Thursday, March 07, 2013

Prof. Maghembe alichefua kanisa

WAZIRI wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, amelaumiwa na uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa kwa kushindwa kuingilia kati mgogoro wa maji uliopo kati ya mwekezaji wa mashamba ya mpunga Mbarali na Shule ya Sekondari ya Kilimo ya Montfort ambayo inauziwa 
maji ili kuweza kulima. 

Kuibuliwa kwa tuhuma hizo zilizoelekezwa moja kwa moja kwa Waziri Maghembe kunafuatia barua kadhaa zilizoandikwa kwenda wizarani na uongozi wa kanisa hilo na ule wa shule hiyo pasipo kujibiwa na serikali licha ya uwekezaji wa kanisa ulilenga zaidi kuwaendeleza vijana. 

“Bado tunaumizwa sana na suala la maji, tumeipigia sana magoti serikali ili itusaidie tupate maji ya kutosha. Shule yetu ni ya mchepuo wa kilimo, ilisajiliwa tukijua kuwa tutalima kwa vitendo baada ya kujiridhisha kuwa maji yapo, tangu apewe mwekezaji ameamua kutuuzia maji,” alilalamika Mkuu wa Shule hiyo, Ansgar Kigane. 


Kigane alisema kuwa tangu shule hiyo ilipoanzishwa miaka 25 sasa imefanya vizuri sana kwenye masomo ya kilimo kutokana na upatikanaji wa maji uliokuwa ukitolewa na Shirika la Kilimo na Chakula (NAFCO) kabla ya kubinafsishwa. 



“Kwa kuwa shule yetu ni ya kilimo hasa mpunga na kwa kuwa wanafunzi waliweza kulima na kupata mavuno ya kutosha ilikuwa rahisi kwao kupata chakula bure shuleni, sasa hali imekuwa ngumu, mwaka huu imebidi tununue maji kutoka kwa mwekezaji kwa masharti magumu,” alisema. 


Alibainisha kuwa licha ya jitihada kubwa za kuiomba Wizara ya Maji iingilie kati ili kuona uwezekano wa shule hiyo kupata maji kwa kupitia mfereji mdogo ulioruhusiwa wakati wa NAFCO, lakini wamekosa majibu sahihi. 


Ofisa Maji Mkuu wa Bonde la Rufiji ambao ndio wenye mamlaka ya kusimamia maji katika Bonde la Usangu, Idrissa Msuya alisema kwa mujibu wa sheria ya maji, mwekezaji aliyepewa kibali cha kuyatumia haruhusiwi kuyauza na kwamba makubaliano yaliyofikiwa ni uamuzi wa pande mbili ambazo haziihusu mamlaka hiyo. 


Msuya alisema kuwa mvutano huo wa maji umefumuka baada ya serikali kubinafsisha mashamba ya NAFCO kwani huko nyuma hali haikuwa hivyo na kwamba mamlaka hiyo imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuleta suluhu ila anashangaa kwanini hawakubaliani. 


Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa, katika barua zake amekuwa akifanya jitihada kubwa za kuipigia magoti serikali ili iweze kuiruhusu shule hiyo ipewe kibali cha kutumia maji kutoka kwenye mfereji wa umma uliojengwa na serikali. 


SOURCE::TANZANIA DAIMA::

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...