kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen ameongezewa mkataba wa miaka miwili, leo ametaja kikosi cha timu hiyo kitakachoingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Morocco mwezi ujao kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia mwakani.
Katika kikosi hicho, kocha huyo Mdenmark amemuorodhesha kipa wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’ pamoja na makipa wengine watatu, Juma Kaseja wa Simba SC, Mwadini Ally na Aishi Manula wa Azam.
Upande wa mabeki amewaita Erasto Nyoni, Aggrey Morris wa Azam, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga SC, Shomary Kapombe wa Simba SC na Yahya Mudathir wa Azam.
Kwa viungo, Poulsen amewaita Haroun Chanongo, Mrisho Ngassa wa Simba SC, Simon Msuva, Frank Domayo, Athumani Iddi ‘Chuji’ wa Yanga SC, Salum Abubakar, Khamis Mcha ‘Vialli’ wa Azam FC na washambuliaji ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya DRC, John Bocco wa Azam FC, Juma Luizio wa Mtibwa Sugar na Zahor Pazi wa JKT Ruvu.