Monday, October 14, 2013

HIVI NDIVYO MKASA WA MWANDISHI WA ITV UFOO SARO ULIVYOKUWA

Mwandishi wa habari wa ITV, aliyejeruhiwa kwa risasi jana asubuhi, alilazimika kuvumilia majeraha ili kujiokoa yeye mwenyewe na wadogo zake watatu waliokuwa wakipigwa risasi, baada ya mama yake mzazi, Anastazia Saro (58), kuuawa.



Mauaji hayo ya kusikitisha, yalifanyika katika eneo la Mbezi Kibwerere, nyumbani kwa mama yake Ufoo ambako alikuwa akiishi na wadogo zake Ufoo ambao ni Goodluck, Innocent na Jonas.

Mtuhumiwa wa unyama huo ametajwa kuwa ni Anthery Mushi, ambaye ni baba mtoto wa Ufoo, na siku ya tukio wawili hao walitokea Mbezi Magari Saba nyumbani kwa Ufoo, kwenda kuzungumza kifamilia na mama mzazi wa mwandishi huyo.
Mushi (40) ni Mhandisi wa kitengo cha Mawasiliano katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Sudan na aliwasili nchini juzi na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Ufoo Mbezi Mgari Saba.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, Ufoo amejeruhiwa katika paja na tumboni, mama yake mzazi alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi ya kifuani na mtuhumiwa Mushi ambaye naye alijiua baada ya kujipiga risasi kichwani katika eneo la kidevuni.

 Walivyowasili nyumbani
Akizungumza na wavuti hii jana mdogo wake Ufoo, Goodluck alisema; "Walikuja wakiwa pamoja (Ufoo na Mushi) mapema alfajiri wakiwa ndani ya gari saa 12 kabla ya kuingia ndani walitusalimia kisha wakaingia sebuleni na kuanza mazungumzo na mama."
Goodluck alidai baada ya muda, walisikia milio ya risasi iliyokuwa ikiambatana na sauti ya mama yao akisema "jamani nakufaa," na walipotaka kufungua mlango ili kujua kulikoni, mlio wa risasi uliendelea kusikika kutoka sebuleni. "Pengine muda huo Ufoo ndiyo alikuwa akifyatuliwa risasi," alisimulia.

"Tulipotoka kujua kulikoni, tulimuona dada (Ufoo) akijiburiza chini kuja katika mlango wa chumba tulichokuwa tumelala... akatuambia jifungieni atatuua wote huyu."
"Tulifunga mlango lakini zilipigwa risasi mbili mlangoni huku Mushi akisema tokeni nje niwamalize. Tulitafuta namna ya kujiokoa na kuamua kupanda juu ya dari la nyumba," alisimulia Goodluck.
Kwa mujibu wa madai ya Goodluck, walipanda darini ili kujiokoa kwa kuwa Mushi alifungua ntungi wa gesi na kusababisha hewa kuwa nzito na nahisi alilenga kulipua nyumba ili kuteketeza wote.

"Tulipoanza kupanda juu, alianza kufyatua risasi kupitia dirishani lakini wakati huu alikuwa nje ya nyumba, tunamshukuru Mungu kwani muda huo wote tayari tulikuwa juu kwenye dari tukijaribu kutoka nje ya nyumba na tulipofanikiwa kutoka,tulikmbilia kwa majirani kutoa taarifa," alisema Goodluck.
Hata hivyo alisema majirani walikuja lakini hakuna hata mmoja aliyejaribu kusogelea nyumba hiyo.

Ufoo yuko wapi?
 Goodluck alisema wakiongozana na askari polisi, waliingia ndani na kumkuta muuaji akiwa amekaa katika moja ya sofa akiwa tayari amekwisha kufa huku mwili wa mama yao ukiwa sakafuni.
Alisema walijaribu kuangalia ndani kumtafuta dada yao bila mafanikio, ndipo walipotoka nje na kukutana na mmoja waendesha pikipiki aliyewaeleza kuwa walimuona dada mmoja akiwa ametapakaa damu akiomba kupelekwa Hospitali ya Tumbi.
Alijiandaa
"Polisi waliingia ndani na kuchukua bastola iliyotumika kwa mauaji pamoja na kuokota maganda ya risasi na wapopekua mfuko aliokuja nao Mushi, ndani yake  walikuta kuna pingu,shoka lenye mpini mfupi pamoja na kamba. Hata hivyo hatukujua alivibeba vitu hivyo kwa sababu gani,"alisema Goodluck.
Alisema baadaye Polisi waliichukua miili ya marehemu wote wawili na kuondoka nayo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Muhimbili
 Ufoo alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana akitokea Tumbi Kibaha, na alifanyiwa upasuaji na juhudi nyingine zilikuwa zikiendelea kuokoa maisha yake.
Hapo jana Mwenyekiti Mtendaji wa IPP , Reginald Mengi aliruhusiwa kumuona Ufoo ambapo alisema anazungumza na hali yake ilikuwa ikiimarika.
Taarifa zilizopatika leo hii kutoka Muhimbili zinaeleza kuwa Ufoo anaendelea vizuri baada ya jitihada za kuondoa risasi mwilini mwake kufanikiwa na hali yake leo inaendelea vyema.
Aidha askari polisi wamegawanyika katika timu tatu, moja Muhimbili, ya pili Kibamba na tatu mtaani kutafuta taarifa muhimu za mauaji.

Imeandikwa na Margreth Itala.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...