HOFU YAKIMBIZA
WAPIGA KURA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibuka na ushindi mnono katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata nne za jijini Arusha.
Katika Kata ya Elerai, mgombea wa CHADEMA
Injinia Jeremia Mpinga alimbwaga Emanueli Laizer wa CCM kwa kura 1,715, dhidi ya
1,239.
Kata hiyo ilikuwa na wapiga kura 23,797
waliojiandikisha na vituo 55 vya kupigia kura, lakini idadi kubwa ya wananchi
hawakujitokeza.
Matokeo ya kura yalitangazwa chini ya ulinzi
mkali wa askari polisi zaidi ya 40 wenye silaha, na kupokelewa kwa shangwe kubwa
na wafuasi na mashabiki wa CHADEMA.
Katika Kata ya Kaloleni, mgombea wa CHADEMA,
Kessy Emmanuel Miliare alimshinda kwa mbali mgombea wa CCM kwa kura 1,470 dhidi
ya 530, wakati mgombea wa CUF ameambulia kura 275. waliojiandikisha 12,674
waliopiga kura 2,292. Kura halali ni 2,277 na zilizoharibika 15.
Akitangaza matokeo katika Kata ya Themi,
Msimamizi wa Uchaguzi, Editha Mboye alimtangaza mgombea udiwani wa CHADEMA,
Mallance Kinabo kuwa mshindi kwa kupata kura 678, akimwacha mbali mgombea wa CCM
Victor Mkolwe aliyepata kura 326, huku yule wa CUF, Lebora Ndervai akipata kura
313.
Kata ya Kimandolu, CHADEMA pia wameibuka na
ushindi mkubwa na kuiacha vibaya CCM.
Mgombea wa CHADEMA, Elishadai Ngowi amemshinda
mgombea wa CCM, Edina Sauli kwa kura 2,265, dhidi ya 1,169 za mpinzani
wake.
KATA YA THEMI: CHADEMA 678; CCM 326; CUF 313
KATA YA KIMANDOLU: CHADEMA 2,665; CCM 1,169
KATA YA KALOLENI: CHADEMA 1,019; CCM 389; CUF 169
KATA YA ELERAI: CHADEMA 1,715; CCM 1,239; CUF 213
KATA YA KIMANDOLU: CHADEMA 2,665; CCM 1,169
KATA YA KALOLENI: CHADEMA 1,019; CCM 389; CUF 169
KATA YA ELERAI: CHADEMA 1,715; CCM 1,239; CUF 213
Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Jiji
la Arusha lilizizima kwa shangwe na nderemo, huku idadi kubwa ya watu
wakijipongeza kwa ushindi huo mkubwa.
Mwigulu Nchemba atimua
Matokeo hayo ambayo yameonekana kuwasononesha
viongozi na wanachama wa CCM, yalimfanya Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu
Nchemba, kuondoka kimya kimya jijini hapa kwa kutumia gari maalumu.
Mwigulu ambaye aliongoza kikosi cha CCM katika
kampeni za kimya kimya, majira ya jioni alionekana akielekea Moshi, huku
wasaidizi wake wakiwemo wabunge wakitoweka katika vituo vya kuhesabia
kura.
Mapema, wabunge wa CHADEMA na wa CCM tangu
asubuhi walikuwa wakizunguka katika kata hizo, huku Mbunge wa Viti Maalumu,
Catherin Mgige (CCM) akitumia gari ndogo, Salon yenye vioo vya giza alionekana
akizunguka kata zote jana.
Ulinzi mkali wa polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatusi
Sabas jana aliongoza kazi ya ulinzi uliokuwa na idadi kubwa ya askari polisi
wenye silaha za moto na mabomu ya machozi.
Akitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye
namba TP 1715, Kamanda Sabas alionekana akizunguka katika mitaa ya kata zote
nne, zilizokuwa zimesheheni idadi kubwa ya askari, wengi kutoka mkoani
Kilimanjaro.
Waangalizi wa kimataifa
Katika tukio la kwanza la kihistoria, uchaguzi
wa kata hizo ulishuhudiwa na waangalizi wa kimataifa kutoka taasisi ya
International Low and Policy Institute yenye makao makuu yake nchini Norway, na
wale wa ndani kutoka Jukwaa la Katiba.
Kiongozi wa waangalizi kutoka Norway, Sterling
Roop, akiongea na Tanzania Daima alisema kuwa idadi ndogo ya wapiga kura
imejitokeza na uwepo wa dosari kadhaa umewafanya baadhi ya wananchi kukosa haki
yao ya kupiga kura.
Roop alisema pamoja na wananchi kuwa na shahada
halali za kupigia kura na majina yao kuwepo, lakini hakukuwa na picha zao katika
daftari la wapiga kura na hivyo wakazuiwa kupiga kura.
Katika vituo vingi, hususani Kata ya Kaloleni
dosari kuu ilikuwa ni kukosekana kwa majina katika daftari la kupiga kura kwa
wananchi ambao wana shahada na pia majina yao kubandikwa katika ofisi za kata
kama wapiga kura halali.
Majina ya wapiga kura yatoweka
Dosari kubwa iliwakumba wapiga kura baada ya
majina, picha na maelezo kukosekana kwenye daftari la wapiga kura karibu katika
kata zote.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Hamid M Hamid alikiri tatizo hilo na kudai kwamba tayari alishawasiliana na
wataalamu wake wa mifumo ya kompyuta (IT) ili washughulikie kasoro hizo kwenye
kila kata iliyokuwa ikiendelea na uchaguzi.
Hata hivyo, alisema kuwa yeye si mchawi kuweza
kubaini chanzo cha hitilafu hizo zilizojitokeza. Baadhi ya upungufu uliobainika
ni baadhi ya watu kuandikishwa zaidi ya mara moja.
Kata ya Kaloleni kwenye kituo cha AICC Nursery
B, mpiga kura Michael Laurence alikuwa ameandikishwa mara tatu kwenye daftari la
wapiga kura akiwa na namba 48674955, 444666858 na 13142914.
Hata hivyo kwenye majira ya saa saba mchana,
wataalamu wa kompyuta wa Tume ya Uchaguzi walifika na kuanza kuwasaidia wananchi
waliokuwa wamejazana kwenye kituo cha kata hiyo.
Mmoja wa wataalamu hao, Siif Mtezo aliwaeleza
waandishi wa habari kuwa tatizo hilo lilisababishwa na watu kujiandikisha zaidi
ya mara moja.
Alisema kilichowafanya wengi washindwe kuona
majina yao ni hofu kama ile inayowakumba wanafunzi wanaoenda kuangalia matokeo,
na kwamba tume ililazimika kuwapigia simu wananchi wengi waliokuwa wameondoka,
na wakarudi kupiga kura.
Wakala wa Chama cha Wananchi (CUF), Malik Abbas
kwenye kituo hicho aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wananchi wengi walifika,
lakini majina yao hayakuonekana na wakaondoka, huku akionyesha baadhi ya picha
ambazo hazionekani vizuri kutokana na kufifia kwenye daftari hilo.
Mgombea udiwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CUF,
Abbas Darwesh alisema wananchi wengi walishindwa kupiga kura akiwemo mtoto wake
Omary Othman ambaye pamoja na kuwa na kitambulisho chake namba 32479962 jina
lake halikuonekana kwenye orodha.
“Inawezekana kweli kuna mchezo mchafu
umefanyika kubadili daftari la wapiga kura kama ambavyo tetesi zilikuwa
zimezagaa, kwa sababu mtoto wangu mwenyewe alipiga kura kwenye kituo hiki katika
uchaguzi wa 2010, lakini leo naambiwa jina lake halipo,” alilalamika
Darwesh.
Msimamizi wa uchaguzi Kata ya Kaloleni, Anna
Lebisa amekiri kukosekana kwa majina ya wananchi katika daftari licha ya kuwepo
katika mbao za matangazo na kusema hawakuruhusiwa kupiga kura.
Miongoni mwa waliokumbwa na kadhia hiyo ni
Omari Othmani na mtangazaji wa TBC, Khalifa Mshana ambaye alilazimika
kulifikisha suala lao kwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji
mstaafu Hamid Mahmood ambaye alimuachia ofisa wa tume kulishughulikia.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba
akiwa na timu yake ya waangalizi wa uchaguzi huo, alisema kura zimeanza kupigwa
taratibu na idadi ndogo ya watu kujitokeza akidai kumechangiwa na hofu kubwa
baada ya kuwepo kwa askari wengi katika vituo vya kupigia kura.
“Wingi wa askari wenye silaha za moto katika
vituo vya kupigia kura umechangia kufanya baadhi ya wananchi kutojitokeza kwa
hofu ya askari hao,’’ alisema Kibamba.
Wafuasi wa CHADEMA watekwa, wapigwa
Matukio ya kutekwa na kupigwa kwa wafuasi wa
CHADEMA yalijiri katika uchaguzi huo jana.
Vijana wanaoaminika kuwa ni wa CCM, wakiwa
ndani ya gari aina ya Land Cruiser iliyoegeshwa kwenye uwanja wa AICC wa Soweto
waliwakamata na kuwapiga baadhi ya wananchi waliokuwa wakielekea katika vituo
vya kupigia kura eneo la Soweto.
Msimamizi wa uchaguzi wa Kata ya Kaloleni,
Lebisa alikiri kuliona gari hilo majira ya saa tatu asubuhi. Aliwaelekeza polisi
waliokuwa kwenye kituo hicho kuwafuatilia, lakini waliondoka kabla
hawajakamatwa.
Aidha, mwananchi mwingine, Hassan Noor ambaye
alikuwa wakala wa CHADEMA kwenye kituo cha AICC Nursery alishindwa kufanya kazi
hiyo baada ya kunyang’anywa barua yake na vijana waliokuwa kwenye gari aina ya
Land Cruiser ya rangi ya maziwa ambayo namba zake hakuzishika.
Akiongozana na wenzake wawili kwenye mzunguko
karibu na kituo hicho cha kupigia kura, Noor aliona gari hilo likisimama karibu
yao na kuwataka waondoke eneo hilo. Aliwaeleza kuwa ni mawakala, ndipo
walipomtaka awaonyeshe barua.
“Nilijua ni askari, na nilipowapa
wakaninyang’anya na kuichana. Kisha wakampiga mwenzangu Boniface Kimaro.
Alipigwa na kitu kama chuma kichwani na wakaondoka. Tumeripoti Kituo cha Kati
cha Polisi,” alisema.
Katika Kata ya Kimandolu, watu sita walikamatwa
wakiwa wamekaa katika gari moja na kupelekwa polisi kwa mahojiano, hali hiyo
ikajitokeza tena katika Kata ya Kaloleni pia, ambako watu wasiojulikana
walikamatwa wakiwa wamejificha ndani ya gari.
Chanzo: Tanzania
Daima
No comments:
Post a Comment