Afisa Habari wa TFF Boniface Wambura.
LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA 25
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea
katika raundi yake ya 25 kesho (Mei Mosi) kwa mechi tano zitakazochezwa
katika miji ya Dar es Salaam, Turiani, Morogoro na Mlandizi.
Licha ya kuwa tayari Yanga imetawazwa
kuwa mabingwa wa VPL msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union
itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni moja kati ya
zitakazovuta macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu nchini.
Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na
mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles
Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah
wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa.
Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza
saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh.
8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati
VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.
Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa African
Lyon katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic
Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani
Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo
wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro.
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi,
Dar es Salaam na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa
mechi kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Nayo Ruvu Shooting itakuwa
nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili
Oljoro JKT kutoka Arusha.
MTANZANIA APEWA ITC KUCHEZA MSUMBIJI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Yusuf
Kunasa kucheza nchini Msumbiji.
Shirikisho la Mpira wa Miguu cha Msumbiji
(FMF) lilituma maombi TFF kumuombea hati hiyo Kunasa anayekwenda
kujiunga na timu ya Estrela Vermelha da Beira inayocheza Ligi Kuu nchini
humo.
Kunasa ambaye msimu huu hakuwa na timu
(free agent) amejiunga na timu hiyo akiwa mchezaji wa ridhaa (amateur).
Zaidi ya wachezaji kumi kutoka Tanzania hivi sasa wanacheza katika klabu
mbalimbali nchini Msumbiji.
MECHI YA SIMBA, POLISI MOROGORO YAINGIZA MIL 18/-
Mechi namba 163 ya Ligi Kuu ya Vodacom
iliyochezwa juzi (Aprili 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na kumalizika kwa Simba kuibuka ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya
Polisi Morogoro imeingiza sh. 18,014,000.
Watazamaji 3,145 walikata tiketi
kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000,
sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh.
3,564,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh.
2,747,898.31.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho
kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa
2,841 na kuingiza sh. 14,205,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa
ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 36 na kuingiza sh.
720,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia
15 ya uwanja sh. 1,812,331.75, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi
sh. 1,087,399.05, Kamati ya Ligi sh. 1,087,399.05, Mfuko wa Maendeleo ya
Mpira wa Miguu (FDF) sh. 543,699.53 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Dar es Salaam (DRFA) sh. 422,877.41.
No comments:
Post a Comment