Friday, October 27, 2017

VIDEO: RAIS MAGUFULI AFANYA UTEUZI MBALIMBALI

Rais John Magufuli amemteua aliyekuwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, huku aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu akiteuliwa kuwa balozi.

Dk. Kashilillah ameteuliwa ikiwa ni takriban wiki tatu kupita tangu alipoondolewa katika wadhifa wa Katibu wa Bunge, nafasi iliyochukuliwa na Stephen Kigaigai.
Rais Magufuli Mei 28,2017 alitengua uteuzi wa IGP Mangu na kumteua Simon Sirro kushika wadhifa huo. Mangu anasubiri kupangiwa kituo cha kazi pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Dk Aziz Mlima.

Uteuzi wa Rais Magufuli, uliotangazwa jana Alhamisi Oktoba 26, 2017 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi uliwahusu pia, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wakuu wa mikoa ambao wataapishwa leo Ijumaa Oktoba 27, 2017 mchana Ikulu jijini Dar es Salaam.

Balozi Kijazi amesema Rais Magufuli amewateua naibu makatibu wakuu wapya saba na kuwapandisha naibu makatibu wakuu wanne kuwa makatibu wakuu kwenye baadhi ya wizara.

Pia, amewahamisha makatibu wakuu wanne na naibu katibu mkuu mmoja kwenda kwenye wizara nyingine.

Balozi Kijazi amesema katika nafasi za wakuu wa mikoa, Rais Magufuli amewateua wa mikoa sita, miongoni mwao ni aliyewahi kuwa waziri katika utawala uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Adam Malima anayekwenda Mkoa wa Mara.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti amepandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara. Balozi Kijazi amesema wakuu wa mikoa walioondolewa kutokana na kustaafu ni Joel Bendera (Manyara), Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga (Geita) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi mstaafu wa Polisi, Zelothe Stephen (Rukwa).

Wakuu wa mikoa walioachwa ni wa Mtwara, Halima Dendego, Jordan Rugimbana (Dodoma) na Dk Charles Mlingwa (Mara). Amesema Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Joackim Wagambo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme akiwa mkuu wa mkoa huo.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...