Thursday, June 13, 2013

RAIS KAGAME AMGOMEA JK



RAIS wa Rwanda, Paul Kagame, amemshambulia kwa maneno makali Rais Jakaya Kikwete, akijibu ushauri alioutoa kwa serikali yake wa kukaa katika meza ya mazungumzo na waasi wa kikundi cha Democratic Force for the Liberation of Rwanda (FDLR), ili kumaliza mapigano. Shirika la Habari la Rwanda, linalojulikana kwa jina la News of Rwanda, jana lilimkariri Rais Kagame akitoa maneno ya kejeli na yenye mwelekeo wa kupuuza ushauri wa Rais Kikwete.

Kauli hiyo ya Rais Kagame, ambayo pia imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya habari, inaonyesha kukerwa na ushauri wa Rais Kikwete ambao ameuita upumbavu uliojazwa ujinga.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kagame kutoa kauli hiyo tangu Rais Kikwete alipotoa ushauri huo, wakati akizungumza katika kikao cha Mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika mapema mwaka huu, mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Waasi wa FDLR ambao jamii yao ni Watutsi, walikimbilia nchini Kongo baada ya mapigano ya kimbari ya mwaka 1994, yaliyosababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wamekuwa wakiendesha chokochoko dhidi ya Serikali ya Rais Kagame.

Akizungumza katika sherehe ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi maofisa 45 wa jeshi lake, Rais Kagame alisema ushauri wa kufanya mazungumzo na waasi wa FDLR ni ujinga na haupo katika historia ya Wanyarwanda.


“Nilinyamza kimya kwa sababu sikupenda kusikiliza ushauri kuhusu FDLR, kwa sababu nafikiri ni upuuzi ulioambatana na ujinga, hatuwezi kuacha maisha yetu kama Wanyarwanda tunavyoishi sasa.

“Ushauri wa Kikwete ni sawa na kucheza na makaburi ya watu wengi ambao ni ndugu zetu,” alisema Kagame.

Katika hatua nyingine, Rais Kagame alilihimiza jeshi lake kujiimarisha na kuendelea na moyo wa ulinzi wakati wote.

Akiwa mjini Addis Ababa, katika mkutano uliojadili suala la amani ya Kongo pamoja na ukanda wa maziwa makuu, Rais Kikwete alitoa ushauri ambao uliwagusa pia Rais Yoweri Museveni na Joseph Kabila, ambao aliwataka kufanya mazungumzo na waasi wanaopingana na serikali zao.

Rais Kikwete alisema Rwanda inapaswa kufanya mazungumzo na waasi wa FDRL ambayo ni njia muafaka ya kutafuta amani katika eneo la Mashariki ya Kongo.
 
 
Inadaiwa kuwa ushauri huo wa Rais Kikwete ulipokelewa kwa hisia tofauti na viongozi wa ngazi za juu, hususan wale wa usalama wa serikali ya Rwanda na wapo walioamini kuwa hana huruma na maisha ya Wanyarwanda, kwa kile walichodai kuwa ameonyesha kuyapendekeza makundi ya waasi ya FDLR, ambayo yanahusishwa na wapiganaji wa Interahamwe, yaliyoendesha mapigano mwaka 1994.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, amekwishakaririwa akieleza kuwa ushauri wa Rais Kikwete ni jambo lisilokuwa la kawaida lenye udhaifu.

Naye mmoja wa wasomi nchini humo aliyezungumzia ushauri wa Rais Kikwete, ambaye ametambulishwa kwa jina moja la Profesa Rwanyindo, aliuelezea ushauri wa Rais Kikwete kuwa upo katika mtazamo wa kupuuza historia iliyolikuta taifa hilo hapo nyuma.

Wahanga wa mauaji ya kimbari wamemuandikia barua Rais Barack Obama wakimuelezea Kikwete anavyoonea huruma kundi la watu ambao Marekani yenyewe imeshawajumuisha katika makundi ya kigaidi.

Dadisi za wachambuzi nchini Rwanda zinaelezea kuwa kauli ya Rais Kikwete ni sawa na mapendekezo yasiyokuwa katika mpangilio kwa kupendelea waasi wa FDLR, hali inayozua wasiwasi kuwa anaweza asiwe na msaada wa kusimami amani, ustawi na ushirikiano katika nchi za ukanda wa maziwa makuu.

Wakati huo huo, Rais Kagame ameyashutumu mashirika mbalimbali vya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na uhusiano wenye mashaka na mamlaka za Afrika.

“Wapo kwa sababu moja …wametoka kwa wakoloni waliotutawala, natolea mfano kwa haya waliyotusema kuwa sisi tunahusika na machafuko yanayotokea Kongo,” alisema Rais Kagame.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...