Tuesday, September 02, 2014

SASA UKICHUKUA FEDHA BENKI ROHO MKONONI


Katuni inayoonyesha ujambazi wa kutumia pikipiki na bastola unavyoshika kasi jijini Dar es Salaam. 

Ni roho mkononi. Hayo ndiyo maneno matatu yanayofaa kuelezea hali ilivyo jijini Dar es Salaam na maeneo kadhaa nchini kwa sasa, hasa pale mtu anapobeba fedha nyingi.
Matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha yamekuwa sugu na kusababisha wananchi wanaopeleka au kutoa fedha benki kuvamiwa, kujeruhiwa au kuuawa mchana kweupe na majambazi wanaotumia pikipiki.
Wananchi wamekuwa wakihoji ni kwa jinsi gani majambazi hao hupata taarifa za mtu aliyekwenda benki ama kuweka au kuchukua fedha.
Mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam, Salum Mashati alisema: “Haiingii akilini, utasikia mtu kaporwa fedha akitoka benki. Eti majambazi wanasema kabisa toa hizo milioni 20, wanajuaje kuwa una kiwango hicho? Huenda watu wa benki wanashiriki uhalifu huu.”
Hata hivyo, meneja wa tawi moja la benki lililopo Mlimani City, ambaye hakupenda jina lake litajwe alikanusha madai hayo... “Si kweli kwamba benki zinashirikiana na majambazi kufanya uhalifu huu. Kwanza wahudumu (bank tellers) hawaruhusiwi kuingia na simu wanapohudumia wateja.
“Hata mteja anapoingia benki hukatazwa kuongea na simu au kuandika ujumbe. Mazingira tuliyojiwekea hayaruhusu kabisa mawasiliano kati ya benki yetu na watu wa nje wakati wa kazi. Nadhani vitendo hivi vya ujambazi vinaanzia kwa wateja wenyewe kutoa taarifa juu ya mipango yao kwa watu ambao si waaminifu,” alisema. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Kauli ya Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alitupa lawama kwa wananchi akisema wamekuwa hawaombi ulinzi wa polisi wakati wa kupeleka au kuchukua fedha benki.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwahi kutoa wito pia kwa taasisi za fedha kulindwa na polisi badala ya walinzi binafsi.
“Wakuu wa benki wanaogopa gharama za ulinzi kwa jeshi la polisi ili kuhakikishiwa usalama lakini mwishowe wanaibiwa kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya kile ambacho wangelipa kwa polisi,” alisema.
Baadhi ya matukio
Juni 23, mwaka huu, Sista wa Shirika la Mtakatifu Maria, Parokia ya Mwenyeheri Anwarite, Makoka, Dar es Salaam, Clecensia Kapuli aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi wakati akitoka Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City na kuporwa fedha.
Agosti 8, mwaka huu, Meneja wa Kampuni ya ununuzi wa korosho na ufuta ya Olam, Jaffari Mgumba aliporwa Sh47 milioni baada ya kuchukua fedha za ushirika katika Benki ya DTB Tawi la Quality Plaza.
Mtu mwingine ambaye jina lake halikufahamika alichukua mkopo wa Sh10 milioni, lakini kwa bahati nzuri, kiasi fulani cha fedha kilibaki benki na kingine akafanya malipo palepale na wakati anaondoa akiwa amebaki na Sh2 milioni alivamiwa na majambazi waliomtaka awapatie Sh10 milioni alizochukua.
Tukio jingine la hivi karibuni ni kuuawa kwa mmiliki wa Kampuni ya Sowers African iliyopo mkabala na Mlimani City, Adson Cheyo Agosti 22, mwaka huu alipokuwa akitoka Benki ya KCB kuchukua na kuporwa fedha hizo.
Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na ujumbe uliokuwa ukisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukionya watu kutembea na fedha nyingi katika maeneo ya Mlimani City, Millennium Tower na Kibo Complex kwa madai si salama. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...