Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa sana na tukio la kushambuliwa na kuuawa kwa
vijana saba hodari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania waliokuwa wanalinda amani
katika eneo la Darfur, Sudan.
Kwa hakika, Rais amesikitishwa sana
na kitendo hicho ambako wanajeshi wengine 14 wa Tanzania wamejeruhiwa na waasi
wa Sudan na ametuma salamu za rambirambi za moyoni mwake kwa Jeshi la Wananchi
wa Tanzania na kwa familia za wafiwa wote.
Aidha, Rais Kikwete anaungana na
Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na familia za wafiwa
kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa Tanzania. Rais pia anaungana na
Watanzania wote kuwaombea wale walioumia katika tukio hilo waweze kupona haraka
na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Katika salamu zake za rambirambi kwa
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis
Adolf Mwamunynge na familia za
wafiwa, Rais Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu amesema:
“Sina maneno ya kutosha ya kuelezea
mshtuko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo vya vijana wetu hao
ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa
majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia
ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na
waassi.”
Rais Kikwete ameongeza kumwambia
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na familia za wafiwa ”Napenda kwa niaba ya Watanzania
wenzangu niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea
walipokwenda Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania
ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri
sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi
yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi yao.”
Amesisitiza Mheshimiwa Rais Kikwete:
“Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo
wangu kuomboleza vijana wetu hawa. Kupitia kwao, natuma salamu za rambirambi
kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na wapigaji wote wa Jeshi letu kwa
kupotelewa na wenzao. “
“Aidha, kupitia kwako, nawatuma
salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na wapenzi wao na ndugu zao
katika tukio hilo. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza. Wajue kuwa
uchungu wao ni uchungu wangu pia na wa Watanzania wote na kuwa kwa pamoja
tunamwomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki
kigumu. Vile vile kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze peponi roho za
marehemu. Amina.’
Kwa walioumia, Rais Kikwete
amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Naungana pia na Watanzania wenzangu katika
kuwapa pole nyingi walioumia katika tukio hilo tukiwaombea kwa Mwenyezi Mungu
wapone haraka na kuendelea na shughuli zao za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa
Mataifa.”
Vijana hao waliopoteza maisha yao na
walioumia, walikuwa sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa
wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi katika Darfur kutoka eneo la
Khorabeche kwenda Nyara waliposhambuliwa na waasi kiasi cha kilomita 20 kutoka
Khorabeche saa tatu asubuhi jana, Jumamosi, Julai 13, 2013.
No comments:
Post a Comment