Wednesday, March 18, 2015

UBUNGE WA ZITTO WANING'INIA...!!!

Zitto Kabwe 

Kitendo cha kutupiana mpira kati ya Ofisi ya Bunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu hatima ya Zitto Kabwe, kimeufanya ubunge wa mbunge huyo kuendelea kuning’inia huku mwenyewe akitazamiwa leo kueleza anachoita ‘maamuzi magumu’.

Kutupiana mpira kulijitokeza jana baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kusema Bunge linasubiri taarifa rasmi ya kufukuzwa uanachama kwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kutoka NEC, ambayo hata hivyo, nayo ilisema inasubiri taarifa kutoka Chadema huku chama hicho kikisema kinashughulikia kwanza kesi zinazowakabili wanachama wake wanaotuhumiwa kumpiga aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa.
Wakati Makinda akieleza hayo, taarifa kutoka kwa watu wa karibu wa mbunge Zitto zilieleza kuwa leo ataibuka bungeni kwa nia ya kuwaaga wabunge kama alivyoahidi wiki iliyopita. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Zitto alishindwa kukubali wala kukataa, lakini akathibitisha kuwa atahudhuria kikao cha Bunge leo.
Chadema ilimvua Zitto uanachama wiki iliyopita saa chache baada ya Mahakama Kuu kutupa shauri lake alilofungua akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa nyaraka za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote. Alipata amri ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili.
Akifafanua suala hilo, Makinda alisema, “Unajua suala hili lilikuwa mahakamani, hivyo ni lazima tupewe taratibu zote za kimahakama. Kama kila kitu kikiwasilishwa moja wa moja uamuzi huo utatangazwa wazi. Unajua suala hili lipo wazi na sisi kama Bunge tunachokisubiri ni taarifa tu.”
Hata hivyo, alisema kwa muda uliobaki wa miezi saba kabla ya uchaguzi mkuu, haiwezekani ukafanyika uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, “Labda kama ingekuwa imebaki miezi 12 au zaidi kabla ya uchaguzi mkuu, hapo ungeweza kufanyika uchaguzi mdogo.”
Katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya muda mfupi kabla ya kuwaaga wananchi wa jimbo lake Jumapili iliyopita, Zitto alisema hatima yake ya ubunge itajulikana wiki hii kama Bunge likipata taarifa za yeye kufukuzwa uanachama.
Alisema iwapo hatua hiyo itakamilika, ataeleza hatua ambazo atazichukua na kufafanua kuwa mpaka sasa hajapata barua ya wito wa kwenda kujitetea katika Kamati Kuu ya Chadema, hivyo mpaka sasa bado ni mwanachama wa Chadema.
Alisema ataendelea kuwatumia Watanzania akiwa mwakilishi wao kupitia jimbo lolote nchini na kusisitiza kuwa atatoa kauli iwapo atagombea ubunge katika jimbo lipi na kwa tiketi ya chama kipi cha siasa.
 Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba aliliambia gazeti hili jana kwa simu kwamba bado hawajapata taarifa ya maandishi ya kufukuzwa kwa Zitto, hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Gazeti hili lilipowasiliana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Bara, John Mnyika kama chama hicho kimetoa taarifa za Zitto NEC kuhusu kuvuliwa kwake uanachama, alijibu kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wanashughulikia kesi zinazowakabili wanachama wa chama hicho wanaotuhumiwa kumpiga aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Slaa.
“Kipaumbele chetu leo (jana) ni mahakamani kutokana na ukubwa wa yanayoendelea katika tukio hili,” alisema Mnyika kupitia ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene.

Chadema Kigoma wampania
Katika hatua nyingine, Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Mkoa wa Kigoma, limesema litamshughulikia   Zitto Kabwe iwapo ataamua kugombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini badala ya Kigoma Kaskazini.
Akihutubia wakazi wa Kata ya Gungu mjini hapa juzi, mwenyekiti wa baraza hilo, Omary Gindi alisema wamejiandaa kushinda ubunge na kutetea nafasi ya kuongoza Halmashauri ya Kigoma Ujiji kama walivyofanya mwaka 2010.
Gindi alisema watambana baada ya Zitto kudai hatagombea kwenye jimbo alilokuwa anaongoza kupitia Chadema na badala yake amejipanga kugombea katika Jimbo la Kigoma Mjini kubadilisha na Peter Serukamba (CCM).
“Zitto aje tu hapa Kigoma Mjini. Tutamuuliza aliwafanyia nini watu wa jimbo lake kiasi kwamba amemaliza kero zao na kuamua kuhama, vinginevyo tutawaeleza wananchi kwamba hafai na amekimbia kwao kwa sababu wananchi wamemwambia hawatamchagua tena kutokana na kushindwa kushirikiana na wapiga kura wake,” alisema Gindi.
Alisema watu wa Kigoma wanaipenda na kuiunga mkono Chadema kwa vile baadhi yao walifungwa jela, kupoteza mali, kujeruhiwa na kupata ulemavu na wengine kukosana na wake au waume zao, jambo lililowafanya kujiona ni sehemu ya chama hicho.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Shaaban Madede aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
“Lazima mhakikishe CCM inang’oka madarakani ili Chadema iweze kuongoza dola na kupigania masilahi ya watu, kwa vile sehemu nyingi kuna kero ya huduma mbovu za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara vijijini, suluhisho pekee ni kuiondoa CCM madarakani,” alisema Madede. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...