Afisa Habari wa TFF Boniface Wambura.
LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA 25
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea
katika raundi yake ya 25 kesho (Mei Mosi) kwa mechi tano zitakazochezwa
katika miji ya Dar es Salaam, Turiani, Morogoro na Mlandizi.
Licha ya kuwa tayari Yanga imetawazwa
kuwa mabingwa wa VPL msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union
itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni moja kati ya
zitakazovuta macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu nchini.
Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na
mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles
Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah
wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa.
Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza
saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh.
8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati
VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.
Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa African
Lyon katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic
Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani
Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo
wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro.