Thursday, January 30, 2014

MAN UNITED YAKATAA MABILIONI KWA JANUZAJ

JANU eb4eb
HATUTAKI, na tena hatutaki hata kusikia. Na ikiwezekana msirudi tena. Ndivyo ambavyo mapovu yamewatoka mdomoni watu wa Manchester United baada ya PSG kurudi mezani juzi Jumapili na ofa ya kumtaka kinda wao mahiri, Adnan Januzaj.
PSG wamekuwa wakitokwa udenda kwa kinda huyo mwenye asili ya Albania aliyezaliwa Ubelgiji miaka 18 iliyopita na hawajali kama aliingia mkataba mpya wa kuichezea Man United mwishoni mwa msimu uliopita.
Hata hivyo, kocha David Moyes amekataa ofa hiyo ya PSG inayodhaniwa kuanzia Pauni 25 milioni na kuendelea huku wakisisitiza kwamba hawana mpango hata wa kukaa chini na kuzungumza na matajiri hao wa mafuta kutoka Paris.
Man United imempatia mkataba mrefu wa miaka mitano Januzaj Oktoba mwaka jana baada ya kugundulika kuwa huenda mchezaji huyo angekuwa huru na kuondoka Mei mwaka huu mara baada ya msimu kumalizika.

Kabla na baada ya kusaini mkataba huo, Januzaj ameibuka kuwa miongoni mwa wachezaji wachache mahiri katika kikosi cha Man United ambacho msimu huu kimekuwa kikisuasua ndani ya uwanja.
Kwa mujibu wa gazeti la Guardian la Uingereza, Januzaj angeingiza kiasi kikubwa cha pesa kama angeamua kukubali kwenda PSG, lakini mwenyewe ameamua kubaki Man United licha ya timu hiyo kuwa katika hatari ya kukosa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Katika mkataba wake wa awali nyota huyo alikuwa akiingiza kiasi cha Pauni 1,000 tu kwa wiki kutokana na kuwa kinda mwanafunzi, lakini mkataba wake wa sasa unamwingizia kiasi cha Pauni 30,000 kwa wiki.

Akiwa na PSG angeweza kuingiza kiasi cha zaidi ya Pauni 80,000 kwa wiki, lakini staa huyo ameamua kubaki Man United na kuendelea kujifunza zaidi wakati huu kocha Moyes akimwamini na kumpanga mara nyingi zaidi katika safu ya ushambuliaji.
Wakati huohuo pia, PSG pia imekataliwa katika ofa yao ya Pauni 14 milioni kwa ajili ya kumchukua kiungo mahiri wa Newcastle United, Yohan Cabaye ambaye amekuwa akisakwa kwa muda mrefu na kocha Laurent Blanc.
Newcastle inaamini kuwa staa huyo Mfaransa ana thamani ya Pauni 25 milioni na inadaiwa kuwa hata Man United wameanza kumtolea macho Cabaye. Chanzo: mwanaspoti

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...