Kaimu kiongozi wa shughuli za serikali bungeni Mh. Samuel Sitta.
SERIKALI imesema haiwezi kubadili msimamo wake kuhusu upigaji wa Kura
ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, licha ya kuwepo maoni ya viongozi
wa dini ambao wanataka jambo hilo lisitishwe.
Kaimu Kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, Samuel Sitta alisema
jana mjini hapa kuwa pamoja na kuwepo kwa tofauti kati ya Jukwaa la
Wakristo na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, msimamo wa Serikali uko pale pale.
Sitta, ambaye anakaimu shughuli za serikali bungeni kutokana na
kutokuwepo kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema Serikali inakubaliana
na maoni ya Kardinali Pengo kuwa waumini waachwe waamue wenyewe kuhusu
Katiba Inayopendekezwa.
Alisema kama viongozi wa dini wamegawanyika hakuna namna ya kuwafanya
wawe na kauli moja, lakini akasisitiza kuwa jambo la msingi ni kuachwa
kwa mtu aamue mwenyewe aina ya kura atakayopiga.
Hivi karibuni Pengo alitofautiana na Baraza la Maaskofu (TEC) na
Jukwaa la Wakristo ambao wanataka upigaji wa kura ya maoni usitishwe,
kwa maelezo kuwa wananchi hawajapewa muda wa kuisoma na kuielewa katiba
hiyo na kama Serikali itang’ang’ania ni vyema waumini wa kanisa wapige
kura ya hapana. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Sitta, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Kutunga Katiba
(BMK) alisema Serikali haiwezi kuwakadiria waseme nini au mambo yao
yaishe vipi. “Demokrasia yoyote huwa na mawazo ambayo yanatofautiana.
Msimamo wa serikali ni ule ule kwamba tutaendelea mpaka kupiga kura ya
maoni,” alisema Sitta.
Mwanasiasa huyo mkongwe alisema; “Wananchi wataamua wenyewe na wale
watakaoona kwamba wameshawishiwa na wakuu wao wa dini kufuata hilo tamko
hawawezi kuwazuia na wale watakaoona kuwa hakuna suala la imani ni
utashi wa kisiasa nao watakuwa na msimamo wao.”
Sitta alisisitiza kuwa ratiba ya Serikali haibadilishwi na tofauti ya
kimtizamo kutoka kwa viongozi hao na kwamba Kura ya Maoni itapigwa
Aprili 30 kama ilivyopangwa.
Mvutano ulioibuka hivi karibuni kati ya Kadinali Pengo na viongozi
wengine wa madhehebu ya Kikristo, umeibua mjadala mzito kwenye jamii
huku wengine wakieleza kuwa viongozi hao wanawayumbisha wananchi.
Kauli ya Pengo imekuja huku tayari tamko ambalo lilitolewa na TEC
limesambazwa makanisani na tayari lilishasomwa katika baadhi ya parokia
na vigango.
Msimamo wa Kadinali Pengo ni kwamba wananchi waisome na waielewe
Katiba hiyo, kwani ndiyo wajibu wa msingi ambao Wakristo wanao kwa sasa
ili kupiga kura inayostahili wakati ukifika.
Kuhusu agizo la waumini kuikataa Katiba Inayopendekezwa, Kadinali
Pengo katika maoni yake anaeleza kuwa wao wakiwa viongozi wa watu,
hawana mamlaka wala uwezo huo, bali wenye uwezo ni wananchi wenyewe.
Hata hivyo, Kadinali Pengo alitaka tamko hilo lisambazwe kwenye
parokia na vigango vyote vya Jimbo Kuu la Dar es Salaam ili waumini
wasomewe, wauelewe kwanza, ili hatimaye waweze kufanya uamuzi sahihi
wakielewa ni nini wanachokitakiwa kukifanya.
Jukwaa la Wakristo linaundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la Makanisa ya
Kipentekoste Tanzania (CPCT). Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment