RAIS
wa Rwanda, Paul Kagame, amemshambulia kwa maneno makali Rais Jakaya
Kikwete, akijibu ushauri alioutoa kwa serikali yake wa kukaa katika meza
ya mazungumzo na waasi wa kikundi cha Democratic Force for the Liberation of Rwanda (FDLR),
ili kumaliza mapigano. Shirika la Habari la Rwanda, linalojulikana kwa
jina la News of Rwanda, jana lilimkariri Rais Kagame akitoa maneno ya
kejeli na yenye mwelekeo wa kupuuza ushauri wa Rais Kikwete.
Kauli hiyo ya Rais Kagame, ambayo pia imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya habari, inaonyesha kukerwa na ushauri wa Rais Kikwete ambao ameuita upumbavu uliojazwa ujinga.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kagame kutoa kauli hiyo tangu Rais Kikwete alipotoa ushauri huo, wakati akizungumza katika kikao cha Mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika mapema mwaka huu, mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Waasi wa FDLR ambao jamii yao ni Watutsi, walikimbilia nchini Kongo baada ya mapigano ya kimbari ya mwaka 1994, yaliyosababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wamekuwa wakiendesha chokochoko dhidi ya Serikali ya Rais Kagame.
Akizungumza katika sherehe ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi maofisa 45 wa jeshi lake, Rais Kagame alisema ushauri wa kufanya mazungumzo na waasi wa FDLR ni ujinga na haupo katika historia ya Wanyarwanda.