapo mashabiki wa muziki wa Hip Hop nchini wakianza kusahau majonzi ya kumpoteza Albert Mangweha aka Ngwair mwezi uliopita, leo wametoneshwa tena kwa kifo cha mwana hip hop mwingine, Langa Kileo aka Lyrically And Naturally Gifted African.

Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano wa hospitali ya taifa ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha aliyezungumza na Clouds FM, Langa amefariki leo June 13, saa 11 jioni baada ya kufikishwa hospitalini hapo tangia juzi mida ya jioni. Hata hivyo amesema kutokana na maadili na taratibu za hospitali asingeweza kutoa chanzo cha kifo cha Langa na jukumu hilo ni la ndugu zake.
Hata hivyo taarifa za awali zilidai kuwa Langa alikuwa anaumwa Malaria kali iliyopelekea kukimbizwa Muhimbili jana jioni.
Baba wa marehemu Mzee Kileo amesema taarifa kamili na mipango ya mazishi zitatolewa pale vikao vya familia vitakapofanywa.Pia baba yake alisema msiba huu umetokea wakati mama yake Langa hayupo Tanzania,alisema kwa sasa mama yake Langa yupo Marekani lakini baada ya kupewa taarifa hizo tayari ameshakata tiketi ya kurudi Tanzania na ataanza safari kesho.Msiba uko nyumbani kwao maeneo ya Mikocheni(Anna Peter).























