Thursday, September 11, 2014

'SARAFU YA SH 500 NI ISHARA MBAYA'




Huo ni uamuzi wa kawaida tu wa kuiongezea uimara wa kukaa muda mrefu kama BoT walivyosema. Kinach opunguza nguvu ya fedha siyo sarafu wala noti...hivyo uchumi tulionao na mfumuko wa bei hatujafikia kiwango cha kusema Shilingi imeshuka thamani,”  Dk Urassa  
Baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutangaza matumizi ya sarafu mpya ya Sh500, baadhi ya wachumi na wadau wa sekta binafsi nchini wamesema hatua hiyo inaashiria kuporomoka kwa thamani ya shilingi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wachumi hao walisema kuwapo kwa sarafu hiyo inaonyesha uwezo wa Shilingi kununua bidhaa unazidi kupungua.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Daniel Machemba alisema Serikali ingejikita zaidi kuzuia kushuka kwa thamani  badala ya kuongeza sarafu.

“Kadri unavyoongeza ukubwa wa fedha, ndivyo inavyozidi kushuka thamani. Hii inamaanisha tunakoelekea tunaweza tukawa kama Zimbabwe kuwa na noti hadi ya Sh100 milioni,” alisema Machemba.

Alisema kuna haja ya Serikali kuzuia matumizi makubwa ya fedha za kigeni nchini hususan Dola za Marekani katika taasisi mbalimbali. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Masoko ya Fedha na Mitaji ya Zansecurities, Raphael Masumbuko alisema hatua hiyo huenda ikasaidia fedha kukaa muda mrefu lakini dhana kubwa itakayobaki miongoni mwa wananchi ni Shilingi kushuka thamani.

Alisema tangu enzi za ukoloni, sarafu imekuwa ikionyesha haina thamani, hivyo kuna baadhi wataona Sh500 ni kama Sh100.

“Kwa maana hiyo watu wengi zikiwamo taasisi za fedha kama maduka ya kubadilishia fedha watakuwa wakizikataa kwa kuwa ni mzigo... tabia hiyo ikiendelea inaweza kuifanya Sh500 ikashuka thamani yake,” alisema Masumbuko.

Watilia shaka thamani

Katibu Mkuu wa Chama cha Wahakiki Mizigo Melini, Michael Kimathi alisema hakuna ubishi kuwa uamuzi huo unaonyesha wazi Shilingi imeshuka thamani.

Kimathi alisema tangu mwanzoni mwa utambulisho wake noti zinazotumika sasa zilionekana kutokuwa imara kama za zamani na Sh500 ilikuwa dhaifu zaidi.

“Bila shaka fedha ikiwa katika sarafu thamani yake ni ndogo na tumeanza na hiyo tutaendelea kuiona hadi sarafu ya Sh1,000. Kama ingewezekana ni bora wangetengeza noti imara kuliko kuifanya sarafu,” alisema Kimathi.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Goodluck Urassa alisema sarafu haina uhusiano wowote na kushuka kwa thamani ya Shilingi kwa kuwa hali hiyo hupimwa na mfumuko wa bei na kiwango cha kubadilisha fedha.

Alisema hatoshangaa kuwapo kwa sarafu ya Sh1,000 au 2,000 kwa kuwa kuna nchi nyingi zenye fedha yenye nguvu kubwa ulimwenguni, lakini wana sarafu kubwa huku akitolea mfano Dola 10 ya Marekani ambayo ikibadilishwa na Shilingi ya Tanzania ni takriban Sh16,000 na 17,000.

Sarafu hiyo ya Sh500 inatarajiwa kuanza kutumika Oktoba mwaka huu kama BoT ilivyotangaza. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...