ASKARI Polisi wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU) mkoani Kilimanjaro wanaolinda mipaka kukabiliana na
biashara za magendo zisiende Kenya, wanadaiwa kuacha lindo na kutinga
ukumbi wa disko wakiwa na silaha nzito za kivita aina ya SMG.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Aprili 20 mwaka huu,
ambapo askari hao zaidi ya watano waliingia katika ukumbi wa disko wa
High Way uliopo njia panda ya Himo na hivyo kutoa mwanya kwa magari sita
aina ya Fuso yaliyokuwa yamesheheni sukari ya magendo kupita kirahisi
kwenda nchini Kenya.
Mbali na askari hao, pia maofisa wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) nao huweka doria katika barabara hiyo ya Mwika,
lakini siku hiyo waliungana na askari wale katika ukumbi wa disko na
kuacha magari hayo yakienda Kenya bila kukaguliwa.
Hata hivyo, raia
wema waliwasiliana na waandishi wa habari za uchunguzi ambapo magari
mawili yalijikuta mikononi mwa wananchi huku moja likiwaponyoka baada ya
dereva wake kukimbia na kwenda kulificha katika mji mdogo wa Himo.
Gari lililobaki mikononi mwa wananchi wakiwamo pia
waandishi wa habari za uchunguzi lilikuwa na namba za usajili T 695 BXH
aina ya Fuso mali ya Susan Bahati Paul wa Moshi Mjini ambalo
lilibainika kusheheni sukari kutoka nchini Thailand.
Gari hilo ambalo lilikuwa mita chache kuingia
nchini Kenya kupitia eneo la machimbo ya mchanga aina ya pozolana,
lilikabidhiwa kwa maofisa wa TRA katika kituo cha forodha cha Holili
likiwa na mifuko 250 ya sukari yenye ujazo wa kilo 50 kia moja.
Alipoulizwa jana juu ya askari wake kwenda
kustarehe disko na kuacha sukari ikienda Kenya, Kaimu Kamanda wa Polisi
mkoani Kilimanjaro, Koka Moita pamoja na kudai hana taarifa, aliahidi
kulishughulikia suala hilo.
Wakati Moita akidai hana taarifa, habari za ndani
ya Jeshi la Polisi zimedokeza kuwa askari wote waliokuwa zamu mpakani
hapo usiku wa kuamkia Aprili 20 mwaka huu, wamehojiwa juu ya tuhuma za
kuachia magari hayo yaliyosheheni sukari ya magendo.
Taarifa hizo zimedokeza kuwa askari hao waliokuwa
kwenye magari mawili ya FFU, waliitwa na kuhojiwa ofisini kwa mkuu wa
upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Kilimanjaro (RCO), Ramadhan
Ng’anzi.
Zaidi ya magari
kumi aina ya Fuso yaliyosheheni sukari ya magendo yamekuwa yakivuka
mpaka kwenda nchini Kenya kila siku kutoka katika mji mdogo wa Himo
kupitia njia ya Kwa Hussein hadi yalipo machimbo ya mchanga aina ya
pozolana mita chache kutoka kituo cha forodha cha Holili na kuingia
nchini Kenya kirahisi.
No comments:
Post a Comment