Na Hudugu Ng'amilo
MWANASIASA
mkongwe na Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale –
Mwiru, amesema makada wenzake wanaomshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wanakitukana Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema
kumtukana au kumshambulia Jaji Warioba, au wajumbe wengine wa tume hiyo
ni sawa na kukitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza serikali.
Kingunge
alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akichangia sura ya kwanza na ya
sita ya rasimu ya Katiba, ambapo alisema wanaomshambulia Jaji Warioba
wanaonyesha utovu wa adabu, kwa kuwa chama kina maadili na adabu katika
kushughulikia masuala mbalimbali.
"Mimi
sitakubali hata kidogo wajumbe watumie msimamo wa chama kumshambulia
Warioba au wajumbe wengine wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, si
halali kumshambulia Warioba au mjumbe yeyote yule binafsi.
"Mimi ni
Mwana CCM niliyeondoka madarakani siku nyingi lakini naamini kuwa
kumtukana mwenzetu ni sawa na kukitukana chama na sisi tuliopo hapa,
wanaomshambulia Warioba wanakosea sana, hapa tuna rasimu ya Katiba
ambayo ina mawazo tu, hakuna watu ndani ya rasimu hiyo, hatupaswi
kukiuka maadili kwa kuwatukana au kuwakashifu watu," alisema.
Alisema
kilichomo ndani ya rasimu ya Katiba si uamuzi wa mwisho, hivyo wajumbe
hawana sababu ya kumsema, kumtukana au kumkejeli mtu yeyote aliyekuwa
kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kingunge
pia alitumia fursa hiyo kukemea lugha za matusi, vijembe na kejeli
zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wajumbe kwenye mijadala mbalimbali.
"Hatuwezi
kukaa hapa ndani kwa kudhalilishana, wale waliokuwa wakitumia lugha
hizo walikuwa wanatudhalilisha wote. Wengine walitumia lugha hizo kwa
waasisi wetu...Unyenyekevu ni sura moja ya msomi ambaye ametumia fedha
za Watanzania kupata elimu yake," alisema.
Alisema
wajumbe wamekwenda bungeni kuwatafutia wananchi wenzeo Katiba mpya,
iliyo bora na lazima izingatie miaka 50 ya muungano ambao umekuwa na
mafanikio makubwa.
"Katiba
bora lazima iimarishe yale mafanikio tuliyoyapata katika kipindi hicho
ikiwemo muungano, umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu na kuunda
mazingira ya amani na utulivu, kama haiimarishi, haifai hata kidogo.
Haya mafanikio yote yametokana na muundo wa serikali mbili ulioasisiwa
na wazee wetu," alisema.
Hakuna Katiba bila UKAWA
Kingunge
alisema kuwa ili Tanzania ipate Katiba mpya iliyo bora, lazima kuwepo
maelewano ya kuwashirikisha wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Alisema
kitendo cha wajumbe wa UKAWA kususia vikao vya Bunge, kinaonyesha
upungufu mkubwa walionao lakini Katiba mpya haitaweza kupatikana bila ya
wao.
Kingunge aliwaomba wajumbe wa UKAWA warejee bungeni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa Katiba ya wananchi.
Alisema
hata UKAWA wakirejea bungeni ni vema wajumbe wakatambua kuwa kupatikana
kwa Katiba mpya kunahitaji maridhiano ya pande hizo mbili.
"Hatuwezi
kupata theluthi mbili ya kura hasa kwa wajumbe wa kutoka Zanzibar
watakaohalalisha maamuzi yetu bila kushirikiana na wenzetu, lazima
tuzungumze, theluthi mbili ni takwa la kisheria, hatuwezi kulikwepa,"
alisema.
Kingunge
alisema kwa muda mrefu Zanzibar kulikuwa na mfarakano mkubwa kati ya CCM
na CUF lakini yalifanyika mazungumzo yaliyodumu kwa takriban miaka 13.
"Tumezungumza
kwa muda mrefu tangu 1998 lakini hatimaye tulibuni suala la kugawana
madaraka...katika hali ya Zanzibar tulisema haiwezekani lazima
tukubaliane, sasa Zanzibar imetulia. Ni kutokana na mazungumzo hayo.
"Suala la
Katiba mpya si utani ni lazima tukubali tuzungumze mpaka
tuelewane....humu ndani sisi wajumbe tuzungumze lakini na wakubwa huko
nje nao ni lazima wazungumze," alisema.
UKAWA waliteka Bunge
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Alli Idd, wamewataka wajumbe wa
UKAWA wabatilishe uamuzi wa kususia vikao vya Bunge Maalumu.
Kauli
hizo walizitoa jana walipokuwa wakichangia sura ya kwanza na ya sita za
rasimu ya Katiba, ambapo walisema Katiba inayotungwa ni ya Watanzania
wote, hivyo ni vema UKAWA wakarejea bungeni.
Balozi
Iddi alisema taifa limetumia fedha nyingi kugharimia ujenzi wa Bunge
Maalumu pamoja na kuwagharimia posho wajumbe wake ambapo mpaka jana
lilitumia zaidi ya sh bilioni 20, hivyo si busara kwa UKAWA kususia
vikao.
Alisema
UKAWA ni sehemu muhimu katika utungaji wa Katiba na wajumbe wake
wametumwa na wananchi ambao wanataka matatizo yao yawekewe utaratibu wa
kushughulikiwa kwenye Katiba.
Alisema
kutokana na umuhimu wa kutunga Katiba, Rais Jakaya Kikwete, amekubali
kuliongezea muda wa siku 60 zaidi Bunge hilo ambalo jana limeahirishwa
hadi Agosti 5, mwaka huu.
Alisema
kuongezewa siku huko kumetokana na kutokamilisha kazi yake kwa siku 70
zilizopangwa awali ambazo zimemalizika jana hivyo UKAWA wanapaswa
kutambua unyeti wa vikao vya bunge na umuhimu wao.
"Pamoja
na serikali kutumia fedha nyingi kutengeneza ukumbi na kulipana posho
UKAWA wameamua kususia vikao vya Bunge. Nawasihi warudi tuendelee na
kazi hii tuliyopewa na wananchi. Katiba haitungwi barabarani au kwenye
mikutano ya hadhara bali bungeni.
"Nawasihi
warejee bungeni tuifanye kazi hii tuliyotumwa na wananchi, tumetumia
fedha nyingi na tutaendelea kutumia, kila mmoja wetu analipwa sh 300,000
kwa siku na serikali inatumia sh milioni 188 kwa siku kulipa posho."
Naye
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema anaamini katika umoja, hivyo
kukosekana kwa wajumbe wa UKAWA ndani ya Bunge kumemsikitisha lakini
ataendeleza jitihada za mazungumzo nao.
Pinda
ametoa rai hiyo wakati ni takriban wiki moja imepita tangu alipokaririwa
akitamba kuwa wanawafuata UKAWA huko huko kwa wananchi kwenda kusema
ukweli.
Pinda
aliwasihi wajumbe wa UKAWA warejee bungeni huku akiwasihi wajumbe
wengine wajiepushe na lugha za kejeli na vijembe ambazo alidai
zimechangia mijadala kuwa katika mazingira magumu.
'Mimi
kila siku huwa nasema kuwa yaliyopita si ndwele...tugange yajayo, naomba
wenzetu UKAWA warejee bungeni, Katiba mpya inahitaji ushirikiano wetu
sote," alisema.
Pinda pia
alisema Tume ya Jaji Warioba imefanya kazi nzuri kwa kuwa yapo mambo
mengi ambayo hayamo kwenye Katiba ya sasa lakini yameorodhoshwa kwenye
Rasimu ya Katiba.
Alibainisha
kuwa anapingana na rasimu hiyo katika eneo moja la muundo wa serikali
tatu kwa kuwa anaamini ni mzigo mkubwa kwa taifa na litachangia kuvunja
muungano.
Alisema
kuwa wanaosema kuwa kutofuata mapendekezo ya tume ya Warioba kwa kuwa
imetumia fedha nyingi, wanakosea kwani wajumbe wa Bunge Maalumu wamepewa
fursa ya kuondoa, kuboresha na kuingiza mawazo wanayoona yanafaa kuwemo
kwenye Katiba mpya.
Naye
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alisema kiti chake kiliamua
kuwaacha wajumbe wajadili kwa uhuru zaidi na wananchi waamue kipi
kinafaa.
'Huko
mitaani tunalaumiwa kwa kuwaachia wajumbe, sisi tulifanya hivyo pasipo
kutumia nguvu, kanuni au askari ili wananchi wajue tabia za wajumbe wao
na kuamua, tungebanana sana najua lazima tungepigana na kutoana ngeu,"
alisema:chanzo Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment