Mpango wa
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta wa kutaka ya wajumbe
wake walioko nje ya nchi kupiga kura kupitisha Katiba inayopendekezwa,
umepingwa na wasomi, ukielezwa ni kinyume na kanuni za Bunge na sheria
za nchi.
Wasomi hao, wanaharakati na wanasiasa wamesema
Tanzania haina utaratibu wa raia wake kupiga kura wakiwa nje ya nchi na
kwamba hiyo ni mbinu ya kufanya udanganyifu.
Juzi, Sitta alisema wajumbe wa Bunge hilo
watakaokuwa nje ya nchi kwa sababu zozote, ikiwamo ya matibabu na Hijja,
watapiga kura hukohuko mara upigaji kura utakapoanza Septemba 26, mwaka
huu na kuwataka wajumbe hao kuacha mawasiliano yao watakapokuwa nje na
kwamba uongozi wa Bunge umeanza kufanya mawasiliano na balozi mbalimbali
za Tanzania, ili wawepo watumishi wake watakaokula kiapo cha kisheria
kusimamia kazi hiyo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk Benson Bana alisema suala la Watanzania kupiga kura wakiwa
nje ya nchi halimo kwenye kanuni zinazoongoza Bunge hilo na ni vizuri
utaratibu huo ukaachwa. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Alisema anachokiona sasa ni Bunge kuendelea
kupoteza fedha za wananchi wakati hakuna maridhiano huku uamuzi ukiwa
umefikiwa kwamba Katiba Mpya itapatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema: “Hata kanuni za mabunge ya Jumuiya za Madola ambazo sisi
tunazifuata ikitokea mjumbe anaumwa anapelekwa kwenye ukumbi wa Bunge
kupiga kura, kura haipigwi sehemu yoyote.
“Hata katika Bunge la Uingereza ikionekana mjumbe
anatakiwa kupiga kura lakini anaumwa atapelekwa ukumbini kwa msaada wa
uongozi wa Bunge, ili aweze kutimiza haki yake ya kidemokrasia lakini
haki hiyo haiwezi kumfuata huko aliko.
“Sitta analichukulia suala la Katiba kama lake
binafsi, utaratibu wa kupiga kura za kificho haukubaliki kwa sababu
utasababisha uchakachuaji,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Utetezi wa Haki za Binadamu
Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema Tanzania haina utaratibu wa
raia wake kupiga kura wakiwa nje ya nchi.
Mwanasheria huyo alisema kinachofanywa na Sitta kinaonyesha namna Bunge la Katiba linavyolazimisha mchakato huo.
“Kituo pekee cha wajumbe wa Bunge Maalumu kupiga
kura ni ndani ya Ukumbi wa Bunge na si vinginevyo. Kinachofanywa na
Sitta ni kuwahadaa Watanzania, mtu anaumwa atapigaje kura wakati hata
kwenye majadiliano hakuwapo? Unalipigia kura jambo ambalo umeshiriki
kwenye majadiliano,” alisema.
Alisema Tanzania haina utaratibu wa raia wake
kupiga kura wakiwa nje ya nchi na kwamba endapo Serikali inataka
kuuruhusu basi ifanye hivyo. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Felix
Kibodya alisema kama kuna idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge Maalumu ambao
wamesafiri kwenda nje ya nchi katika kipindi hiki, basi Bunge
liahirishwe kama ambavyo wadau wamekuwa wakishauri.
“Nani atatuhakikishia usalama wa kura hizo, kama
ni upigaji wa kura za siri nani atatunza siri hizo, tunajiuliza maswali
mengi je, kutakuwa na msimamizi wa upigaji huo wa kura,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania
(Jukata), Hebron Mwakagenda alisema ingawa kuna nchi zenye utaratibu wa
raia wake kupiga kura wakiwa nje ya nchi, Tanzania haina utaratibu huo.
“Sitta anafanya mambo ya ajabu kuanzisha utaratibu
huo, hii inaonyesha mambo yameshakuwa magumu na sasa wanaokoteza kura
popote zilipo,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Iringa, Profesa
Gaudence Mpangala alisema Sitta anataka kuokoteza kura na kwamba Katiba
ni suala la maridhiano na si wingi wa kura... “Ndiyo maana nimekuwa
nikipendekeza Bunge Maalumu lisitishwe kwa sababu linapoteza fedha za
wananchi,” alisema.
Wakili Peter Shayo wa Arusha alisema utaratibu wa
kuwaruhusu wajumbe walioko nje ya nchi kupigia kura Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa ni kukiuka kanuni za Bunge hilo.
“Ukisoma vizuri kanuni za hilo Bunge, kura za siri
zinataka kuwapo kwa mawakala, nje ya nchi watapatikanaje? Maana ama
anapiga kura ya ndiyo au hapana lazima kuwe na wakala anayemwamini, huko
nje wanawapataje?” alihoji.
Hata
hivyo, Mjumbe wa Bunge hilo, Charles Mwijage
alisema haoni tatizo kwa wajumbe watakaokuwa nje ya nchi kupiga wakiwa
huko... “Naamini Mwenyekiti (Sitta) na timu yake ya wataalamu
wamezipitia hizo kanuni na kujiridhisha lakini usisahau kanuni pia
zinaweza kufanyiwa marekebisho kama ni lazima.” Kuwa wa kwanza kupata
habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment