Wakati
Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu
aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Arusha,Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe
amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao watawasili
Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama kwenye
msiba huo.
Alisisitiza
kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya
kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa
majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.
Wakati
Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi
akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari, alisema taarifa za
awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa mkono (grumeti) na
hivi sasa timu ya wataalamu ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni
Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na uchunguzi wa
tukio hilo.
Naye
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP),
Said Mwema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameahidi kupambana
na kuhakikisha wahusika wanapatikana.
Alitoa
taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es Salaam na kusema hadi
jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni wawili na 68 ni
majeruhi.
Waliokufa
ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa Chadema, Kata ya Sokoni 1,
Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin.
"Mpaka
hivi sasa watu waliokufa ni wawili na wengine 68 wamejeruhiwa na
mlipuko huo, lakini naahidi kuwa tutapambana na kuhakikisha tunawapata
wahusika," alisema Mwema.
Sanjari
na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa bomu, Mwema alisema timu ya
jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda Arusha kuongeza nguvu
katika upelelezi.
Hata
hivyo, hakufafanua zaidi juu ya mtuhumiwa huyo kutokana na kile
alichosema taarifa husika zinafanyiwa uchunguzi kabla ya kuwakamata
watu sahihi waliohusika na tukio hilo.
Kwa
mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao Makuu inayoongozwa na
makamishna wawili, imeondoka kwenda mkoani Arusha kuongeza nguvu katika
operesheni na upelelezi.
Timu
hiyo inaongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na
Isaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai,
wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.
Alisema
polisi inafanya operesheni kali nchini kote kuhakikisha inawatia
mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda uhalifu huo.
"Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea," alisema.
IGP
ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za wahalifu hao, atoe taarifa
kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo
chochote cha polisi ili wakamatwe.
‘Kwa
nini iwe Arusha’ hii ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mulongo
aliyoitoa baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali za Mount Meru,
St Elizabeth pamoja na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre
jijini.
“Nawapa
pole sana ndugu zangu wa Chadema, na wana Arusha kwa ujumla pamoja na
watanzania. Lakini najiuliza kwa nini Arusha …tukio hili limenihuzunisha
sana na nawaomba tusiingize masuala ya kisiasa, tuache polisi
wachunguze tukio hili kwani timu ya wataalamu kutoka Jeshi la Ulinzi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na wataalamu wengine wanachunguza tukio
hili na wahusika watachukuliwa hatua.’’
Mulongo
ambaye tukio hilo la juzi limekuja ikiwa ni mwezi mmoja tangu kutokea
kwa mlipuko katika Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi la Olasiti,
alisema jana anayefanya ulipuaji wa mabomu na kumwaga damu za watu
mbalimbali na wengine kufa, ipo siku Mungu atamhukumu.
Kati
ya majeruhi 59 waliolazwa kwenye hospitali hizo, wawili wamehamishiwa
Hospitali ya KCMC kutoka Hospitali ya AICC kwa matibabu. Wagonjwa
wengi wamelazwa hospitali ya Selian ambao ni 40. Hata hivyo, wanane
waliruhusiwa baada ya matibabu.
Mkuu
wa Mkoa alisema anajisikia mnyonge kutokana na matukio hayo mawili
tofauti; mlipuko wa kanisani na la juzi wakati Chadema ilipokuwa
ikihitimisha kampeni zake za udiwani kwenye kata nne za Themi, Kaloleni,
Elerai na Kimandolu ambao hata hivyo uliahirishwa kutokana na tukio
hilo.
Mulongo
alitaka wananchi wasihusishe na masuala ya kisiasa badala yake
wawaachie polisi kuchunguza tukio hilo. Kwa mujibu wa Mulongo, watu
kadhaa wamekamatwa.
Katika
kipindi kisichozidi miezi miwili, mji wa Arusha umeshuhudia majeruhi
wasiopungua 130, na vifo vya watu watano vilivyotokana na kurushwa
mabomu na watu wasiojulikana katika mikusanyiko kanisani na kwenye
mkutano huo wa siasa wa Chadema.
Katika
tukio la mwezi uliopita katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi, watu watatu walifariki na wengine wapatao 59 kujeruhiwa.
Mmoja
wa watuhumiwa ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda,
Victor Ambrose alifikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika katika
shambulio hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari, daktari wa hospitali ya Selian, Paul Kisanga
alisema walipokea wagonjwa 48 kabla ya wanane kuruhusiwa.
Alisema
miongoni mwa wagonjwa hao, wamo watoto watano wanne wakiwa wa kiume na
mmoja wa kike. Mtoto Fahad Jamal (7) amelazwa kwenye wadi ya wagonjwa
mahututi chini ya uangalizi wa madaktari.
Hospitali
ya St Elizabeth wapo wagonjwa wanane na Mount Meru imepokea wagonjwa
tisa. Mganga Mkuu wa Mkoa wa hospitali ya Mount Meru, Frida Mokiti
alisema wamepokea miili ya marehemu wawili ambao ni Judith Moshi (25)
ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) kata ya Sokoni 1,
Jijini Arusha pamoja na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin
(13).
Kwa
mujibu wa majeruhi wa tukio hilo, Abraham Samuel waliona kitu kikiwa
kwenye mfuko wa rambo kikirushwa juu na baada ya muda mfupi walisikia
vilio na wengine kuzimia.
Kitu
hicho kilirushwa kabla ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Taifa,
Freeman Mbowe kuhitimisha kampeni za uchaguzi za udiwani wa kata nne za
Jimbo la Arusha Mjini.
Mlipuko
huo unadaiwa kuwa ulitokea jirani na gari la matangazo la Chadema, aina
ya Mitsubishi Fuso lililokuwa karibu na jukwaa alilokuwa akitumia
Mbowe.
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe amedai tukio hilo si la bahati mbaya bali lilipangwa na kundi la watu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, alisema wabunge wa chama hicho leo
hawataingia bungeni bali watawasili jijini Arusha kwa ajili ya kuungana
na wananchi pamoja na wanachama wa kwenye msiba huo.
Kwa
mujibu wa Mbowe, marehemu Judith atapelekwa mkoani Kilimanjaro na
Justin atapelekwa mkoani Tabora kwa ajili ya maziko mara baada ya polisi
kukamilisha uchunguzi juu ya tukio hilo.
Alisisitiza
kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya
kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa
majibu juu ya vifo hivyo marehemu hao watasafirishwa.
‘’Nimetembelea
majeruhi jana hospitalini lakini kwa Hospitali ya Selian, Arusha
Lutheran Medical Centre majeruhi ni wengi lakini walioumia sana ni
watoto kuna mtoto mmoja amekatika mkono na mguu ambaye ni Sharifa
Jumanne na Amiri Ally ana vyuma vitatu mwilini mwake,’’alisema Mbowe.
Ingawa
polisi imesema inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kutoa
taarifa kamili, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kwamba zipo taarifa
kwamba shambulio hilo liliambatana na risasi za moto.
Chama
cha Wananchi (CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim
Lipumba, kimelaani tukio hilo na kutaka Serikali ichukue hatua za haraka
na kukamata waliohusika na matukio hayo iwe fundisho.
“Hatuna
sababu na tusijenge utamaduni wa nchi yetu kugeuka eneo ambalo palipo
na mkusanyiko mabomu yanalipuka, Tanzania ni nchi ya amani, kwa matukio
haya CUF tunalaani kwa nguvu zote na kutoa pole kwa familia
zilizoathirika,” alisema Lipumba.
Lipumba
alisema kitendo kilichofanyika katika mkutano huo wa Chadema ni unyama
wa kutisha wenye makusudi ya kundi fulani kutekeleza azma yao dhidi ya
chama, watu, kundi na viongozi.
Alisisitiza
kuwa utamaduni huo wa kufanya unyama katika mkusanyiko wa watu
unapaswa kudhibitiwa mapema ili kuepusha madhara mengine ndani ya jamii
kwa kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na familia tegemezi.
“Tumefikia
hatua mbaya sana ya kufanya siasa za mabomu huu ni utamaduni unaopaswa
kukemewa na kupingwa, matukio haya yanajirudia kutokana na Serikali
yenyewe kuyakaribisha kwa kushindwa kuwachukulia hatua kali wahusika,
tunaomba dola ifanye ifanyalo katika uchunguzi wake na kuwakamata na
kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment