Thursday, January 08, 2015

ESCROW YAWANG'OA WAFANYAKAZI 7 TRA

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (kulia), akimjulia hali aliyejifungua watoto pacha katika Hospitali ya Mwananyamala, Mwamvita Kilasi wakati waziri huyo alipokwenda hospitalini hapo kutoa misaada mbalimbali katika wodi ya watoto. Waziri huyo alikuwa akisheherekea siku yake ya kuzaliwa.

Sakata la ufisadi wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow limewang’oa wafanyakazi saba wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wafanyakazi hao wamesimamishwa kazi ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge kuhusu ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu kashfa hiyo.
Wengine ambao tayari wameshawajibika katika kashfa hiyo ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliyejiuzulu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyefukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliyesimamishwa kupisha uchunguzi. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema pia Serikali imetoa siku 30 kwa walionufaika na mgawo wa mamilioni ya fedha kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering Ltd, James Rugemalira kulipa kodi kulingana na kiasi walichopokea.
Hatua TRA
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kwa wafanyakazi wa TRA waliohusika na sakata hilo Nchemba alisema; “Mpaka sasa wafanyakazi saba wamesimamishwa kazi ili kupisha vyombo vinavyohusika viweze kuchukua hatua zaidi na mimi nilikuwa nasema wachukue hatua zaidi kwa kuwa haiwezekani badala ya Dola milioni 20 mtu anaweka fedha za Tanzania Sh20 milioni, hii ni makusudi au njama za kutekeleza wizi huo.
“Ukisema ulikuwa unajua ni njama, hivyo hustahili kuwapo na ukisema ulikuwa hujui pia hustahili kuwapo. Huwezi kusomeshwa kwa kodi ya Watanzania halafu unapopewa fursa ya kusimamia makusanyo ya kodi ukafanya unavyojua,” alisema Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM).
“Mtu hawezi kuiba Sh30 bilioni halafu ukamfukuza kazi pekee, hii utakuwa unampa likizo ya kwenda kutumia fedha hiyo, ifike mahali mtu anapoiba anafilisiwa mali zake ili kuwa fundisho kwa wengine.”
Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) alisema kitendo cha mtumishi wa umma kufanya vibaya na kisha kuhamishiwa sehemu nyingine haitakiwi kuwapo kwa kuwa hiyo ilikuwa inatokea wakati watumishi wakiwa wachache.
“Unajua zamani unakuta wahandisi ni wachache unapomfukuza moja kwa moja unakosa wa kukaa nafasi hiyo lakini sasa watumishi na wataalamu ni wengi mtu akikosea ni kumwondoa akatafute kazi sehemu nyingine kwani hatutakiwi kufumbia macho vitendo hivi,” alisema Nchemba.
Waliopata mgawo
Kuhusu walionufaika na mgawo huo, Nchemba alisema “TRA imeshawatumia fomu za mahesabu ya kodi wanazotakiwa kulipa na wao sasa wakae na wahasibu wao waseme wanatakiwa kulipa kiasi gani ndani ya siku 30 kuanzia Januari Mosi mwaka huu.
Baadhi walionufaika na mgawo huo na kiwango walichopokea katika mabano ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni), Profesa Tibaijuka (Sh1.6 bilioni), Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja (Sh40.4 milioni), aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Mbunge mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni), aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni).
Majaji walioingiziwa fedha ni Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji A.K Mujulizi (Sh40.4 milioni).
Siku ya kuzaliwa
Aidha, jana ilikuwa ni siku yake ya kuzaliwa, Nchemba alifanya kazi mbalimbali za kujitolea na akisema: “Sasa nimetimiza miaka 40 ya utumishi, zamani nilikuwa natimiza miaka ya utegemezi lakini hii ni ya utumishi.”
Alipoulizwa kama kauli hiyo ina uhusiano na mchakato wa kuwania urais alisema: “Sasa nina kazi moja ya kumsaidia waziri wangu (Saada Mkuya) na Rais Jakaya Kikwete. Licha ya kuwa naibu waziri bado ni naibu katibu mkuu ambaye natakiwa kusimamia kanuni, miongozo na maadili ya chama changu lakini muda utakapofika kama ni mto tutavuka pamoja,” alisema Nchemba.
Katika kuadhimisha siku hiyo, Nchemba alitoa misaada kwa wajawazito katika Hospitali ya Mwananyamala, Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Chakuwama Sinza na kuchangia damu katika Kituo cha Mpango wa Taifa wa Damu Salama.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sophinias Ngonyani alimweleza Nchemba changamoto wanazokutana nazo ikiwamo upungufu wa wodi na vitanda ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa wanaopokewa. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...