Waziri wa zamani wa Wizara ya
Nishati na Madini, Daniel Yona ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
kuwa mchakato wa kumpata mkaguzi wa madini ya dhahabu ulifuata
utaratibu kwa kusimamiwa na Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Aliyaeleza hayo jana alipojitetea dhidi ya
mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara
ya Sh11.7 bilioni yanayomkabili na wenzake wawili.
Akiongozwa na wakili wake, Eliasa Msuya kutoa
ushahidi wa utetezi mbele ya jopo la mahakimu watatu wanaoisikiliza kesi
hiyo, John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela, Yona alidai kuwa
wakati wakiendelea na utaratibu wa kumtafuta mkaguzi wa dhahabu walipata
ushauri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Alidai kuwa utaratibu wa kumtafuta mkaguzi huyo
nchini ulitokana na malalamiko ya wananchi, Bunge, vyombo vya habari na
mashirika yasiyo ya kiserikali mwaka 2002, kuhusu mapato ya madini hayo
yaliyokuwa yakichimbwa na kampuni tano za kigeni. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Wizara ya Nishati iliamua kuhakiki gharama za
madini hayo kwa kuwa BoT ndiyo iliyosimamia akaunti za kampuni hizo
ndani na nje ya nchi, iliruhusu kufungua akaunti zake pamoja,
tulikubaliana kumtafuta mkaguzi wa dhahabu,” alieleza Yona.
Yona alidai kuwa BoT na wizara, walianza mchakato
huo wa kuhakikisha anapatikana mzabuni mkaguzi wa dhahabu kwa kufuata
utaratibu na sheria za nchi.
Alidai kuwa baada ya kufanyika kwa majadiliano,
Mei 11, 2003 aliamwandikia dokezo Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa
kuhusu ukaguzi wa dhahabu.
Akiendelea kujitetea, Yona alidai kuwa
alimfahamisha Rais Mkapa kuhusu majadiliano waliyoyafanya kati ya Wizara
ya Nishati, Wizara ya Fedha, BoT na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa
yanaendelea vizuri.
Aliongeza kuwa Machi 3, 2003, alimwandikia Rais
dokezo kuomba aruhusu kutekeleza ukaguzi wa dhahabu kwa kufuata taratibu
na sheria.
Yona alidai kuwa Machi 20, 2003 Rais alimjibu
kwamba anakubali waendelee na mchakato haraka na kwamba wao walimwahidi
kuwa mchakato huo utazingatia mapato ya nchi na ushauri wa AG na kwamba
walizingatia hilo.
Hata hivyo, Yona hakuweza kuendelea kutoa ushahidi
wake wa utetezi baada ya Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyekomya
kupinga kupokewa kwa nyaraka ya kielelezo cha ushahidi kutoka Ofisi ya
AG.
Baada ya kutolewa kwa hoja hiyo, mahakimu hao
walikubaliana kuiahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kumpa nafasi
wakili wa serikali, Oswald kujiridhisha na kielelezo hicho.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, Yona na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Washtakiwa hao wanakabiliwa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Inadaiwa kwamba walitenda makosa hayo Agosti, 2002
kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart ya
nchini Uingereza kinyume cha sheria. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment