Monday, August 11, 2014

ZESCO YATIBUA SHEREHE YA SIMBA DAY...!!!

Mabao matatu yaliyofungwa na Jackson Mwanza, Clatons Chama na Winston Kalenga, yamesababisha siku ya Simba ‘Simba Day’ kuwa chungu baada ya Zesco kuizamisha miamba hiyo kwa mabao 3-0.
Safu ya ulinzi ya Simba iliyoshindwa kuelewana iliizawadia Zesco ya Zambia mabao matatu, wakati wa mchezo huo wa kuadhimisha siku muhimu ya klabu hiyo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ikiwa inatumia mchezo huo kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wake wapya iliyowasajili, Simba iliendeleza rekodi yao ya kutoshinda katika mchezo wa Simba Day tangu kuanza kuiadhimisha siku hiyo.
Ukihudhuriwa na mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, ambaye aliwataka Simba kucheza kimataifa zaidi, kikosi hicho cha kocha Zdravko Logarusic kilijikuta katika siku mbaya msimu huu.
Simba ilianza kuruhusu bao la kwanza dakika ya 14, wakati Mwanza akiunganisha kwa kichwa krosi safi kutoka wingi ya kushoto. Mabeki wa kati wa Simba, Donaldi Mosoti na Joseph Owino walionekana kushindwa kujua nani wa kumkaba na kumuacha Mwanza akiruka peke yake.
Mshambuliaji mpya wa Simba, Paul Kiongera alishirikiana vizuri na Amissi Tambwe, lakini hawakuwa makini kwani Tambwe alikosa nafasi kadhaa za wazi.
Nafasi ya kwanza kwa Tambwe ilikuwa dakika ya saba, wakati shuti la Kiongera lilipopanguliwa na kipa wa Zesco, lakini Tambwe alishindwa kuumalizia mpira huo vizuri.
Simba ilikuwa na kipindi cha pili kibaya zaidi, kwani mabeki wake wa kati walisababisha penalti kwa kumwangusha Chama aliyekuwa anakwenda kufunga na mshambuliaji huyo kuukwamisha mkwaju huo wavuni.
Dakika tano za nyongeza zilikuwa mbaya zaidi kwa Simba, ambapo shambulizi la kushtukiza lilizaa bao baada ya mabeki wa Simba kwa mara nyingine wakishindwa kuondoa krosi ndogo ambayo ilimaliziwa kiufundi na Kalenga. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...