Bismillar Rahmanir Rahiim
JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAM (T)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA KUCHUKULIWA NA POLISI SHEIKH PONDA ISSA PONDA TOKA HOSPITALI
Jana asubuhi majira ya saa nne na nusu askari wa jeshi la Polisi na watu wanaoaminika kuwa usalama wa taifa walikwenda hospitali ya Muhimbili (MOI) na kumchukua Sheikh Ponda Issa Ponda. Juhudi za Sheikh Mwenyewe, mkewe na waislam waliokuwepo pale hospitali kutaka abaki hospitalini kuendelea na matibabu hazikuzaa matunda. Mpaka Sasa bado tunafuatilia kujua mahali Kiongozi huyo wa Kiislam alikopelekwa.
Tumepokea kwa masikitiko makubwa sana habari hizi na tunashindwa kuamini kama mambo haya yanaweza kufanywa na Serikali inayodai kutawala kwa kufuata utawala bora unaojali sheria, uadilifu, utu na uhuru wa kujieleza.
Kitendo cha kumpiga risasi Sheikh Ponda na kisha kumchukua toka hospitalini na kumpeleka Gerezani kwa kukiuka taratibu ni kinyume cha haki za binadamu, utawala bora na uhuru wa maisha ya mtu. Matibabu ni haki mojawapo kwa binadamu yoyote hata kama kuna wanaomtuhumu. Tuhuma juu ya mtu si sababu ya kukiuka taratibu, kuvunja sheria na hata kumtisha unayemtuhumu kwani njia hiyo haiwezi kutatua tatizo bali inalifanya kuwa kubwa zaidi.
Jumuiya na Taasisi za Kiislam tunalaani kwa mara nyingine kitendo cha Polisi na Usalama wa Taifa kutenda vitendo vinavyoashiria uonevu kwa viongozi wa dini ya Kiislam na tunaitaka Serikali kutenda uadilifu kwa raia wake hata pale inapokuwa inaamini kuwa raia hao wanamakosa.
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zinapinga kwa kauli moja tume iliyoundwa na jeshi la polisi kuchunguza unyama aliofanyiwa Sheikh Ponda na waislamu hawatatoa ushirikiano kwa tume hiyo ya jeshi la polisi.
Jumuiya na Taasisi za Kiislam zinaitaka serikali kuunda tume huru itakayohusisha viongozi wa kiislamu wanaoaminika kwa ummah kuchunguza tukio la kupigwa risasi Sheikh Ponda Issa Ponda ili kujenga mustakbali mzuri wa amani ya Taifa letu.
Jumuiya na Taasisi za Kiislam hapa nchini zinaamini kuwa ufumbuzi wa suala la amani ya kweli na ya kudumu ya nchi yetu, upo katika kushughulikia madai ya msingi ya waislam dhidi ya Serikali ambayo ndio chanzo cha kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda kwa kuyasema waziwazi, na si kwa kuwatesa, kuwadhalilisha na kuwaauwa Viongozi wa kiislam.
Kutokana na tukio hili Jumuiya na Taasisi za Kiislam zimeitisha mkutano wa dharura utaofanyika katika viwanja vya Nurul yakin siku ya Jumapili saa 9 alasili kutafakari kwa pamoja na hatimae kuchukua hatua za msingi zitazoleta tija ya kweli ili Viongozi wa Kiislam wasiendelee kudhalilishwa.
SHEIKH JUMA SAID ALLY
MWENYEKIT JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAM
16/08/2013