Monday, October 06, 2014

YANGA MDOGO MDOGO, MTIBWA KILELENI

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la pili walilopata katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda 2-1.

Yanga imeendelea kutoa dozi Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa 2-1 JKT Ruvu katika mechi iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa huku Mtibwa Sugar ikiichapa Mgambo Shooting 1-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Hii ni mechi ya pili kwa Yanga kushinda katika Ligi Kuu kwani iliichapa Tanzania Prisons 2-1, lakini katika mechi yake ya ufunguzi wa msimu huu ilichapwa 2-0 na Mtibwa hivyo kuanza safari yake ya kusogea katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi kwa mwendo mdogo mdogo.
Katika mechi ya jana, hadi mapumziko Yanga ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa kwa shuti kali na beki Kelvin Yondani dakika ya 35 akiunganisha pasi safi ya Haruna Niyonzima.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Niyonzima kwa mpira wa faulo uliokwenda moja kwa moja nyavuni dakika ya 73 huku bao la JKT Ruvu likifungwa dakika ya 90 kwa shuti kali na Jabir Aziz akiwa nje ya 18. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Baada ya kupata bao la kwanza, Yanga iliongeza kasi huku ikimiliki zaidi mpira, lakini ilishindwa kutengeneza pasi za mabao.
Hata, hivyo katika kipindi cha kwanza JKT Ruvu inayoundwa na wachezaji wanaoifahamu Yanga kama Jackson Chove, Jabir Aziz, Idd Mbaga na Reliant Rusajo itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutumia vizuri nafasi ilizopata.
Kipindi cha pili, JKT ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Lusajo na Gido Simon na nafasi zao kuchukuliwa na Ally Bilali na Amos Edward, mabadiliko ambayo yaliisaidia kupeleka mashambulizi katika lango la Yanga.
Yanga yenyewe kipindi cha pili ilicheza taratibu huku ikitengeneza mashambulizi ya kushtukiza, pia ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Edward Manyama na Andrey Coutinho na nafasi zao kuchukuliwa na Salum Telela na Mrisho Ngasa. Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kwani dakika ya 73 walipata bao la pili ambalo lilifungwa na Niyonzima kwa mpira wa faulo nje kidogo ya 18. Yanga ilipata faulo hiyo baada ya Hassan Dilunga kuchezewa rafu na Mohamed Faki.
Baada ya kufungwa bao hilo, JKT Ruvu ilifanya tena mabadiliko kwa kumtoa Mbaga na nafasi yake kuchukuliwa na Najim Maguli, pia Yanga ilimtoa Niyonzima na kumuingiza Nizar Khalfan.
Katika mechi hiyo, JKT Ruvu ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 90 ambalo lilifungwa kwa shuti kali na Jabir Aziz.
Akizungumza baada ya mechi kumalizika kocha wa Yanga, Marcio Maximo alisema,”Timu yoyote ikicheza na Yanga inakaba sana na ndivyo ilivyokuwa kwa JKT Ruvu, lakini tulicheza vizuri kipindi cha pili, ligi ni ngumu.”
Kocha wa JKT Ruvu, Fred Minziro alisema,”Mechi ilikuwa ngumu, tatizo bahati haikuwa yetu ila tulicheza vizuri.”

Katika mechi nyingine iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro, Mtibwa Sugar iliichapa 1-0 bao lilikufungwa na Ally Shomari katika kipindi cha kwanza. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...