Tuesday, September 17, 2013

SERIKALI YAPINGA KESI YA WAZIRI MKUU PINDA


Kesi inayomkabili waziri mkuu Mizengo Pinda na mwanasheria mkuu wa serikali imetajwa mahakamnai kwa mara ya kwanza ambapo wamewasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi ya kikatiba waliyofunguliwa na kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na chama cha wanasheria Tanganyika.


Katika kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013, LHRC na TLS,wanadai kuwa Pinda alivunja katiba kutokana na kauli aliyoitoa bungeni hivi karibuni wakidai kuwa ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
 
Hata hivyo Pinda na mwanasheria mkuu kwa pamoja katika majibu yao ya madai hayo, wamewasilisha pingamizi la awali ambapo pamoja na mambo mengine wamedai kuwa walalamikaji na watu walioorosheshwa katika kesi hiyo hawana mamlaka kisheria kufungua kesi hiyo.
 
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na jaji kiongozi, Fakihi Jundu akisaidiana na jaji Dk Fauz Twaib na jaji Augustine Mwarija ambapo upande wa wadaiwa uliwakilishwa na mawakili wa serikali wakuu watatu, Nickson Mtingwa, Sarah Mlipana na Alesia Mbuya.

Aidha upande wa walalamikaji uliwakilishwa na mawakili wanne kati ya saba waliotajwa awali .Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo, mmoja ya mawakili hao amesema wamepewa siku 14 kujibu pingamizi lililotolewa .


Wakati kesi hiyo ilipotajwa mahamani hapo upande wa madai uliomba siku 21 kuwasilisha majibu ya wadaiwa ambapo hata hivyo wakili wa serikali mkuu, Mtingwa, alipinga ombi hilo katika kipengele cha muda ulioombwa na badala yake akapendekeza wapewe siku 14 tu.


Mahakama katika uamuzi wake uliosomwa na jaji kiongozi Jundu, ilikataa ombi la wadai na kukubaliana na ombi la wadaiwa, na kuwapa wadai siku 14 badala ya siku 21 kama walalamikaji walivyomba ili kuweza kuwasilisha majibu yao. Tembelea http://jambotz8.blogspot.com/ kila siku.


Mahakama hiyo iliamuru wadai wawasilishe mahakamani majibu yao kabla au septemba 30, na kupanga kusikiliza pingamizi la awali la wadaiwa oktoba 18.
Itakumbukwa kuwa pinda alitoa kauli hiyo inayolalamikiwa, katika mkutano wa 11 wa bunge wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu bungeni, juni 20,2013.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...