Ni
nadra kutokea lakini wafuasi wa vyama vya siasa vya CCM na Chadema,
wameungana kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuhusu kero ya maji eneo la
Kimara-Golani, Dar es Salaam.
Rais Kikwete alikutana na hali hiyo wakati akifungua Daraja
la Kimara jana, tukio hilo liliwakusanya watu wengi hasa wanachama wa
CCM na Chadema waliokuwa wamevalia sare za vyama vyao.
Wafuasi wa Chadema waliongozwa na Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika ambao walikuwa wakipeperusha bendera za chama chao na kuimba
nyimbo mbalimbali huku wakidai maji. Hata hivyo, kutokana na hali hiyo,
wafuasi wa CCM waliungana na wenzao wa Chadema, kupiga kelele juu ya
suala hilo kiasi cha kugusa hisia za Rais Kikwete.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa daraja hilo, Rais Kikwete
aliahidi kuitisha kikao Jumatatu ijayo kitakachomhusisha Profesa
Maghembe na maofisa wa wizara yake, wabunge wa Dar es Salaam, Mkuu wa
Mkoa, wakuu wa wilaya ili kuweka mikatati ya pamoja kutafuta ufumbuzi wa
suala hilo.
“Ninaomba Machi 25... tukutane ili tuweke mikakati ya pamoja
kutafuta ufumbuzi wa suala hili,” alisema Rais Kikwete.
Akiwa Hospitali ya Mwananyamala, Rais Kikwete alizindua
maabara ya kisasa kwa ajili ya uchunguzi na akazungumzia suala la dawa
za kulevya kwa kusema atahakikisha mapambano yanaendelea kwani dawa hizo
zinaua nguvu kazi ya taifa ambayo ni vijana.