John Tendwa alipaswa kuwa
ameondoka kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, tangu mwaka 2008,
alipofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Aliendelea kufanya kazi
zake hata baada ya muda wa mkataba wake
alioongezewa kuwa umefikia mwisho, hivyo alikuwa anakalia ofisi hiyo ya umma,
kinyume cha sheria.Ametumia muda huo wa miezi kadhaa, aliokuwa
anakalia ofisi ya umma kinyume cha sheria, kuropoka na kuharibu demokrasia, kwa
manufaa ya mamlaka iliyomteua na CCM. Kutokana na mwenendo (maneno na matendo)
wake mbovu, CHADEMA ilitangaza kutokumpatia ushirikiano wowote, yeye kama
Tendwa. Ikamtangaza kuwa adui wa demokrasia nchini.
Kwa muda wote huo, CHADEMA ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Badala ya kuifuta CHADEMA na kufanikisha dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye.
Kuondoka kwa Tendwa hakuzuii kutekelezwa kwa mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, iliyomkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa, hivyo akasababisha kutokea kwa mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Nyololo, Iringa.
Kwa muda wote huo, CHADEMA ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Badala ya kuifuta CHADEMA na kufanikisha dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye.
Kuondoka kwa Tendwa hakuzuii kutekelezwa kwa mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, iliyomkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa, hivyo akasababisha kutokea kwa mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Nyololo, Iringa.
Hivyo CHADEMA, kupitia Kurugenzi ya Habari na Uenezi, inataka kauli ya Rais Jakaya Kikwete juu ya utekelezaji wa mapendekezo hayo kwa Tendwa watu wengine, akiwemo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na wote waliotajwa katika ripoti hiyo ya chombo cha serikali, kuwa walivunja sheria za nchi na kusababisha mauaji ya mwandishi, raia asiyekuwa na hatia.
Tunamkaribisha 'with benefit of doubt', msajili mpya, Jaji Francis Mutungi, kwenye kazi na majukumu yake mapya. Wapenda demokrasia na maendeleo nchini, wanamtarajia atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia haki, sheria na utawala bora, asije akapita njia ya Tendwa.
Kupitia mchakato wa Katiba Mpya unaojadiliwa sasa hivi, CHADEMA tunapendekeza Ofisi ya Msajili ipewe uhuru zaidi na uteuzi wake, usiwe suala la Rais kuamka tu na kuamua kuteua bila wahusika kuomba, kuchujwa na kuthibitishwa na mamlaka nyingine tofauti na iliyoteua.
Tunatambua kuwa msajili mpya aliwahi kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani, kwa muda mfupi, kisha akateuliwa kuwa Jaji na akateuliwa pia nafasi zingine. Na sasa mwaka mmoja baada ya kutumikia nafasi hizo, ameteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Jaji Mutungi, anapaswa kuonesha kwa maneno na vitendo kwamba hatakuwa kama Tendwa, kwa kuanza kushughulikia matendo ya kiharamia yaliyofanywa na Green Guards wa CCM kwenye chaguzi za madiwani, zilizomalizika karibuni, ambazo si tu yalikuwa kinyume na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambayo Jeshi la Polisi wanatakiwa kuchukua hatua, bali pia yalikuwa kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa. Hivyo yako kwenye mamlaka yake.
Jaji Mutungi, amshauri Rais Jakaya Kikwete kushughulikia mapendekezo ya Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, juu ya uvunjifu wa sheria wa wazi uliofanywa na askari polisi na John Tendwa, hivyo kusababisha mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012, huko Nyololo, Iringa.
Aidha, Jaji Mutungi anapaswa kumshauri Rais Kikwete kujibu na kufanyia kazi barua mbili alizoandikiwa na CHADEMA juu ya kuunda Tume Huru ya Kimahakama/Kijaji, kuchunguza mauaji yaliyofanyika kwenye shughuli halali za kisiasa za CHADEMA.
Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mauaji mfululizo mkoani Morogoro na Iringa, CHADEMA ilimwandikia barua Rais Kikwete kumtaka aunde Tume ya Kimahakama kuchunguza utata wa vifo hivyo na vingine kadhaa vilivyotokea kwenye shughuli halali za kisiasa, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ili ukweli ujulikane, haki itendeke na wahusika wachukuliwe hatua, hadi sasa rais hajafanya hivyo.
Itakumbukwa pia kuwa baada ya mlipuko wa bomu la Arusha, kwenye mkutano wa kampeni, CHADEMA pia ilimtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake kuunda Tume Huru ya Kimahakama, ili ushahidi juu ya tukio hilo uwasilishwe, hadi sasa pia rais yuko kimya. Hivyo kwa nafasi yake, msajili mpya atoe ushauri kwa rais kuchukua hatua hizo, ili vyama vitimize wajibu wa kikatiba kufanya kazi zake kwa haki, uhuru na sheria za nchi zinazosimamia shughuli za vyama vya siasa nchini.
Imetolewa leo, Jumatatu, 5 Agosti, 2013 na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari, CHADEMA