Wednesday, June 05, 2013

Azam yawatupia virago Babi, Uhuru



Abdi Kassim ‘Babi’

Dar es Salaam. Azam FC imetoa mkono wa kwa heri kwa kiungo wake mkongwe Abdi Kassim ‘Babi’ na Uhuru Seleiman aliyekuwa kwa mkopo. Meneja wa timu hiyo, Patrick Kahemela alisema jana kuwa sababu kubwa ya kuachana na wachezaji hao ni mikataba yao kumalizika pamoja na umri kuwatupa mikono.

Wachezaji waliotupia virago ni pamoja na Lewis Cosmas aliyejiunga na Ruvu Shooting na Abdulhalim Humoud aliyepata timu Afrika Kusini ya Jomo Cosmos. Akizungumza na gazeti hili Abdi Kassim alisema “Ni kweli mkataba wangu kuitumikia Azam umeisha ingawa walinitaka nisaini mpya, lakini tukashindwa kuafikiana. “Naamini bado nina nguvu na uwezo wa kucheza soka. Kwa hiyo niko tayari kujiunga na timu yoyote ambayo itaonyesha nia ya kunitaka.” alisema Babi aliyekipiga na klabu za Mlandege ya Zanzibar, Mtibwa Sugar, Yanga, DT Long ya Vietnam pamoja na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Anaeleza kuwa yuko tayari kujiunga na Yanga, Mtibwa Sugar ama Coastal Union iwapo zitaonyesha kutaka kumsajili kwa ajili ya msimu ujao. Klabu ya Mtibwa iliwahi kukiri kutaka kumrejesha Babi nyumbani katika dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu.
Wachezaji wengine walioachwa na Azam ni kipa Deogratius Munishi, Sunday Frank na Uhuru Seleiman aliyekuwa akiitumikia klabu hiyo kwa mkopo akitokea Simba. “Munishi mkataba wake umekwisha huku Uhuru akirejeshwa Simba, baada ya kumaliza msimu wake wa mkopo na Azam.” alisema Kahemela.

Alieleza kuwa kama ilivyokuwa wakati wa dirisha la uhamisho wa wachezaji msimu ulioisha Azam ilimsajili George Odhiambo ‘Blackberry’ peke yake.

“Safari hii tena tumeamua kuwapandisha wachezaji wawili wa U-20, Mudathir Yahaya na kipa Hamadi Juma na kufunga zoezi la usajili,”

“Kwa mujibu wa ripoti ya kocha Stewart Hall, inaeleza hakuna sababu ya kwenda nje kusajili wachezaji ambao viwango vyao havipishani na waliopo klabuni.” alisema kiongozi huyo.

Aidha alisema wachezaji wengine wote waliosalia wanabaki klabuni hapo ingawa, kocha amependekeza baadhi ya vijana wa U-20 walioonyesha viwango vya juu wapandishwe timu kubwa.

Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...