Mabao matatu yaliyofungwa na
Jackson Mwanza, Clatons Chama na Winston Kalenga, yamesababisha siku ya
Simba ‘Simba Day’ kuwa chungu baada ya Zesco kuizamisha miamba hiyo kwa
mabao 3-0.
Safu ya ulinzi ya Simba iliyoshindwa kuelewana
iliizawadia Zesco ya Zambia mabao matatu, wakati wa mchezo huo wa
kuadhimisha siku muhimu ya klabu hiyo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Ikiwa inatumia mchezo huo kwa ajili ya
kutambulisha wachezaji wake wapya iliyowasajili, Simba iliendeleza
rekodi yao ya kutoshinda katika mchezo wa Simba Day tangu kuanza
kuiadhimisha siku hiyo.
Ukihudhuriwa na mgeni rasmi, Naibu Waziri wa
Fedha, Adam Malima, ambaye aliwataka Simba kucheza kimataifa zaidi,
kikosi hicho cha kocha Zdravko Logarusic kilijikuta katika siku mbaya
msimu huu.
Simba ilianza kuruhusu bao la kwanza dakika ya 14, wakati Mwanza akiunganisha kwa kichwa krosi safi kutoka wingi ya kushoto. Mabeki wa kati wa Simba, Donaldi Mosoti na Joseph
Owino walionekana kushindwa kujua nani wa kumkaba na kumuacha Mwanza
akiruka peke yake.
Mshambuliaji mpya wa Simba, Paul Kiongera
alishirikiana vizuri na Amissi Tambwe, lakini hawakuwa makini kwani
Tambwe alikosa nafasi kadhaa za wazi.
Nafasi ya kwanza kwa Tambwe ilikuwa dakika ya
saba, wakati shuti la Kiongera lilipopanguliwa na kipa wa Zesco, lakini
Tambwe alishindwa kuumalizia mpira huo vizuri.
Simba ilikuwa na kipindi cha pili kibaya zaidi,
kwani mabeki wake wa kati walisababisha penalti kwa kumwangusha Chama
aliyekuwa anakwenda kufunga na mshambuliaji huyo kuukwamisha mkwaju huo
wavuni.
Dakika tano za nyongeza zilikuwa mbaya zaidi kwa
Simba, ambapo shambulizi la kushtukiza lilizaa bao baada ya mabeki wa
Simba kwa mara nyingine wakishindwa kuondoa krosi ndogo ambayo
ilimaliziwa kiufundi na Kalenga. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz