Thursday, January 30, 2014

NEC "DAFTARI LA WAPIGA KURA LITABORESHWA"

 
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva.PICHA|MAKTABA 
**********
Pamoja na kushindwa kutaja tarehe rasmi ya kuanza kuboresha daftari la kudumu la wapigakura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesema daftari hilo litaboreshwa kabla ya kuanza kwa upigaji wa kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya. Upigaji wa kura hiyo utafanyika ndani ya siku 70 baada ya kumalizika kwa Bunge Maalumu la Katiba linalotarajiwa kuanza katikati ya mwezi ujao mjini Dodoma. Litafanyika kwa kati ya siku 70 na 90.

Nec imetoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wananchi kwamba tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, daftari hilo halijawahi kuboreshwa, jambo ambalo litasababisha upigaji wa kura kwa ajili ya kupata Katiba Mpya kutawaliwa na vurugu. Malalamiko hayo yanatokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu waliotimiza umri wa kupiga kura lakini hawamo katika daftari hilo.
Pia waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura na wenye kasoro mbalimbali zinazowafanya wapoteze sifa.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva jana alitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa tume hiyo imeshapata fedha kutoka serikalini kwa ajili ya kuendesha mchakato wa kufanya maboresho hayo.

“Tumeanza mchakato wa kuboresha daftari kwa kuanza kuhakiki vituo vya uandikishaji wa kupiga kura vitakavyoongezeka kwa lengo la kuvisogeza karibu zaidi na wananchi,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Inafafanua kwamba mpaka kufikia upigaji wa kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya na uchaguzi mkuu mwaka 2015, daftari hilo litakuwa limeshafanyiwa marekebisho.
“Nec inawataka wananchi kutokuwa na wasiwasi juu ya suala hili. Jukumu la kusimamia na kuendesha mchakato huu ni la tume hii hivyo vyombo vingine visijiingize katika shughuli zisizowahusu” inaeleza.
Katika taarifa hiyo Nec imevitaka vyama vyote 21 vya siasa nchini kuwahamasisha wananchi kushiriki katika kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu ujao, siyo kuwayumbisha wananchi juu ya suala hilo.
MWANANCHI

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...