Thursday, March 21, 2013

KISA KINENE KESI YA LWAKATARE


MBOWE ASEMA HUO NI MTIRIRIKO WA MABAVU YA DOLA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilimfutia kesi ya makosa ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph, kisha kuwakamata tena na kuwafungulia kesi mpya yenye mashitaka yaleyale.
Awali ilielezwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka ( DPP), Dk. Eliezer Feleshi, aliwasilisha hati ya kuwafutia kesi washitakiwa kwa sababu hana haja ya kuendelea nayo.
Hata hivyo baada ya kuachiwa, Lwakatare na mwenzake walikamatwa tena na kufikishwa mahakamani hapo kisha kufunguliwa kesi mpya namba 6/2013 ambayo imepangiwa kwa Hakimu mpya, Aloyce Katemana.
Katika kesi ya awali namba 37/2013 iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Lwakatare na wenzake Machi 18, mwaka huu, jana ilikuwa imekuja kwa ajili ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, kuitolea uamuzi wa ama kuwapatia dhamana washitakiwa hao au la.
Lakini Hakimu Mchauru alijikuta akishindwa kutoa uamuzi wake kwa sababu mawakili viongozi wa serikali, Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo, waliwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.
“Kwa kuwa kesi hii Na. 37/2013 ilifunguliwa na upande wa Jamhuri Machi 18, mwaka huu, na leo kesi hii ilikuja kwa ajili ya mahakama kutolea uamuzi wa maombi ya washitakiwa kupatiwa dhamana au la, pamoja na maombi mengine…mahakama hii inasema haitaweza kutoa uamuzi wake kwa sababu DPP amewasilisha hati ya kutotaka kuendelea kuwashitaki, hivyo mahakama hii inawafutia kesi washitakiwa wote,” alisema Hakimu Mchauru.
Baada ya Hakimu Mchauru kuwafutia kesi, askari kanzu waliwakamata tena washitakiwa hao na kuwaweka chini ya ulinzi na ilipofika saa 4:20 asubuhi, waliingizwa tena katika ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi mwingine, Aloyce Katemana.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...