WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa
kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Pasaka Machi 31 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Taarifa kwa vyombo
vya habari, iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya
tamasha hilo, Alex Msama ilieleza kuwa tayari Ofisi ya Waziri Mkuu
imeshathibitisha kuhusiana na ujio wake kwenye tamasha hilo.
“Tunafurahi kwamba tamasha letu mwaka
huu Dar es Salaam mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mwaka
jana alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe,” ilisema taarifa hiyo
ya Msama.
Waimbaji mbalimbali wa ndani na nje ya
Tanzania wanatarajiwa kutumbuiza kwenye tamasha hilo, ambapo wan je ya
nchi ni Sipho Makhabane wa Afrika Kusini, Ephraim Sekeleti wa Zambia na
Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi
Kenya, pamoja na kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali Rwanda.
Kwa upande wa wasanii wa hapa nchini
watakaotumbuiza ni Upendo Kilahiro, Rose Muhando, Upendo Nkone na John
Lissu, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.
Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es
Salaam Machi 31 na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine
Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora Iringa na Aprili 6 Uwanja wa
Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba,
Mwanza.