MAAFISA watatu wa polisi wa utawala (AP)
walijeruhiwa kwenye mapigano yaliyozuka kati yao na wenzao wa Uganda
kwenye kisiwa kinachozozaniwa cha Migingo.
Mzozo huo wa
mwishoni mwa wiki ulianza pale maafisa wa Uganda waliokuwa na sare rasmi
walipoenda katika ufuo wa karibu wa Nyandiwa kurekebisha mashua yao.
Lakini wakazi wa
Nyandiwa waliwazuia kutia nanga wakisema kwa vile walikuwa na sare na
bunduki, walihofia wangeliwahangaisha kwa kuwapokonya samaki wao.
Mmoja wa
wavuvi wa eneo hilo Bw Oloo Okello, alisema maafisa hao wa Uganda
walirejea Migindo wakuwa na hasira bila ya kurekebisha boti lao.
“Waliporejea walisema
kwamba polisi wa Utawala wa Kenya wa kitengo cha kushika doria mpakani,
Rural Border Patrol Unit (RBPU), walio kisiwani Ugingo hawatakiwi kutia
guu Migingo.
Lakini maafisa hao watatu wa polisi wa Kenya walipuuza tangazo hilo na kwenda kisiwani Migindo kununua bidhaa.
Ni wakati huo
walipoanza kutandikwa na maafisa hao wa Uganda, huku maafisa wa usalama
wa Kenya, wakiwemo polisi wa kawaida wakitazama kwa mbali bila kufanya
lolote.
Maafisa hao
wa polisi wa Kenya hawakuwa na silaha wakati huo na inasemekana
walipigwa kutokana na agizo kutoka Kampala, ingawa Taifa Leo haikuweza
kuthibitisha madai hayo.
Ripoti
nyingine zinasema kwamba maafisa hao wa Uganda walikuwa wakienda eneo la
Nyandiwa na wakazuiwa na polisi hao wa Utawala. Inadaiwa kuwa polisi wa
Utawala wa Kenya walikuwa wamesisitiza kuwa, kama maafisa hao wa
usalama wa Uganda walikuwa na lasima ya kuingia kwenye eneo la Kenya,
basi hawakuwa na budi kuacha silaha zao.
Onyo
Jambo hilo liliwaudhi maafisa hao wa Uganda ambao inasemekana waliwaonya Wakenya nao wasithubutu kuweka guu Migingo.
Naibu
Kamishna wa Kaunti wa eneo la Nyatike, Bw Moses Ivuto, alisema ingawa
tukio hilo ni la kusikitisha, suala hilo tayari limeanza kushughulikiwa
na wakuu wa serikali zote mbili.
Alisema inawezekana kuwa mkuu wa polisi wa Uganda katika kisiwa cha Migingo huenda hakuwa na habari kuhusu tukio hilo.
“Inawezekana
mkuu wa polisi wa Uganda aliye Migingo hakuelewa kuwa maafisa wake
waliingia eneo la Kenya wakiwa na silaha. Kawaida huwa polisi wa upande
mmoja hawaruhusiwi kwenda eneo jingine akiwa na silaha,” akasema.
Kaimu kamanda
wa polisi hao wa Utawala katika eneo hilo Bw Peter Gikonyo, alisema
wanafanya juhudi kuhakikisha maafisa wa usalama wa nchi hizo jirani
kwenye kisiwa cha Migingo wanafanya kazi kwa ushirikiano.
No comments:
Post a Comment