Daktari
bingwa wa uchunguzi wa magonjwa ya saratani katika Kitengo cha
Patholojia, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Henry Mwakyoma na
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Taasisi ya Saratani ya
Ocean Road, Dk Crispin Kahesa wameeleza hayo jijini Dar es Salaam.
Walisema
kuwa ingawa bado hakuna visababishi kamili vya saratani hiyo, asilimia
90 ya wagonjwa wa saratani ya koo wamekuwa na historia ya uvutaji
sigara, unywaji pombe kali kama viroba na kula aina za vyakula
vilivyochomwa
ikiwamo nyama na samaki, ulaji pilipili, ndimu, ‘chilisosi’ na unywaji wa vitu vya moto kupita kiasi.
Anasema kuwa Saratani ya Koo ni mbaya zaidi ukilinganisha na saratani za aina nyingine.
Anaeleza:
“Saratani ya Koo ni mbaya ukimwona mgonjwa unaweza kulia, hawezi tena
kula na ikibidi huingiziwa mipira maalumu ili kupitisha chakula, lakini
kuna wakati hata mipira huziba, hivyo huishi kwa dripu ya chakula
pekee.”
Naye
Dk Mwakyoma anaeleza kuwa Saratani ya Koo hushambulia seli zinazotanda
koo na kutengeneza uvimbe katikati ya koo ambao huanza kuleta madhara
taratibu.
“Ukiwa
na Saratani ya Koo, itakuchukua muda mrefu sana mpaka kuanza kuona
viashiria mbalimbali, awali mgonjwa huanza kupata shida kumeza chakula.
Wengi hufika hapa wakiwa wamechelewa na tunavyofanya vipimo huwa katika
hatua mbaya sana,” anasema Mwakyoma.
Anazitaja
aina kuu mbili za Saratani ya Koo kuwa ni: “Oesophagus Carcinoma na
Squamous cell carcinoma, ambazo hutofautiana kulingana na jinsi seli
zake zinavyoonekana kwenye darubini.
Hata hivyo, pamoja na tofauti hizo za mwonekano, utambuzi na matibabu ya aina hizi za Saratani ya Koo hufanana.”
Anabainisha
kuwa aina zote mbili huanza kwa kuathiri seli zilizo katika utando wa
ndani wa ukuta wa koo, uitwao ‘mucosa’ kabla ya kusambaa maeneo
mengine.
Kwa
upande wake Dk Kahesa anasema kuwa katika hatua za awali, mgonjwa
mwenye Saratani ya Koo anaweza asionyeshe dalili zozote. Hata hivyo,
kadiri saratani inavyozidi kukua na kuenea, mgonjwa anaweza kuanza kuona
dalili.
“Dalili
ya kwanza ya mgonjwa wa saratani ni chakula kukwama kwenye koo, siku za
mwanzo mgonjwa anaweza kushindwa kumeza chakula kigumu kisha cha
majimaji na baadaye akashindwa kumeza hata mate.
Maumivu
wakati wa kumeza chakula, hasa chakula kigumu, maumivu kwenye kifua au
mgongoni, kupungua uzito, kiungulia na sauti ya mkwaruzo au kikohozi
kikavu cha zaidi ya wiki mbili,” anasema.
Hata
hivyo Dk Mwakyoma anasema kuwa wapo wanaopata Saratani ya Koo kulingana
kwa kurithi kutoka kwa wazazi wao pamoja na umri kuwa mkubwa aliosema
pia huchangia tatizo hilo.
“Wapo
waliopata saratani kufuatana na urithi na hata umri, lakini tatizo hili
pia limeshamiri sana maeneo ya Kilimanjaro, kama tunavyosema mtindo wa
maisha nao unachangia. Watu wa mkoa huo wana utamaduni na kunywa pombe
kali na nyama choma.”
Anautaja
mkoa unaofuatia kwa waathirika wengi wa saratani kuwa ni Dar es Salaam,
ambako alisema wanapatikana watu wenye umri kuanzia miaka 45.
“Hawa
kwa makadirio huwa wameanza kukumbwa na tatizo hili wakiwa kati ya
miaka 30, ambapo kadri siku zinavyosonga ndivyo saratani inavyozidi
kukua, lakini mtu huyu akichelewa kupatiwa matibabu hufa haraka tofauti
na aliyewahi,” anasema Mwakyoma.
Utafiti wa Saratani ya Koo nchini
Taasisi
ya Afya ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mara ya kwanza ilifanya
utafiti wa Saratani ya Koo mwaka 1983 hadi 1992 ambapo ilibaini kuwa
kati wagonjwa 546 waliopimwa kulikuwa na wastani wa wagonjwa 116
wanawake huku 430 wakiwa ni wanaume.
Utafiti
huo ulifanywa na Dk Henry Mwakyoma kwa kushirikiana na Dk N Mbebati, Dk
M Aboud, Dk J Kahamba na Dk C Yongolo uliokamilika Juni 1, 1994,
ulibaini ukuaji wa Saratani ya Koo Kanda ya Kaskazini kwa watu wenye
umri kati ya miaka 50-59.
Dk
Mwakyoma anasema kuwa licha ya utafiti huo kufanyika kwa watu wenye
umri kuanzia miaka 21 hadi 90, wagonjwa wengi walikuwa wenye umri wa
miaka 50-59 hali ambayo ni tofauti na sasa.
“Wakati
tunafanya utafiti huo hapa Muhimbili, ugonjwa huu ulikuwa unawakumba
watu wazima wenye umri kuanzia miaka 50 - 59, hivi sasa vijana wadogo wa
miaka 40 tunawatambua tayari wana Saratani ya Koo, ambayo hata hivyo
bado ni ngumu kutibika tofauti na saratani za aina nyingine,” anasema
Mwakyoma.
Watumiaji wa vilevi
Amos (si jina lake kamili) anasema kuwa anatumia pombe kali aina ya Konyagi, lakini si kila siku.
“Natumia
Konyagi, lakini huitumia kwa lengo la kuongeza nguvu za kiume, nikinywa
huwa nahisi nguvu zinaongezeka,” anasema na kuongeza: “Lakini pombe hii
ni chungu, nikinywa huwa nahisi moto katika koo langu, ikishapita
huhisi ahueni.”
Mwanamume mwingine anayevuta sigara (Hamisi) anasema kuwa hawezi kumaliza saa tatu bila ya kuvuta sigara.
“Najisikia
kukwanguliwa na kero kubwa kooni mwangu, hivyo nalazimika kutumia
sigara kila wakati, nilijaribu kuacha, lakini nikahisi nitakufa,
naendelea mpaka leo na nipo vizuri tu,”alisema.
Amos
alipoulizwa kuhusu ufahamu wake katika ugonjwa wa Saratani ya Koo
alisema: “Mh, unaniogopesha, sijawahi kupata elimu hii ingawa nafahamu
kwamba inaharibu mapafu, ila hii inanitisha. Nikipata tiba nitaacha
kutumia sigara.”
Matibabu ya Saratani ya Koo
Dk Kahesa anasema kuwa uchaguzi wa aina gani ya tiba itumike hutegemea zaidi eneo lililoathiriwa na saratani hiyo.
“Iwapo
saratani imeshambulia viungo vilivyo karibu na koo na kusambaa hadi
kufikia kwenye tezi au viungo vingine vya mwili, yaweza kutibiwa kwa
kufanya upasuaji, kutumia mionzi, kutumia kemikali maalumu, au yote
matatu.”
Kwa
upande wa upasuaji anasema kuwa upo wa aina tofauti ukitegemea sehemu
saratani ilipo na kwamba wakati wa upasuaji sehemu iliyoathiriwa au koo
lote vinaweza kuondolewa.
Hata
hivyo anafafanua kuwa kabla upasuaji haujafanyika, daktari hujadiliana
na mgonjwa wake kumweleza ni aina gani ya upasuaji utakaofanyika, faida
na hasara zake, na nini cha kutarajia kutokana na upasuaji huo.
“Kuna
aina ya tiba inayotumia mionzi yenye nishati kubwa kuua seli
zilizoathiriwa na saratani. Kwa kawaida tiba ya mionzi huathiri seli
zilizo katika eneo linalotibiwa tu.
Pia tiba ya mionzi inaweza pia kutumika kuua seli za saratani zilizobakia mara baada ya kufanyika kwa upasuaji,” anasema.
Anaitaja
aina ya tatu kuwa ni tiba ya kemikali (Chemotherapy), akisema: “Tiba
hii hutumia kemikali kuua seli zenye saratani. Kwa kawaida dawa hizi
hutolewa kwa njia ya sindano kupitia kwenye mshipa wa damu wa vein.”
Tafiti nyingine duniani
Tafiti
zilizofanyika katika nchi mbalimbali zimeonyesha kuwa India ndiyo nchi
inayoongoza kwa Saratani ya Koo kuua watu wengi kwa mwaka hali
inayoelezwa kutokana na aina za vyakula vinavyoliwa na jamii hiyo,
ikiwamo pilipili kwa wingi.
Tafiti
zinaeleza kuwa watu 17,460 kutoka nchini humo kati yao 13,950 wanaume
na 3,510 wanawake, wamekufa mwaka 2012 kutokana na Saratani ya Koo.
SOURCE::MWANANCHI::
No comments:
Post a Comment